杏MAP导航

Tafuta

Shirika la Wamisionari Wabenediktin wa Tutzing lilianzishwa kunako mwaka 1885 huko Reichenbach, nchini Ujerumani na Padre Andreas Amrhein. Shirika la Wamisionari Wabenediktin wa Tutzing lilianzishwa kunako mwaka 1885 huko Reichenbach, nchini Ujerumani na Padre Andreas Amrhein.   (Missionary Benedictine of Tutzing)

Watawa Wabenediktini wa Tutzing: Uongozi Ni Huduma ya Upendo

Hayati Baba Mtakatifu Francisko: Kanisa linawahitaji viongozi wanaoweza kujisadaka katika maisha yao kwa ajili ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza Watu wa Mungu, kwa kutambua kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma kwa ajili ya kutekeleza mapenzi ya Kristo Yesu kwa ndugu zake, kwa kujikita katika upendo na unyenyekevu; uvumilivu na udumifu, ili Familia ya Mungu iweze kukua, kutembea, kujenga na kumshuhudia Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu.

Na Sr. Bonifasia Ngonyani, OSB, - Roma, Italia.

Hayati Papa Francisko anasema: Kanisa linawahitaji viongozi wanaoweza kujisadaka katika maisha yao kwa ajili ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza Watu wa Mungu, kwa kutambua kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma kwa ajili ya kutekeleza mapenzi ya Kristo Yesu kwa ndugu zake, kwa kujikita katika upendo na unyenyekevu; uvumilivu na udumifu, ili Familia ya Mungu iweze kukua, kutembea, kujenga na kumshuhudia Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu. Tangu mwanzoni mwa Kanisa walikuwepo watu, wanaume na wanawake, ambao kwa kutekeleza mashauri ya kiinjili walinuia kumfuata Kristo kwa hiari zaidi na kumwiga kwa karibu, na walienenda, kila mmoja kwa jinsi yake, katika maisha ya wakfu kwa Mungu. Wengi miongoni mwao, kwa kufuata msukumo wa Roho Mtakatifu, waliishi maisha ya upweke, au walianzisha familia za kitawa, ambazo Kanisa kwa mamlaka yake lilizikubali kwa moyo na kuziidhinisha. Hivyo, kwa mpango wa kimungu, wingi wa ajabu wa mashirika ya kitawa ukasitawi, nayo yamechangia sana ili Kanisa lisiwe tu limekamilishwa lipate kutenda kila tendo jema (taz. 2Tim 3:17), na liwe limeandaliwa hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe (taz. Efe 4:12), bali pia, liwe linapendeza kwa wingi wa karama mbalimbali za wanae, nalo lionekane pia kama bibiarusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe (taz. Ufu 21:2), na kwa njia yake hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane (taz. Efe 3:10).

Sr. Rosann Ocken, OSB, Mama Mkuu wa Wamisionari wa Tutsing
Sr. Rosann Ocken, OSB, Mama Mkuu wa Wamisionari wa Tutsing   (Missionary Benedictine of Tutzing)

Katika wingi huu wa karama, wale wote wanaoitwa na Mungu kutekeleza mashauri ya kiinjili na kuyatimiza kiaminifu, wanajiweka wakfu kwa Bwana kwa namna ya pekee, kwa kumfuasa Kristo ambaye, akiwa bikira na maskini (taz. Mt 8:20; Lk 9:58), aliwakomboa wanadamu na kuwatakatifuza kwa njia ya utii wake mpaka kufa msalabani (taz. Flp 2:8). Vivyo hivyo nao watu, walihimizwa na pendo ambalo Roho Mtakatifu amemimina mioyoni mwao (taz. Rum 5:5) wanaishi zaidi na zaidi kwa ajili ya Kristo na kwa ajili ya Mwili wake ulio Kanisa (taz. Kol 1:24). Kwa hiyo, kama wanavyojiunga kwa ari na Kristo kwa njia ya kujitolea kwao maisha yote, ni kadiri hiyohiyo maisha ya Kanisa yananufaika na utume wake unazidi kuwa na nguvu za kuleta matunda. Rej. Mapendo kamili (Perfectae caritatis), 1. Shirika la Wamisionari Wabenediktin wa Tutzing lilianzishwa kunako mwaka 1885 huko Reichenbach, nchini Ujerumani na Padre Andreas Amrhein. Mwaka 1887, Shirika lilihamisha makao yake toka Reichenbach kwenda St. Ottilien, Jimboni Augsburg. Kwa mara nyingine tena, hapo mwaka 1904 Shirika lilihamishia Makao ya Nyumba mama toka St. Ottilien kwenda Tutzing, Ujerumani. Katika miaka 140, Shirika limeenea na kufanya utume wake kwenye Mabara makuu matano duniani ambayo ni: Afrika, Ulaya, Asia, Amerika ya Kaskazini na Amerika ya Kusini. Barani Afrika, Shirika linafanya utume wake huko nchini: Kenya, Uganda, Namibia, Angola na Tanzania. Tanzania lina nyumba kuu mbili huko: Peramiho Jimbo kuu la Songea na Ndanda Jimbo la Mtwara. Makao makuu ya Shirika yako Roma ambapo Mama Mkuu wa Shirika na Halmashauri yake wanaishi na kufanya utume wao kwa ajili ya Shirika.

Wamisionari Wabenediktin wa Tutzing, wakishuhudia furaha ya Injili
Wamisionari Wabenediktin wa Tutzing, wakishuhudia furaha ya Injili

Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Kanisa linawahitaji viongozi wanaoweza kujisadaka katika maisha yao kwa ajili ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza Watu wa Mungu, kwa kutambua kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma kwa ajili ya kutekeleza mapenzi ya Kristo Yesu kwa ndugu zake, kwa kujikita katika upendo na unyenyekevu; uvumilivu na udumifu, ili Familia ya Mungu iweze kukua, kutembea, kujenga na kumshuhudia Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu. Viongozi wa Kanisa waoneshe dira na njia ya kufuata kwa mfano na ushuhuda wa maisha yao. Waamini hawawapendi anasema Baba Mtakatifu Francisko, viongozi wenye dharau wasiowajali watu, wanaowaangalia maskini kama "soli ya kiatu"! Viongozi wajitaabishe kuwapenda, kuwafahamu kwa majina waamini wao na kuwasaidia kukua na kukomaa katika maisha ya kiroho na kiutu! Viongozi wawe karibu na waamini wao kwa njia ya huduma makini, katika hali ya unyenyekevu, kiasi na sadaka. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anawataka viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanakuwa na uwiano mzuri wa maisha na utume wao kwa kujikita katika Sala, Ibada ya Misa Takatifu na baadaye utume; baada ya kujitajirisha katika Neno la Mungu, linalokuwa ni dira na mwongozo wa siku. Baba Mtakatifu anasema, uinjilishaji mpya unawahitaji watu wenye uwezo wa kutolea ushuhuda amini imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Uinjilishaji mpya ni dhana inayojikita katika utakatifu wa maisha kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utukufu wa Mungu na heshima kwa binadamu kwa kujenga umoja, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu.

Wamisionari Wabenediktin wa Tutzing wakisali
Wamisionari Wabenediktin wa Tutzing wakisali

Ni katika muktadha wa uongozi kama huduma ya upendo, Mwaka 2024 katika Makao makuu ya shirika mjini Roma, mwezi wa kumi na moja, walikusanyika wajumbe nawawakilishi toka nyumba zote za Shirika kwa ajili ya mkutano mkuu na uchaguzi wa viongozi wa Shirika, yaani Mama Mkuu na Halmashauri yake na kusimikwa rasmi mnamo tarehe 20 Januari 2025. Shirika linawashukuru sana Mama Mkuu, Sr. Maoro Sye, OSB aliyemaliza kipindi chake cha uongozi na Halmashauri yake kwa kazi ya kulionongoza Shirika letu katika miaka sita iliyopita. Kisha Shirika linamkaribisha na kumwombea Mama Mkuu mpya, Sr. Rosann Ocken, OSB na Halmashauri yake hekima na uchaji wa Mungu ili kuliongoza Shirika letu kadiri ya nyakati za sasa na mpango wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema, Siku ya 62 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa kwa mwaka 2025 anasema, wito ni zawadi ya thamani ambayo Mungu hupanda mioyoni, wito wa kutoka ndani ya nafsi yako ili kuanza safari ya upendo na huduma. Na kila wito katika Kanisa uwe wa waamini walei au wa huduma ya maisha ya wakfu ni ishara ya tumaini ambalo Mungu analo kwa ulimwengu na kwa kila mmoja wa watoto wake. Katika Ulimwengu mamboleo, vijana wengi wanahisi kupotea, hawana uhakika na fursa za ajira; wanakosa utambulisho na mwelekeo wa kimaadili; kuna udhalimu mkubwa kwa wanyonge na maskini, vita, vurugu na kinzani mbalimbali, lakini Kristo Yesu anapenda kuwahamasisha waja wake kutambua kwamba, anapendwa, anaitwa na kutumwa kama msafiri wa matumaini.

Malezi na majiundo ya kitawa ni muhimu sana
Malezi na majiundo ya kitawa ni muhimu sana

Viongozi wa Kanisa wanahimizwa na Hayati Baba Mtakatifu Francisko kuwakaribisha, kutambua na kuwasindikiza vijana wa kizazi kipya kwa ufundi na ustadi mkuu. Vijana ni wahusika wakuu, kwa kushirikiana na Roho Mtakatifu ambaye huamsha ndani yao hamu ya kufanya maisha yao kuwa ni zawadi ya upendo. Kumbe, tunapo uombea uongozi mpya ufanisi bora wa kazi, tunamwomba Mwenyezi Mungu atuongezee miito ya kutosha ili kuleta ufanisi bora katika kazi zetu za kitume yaani kumkomboa mwanadamu kiroho na kimwili ili hatimaye Mwenyezi Mungu atukuzwe katika yote. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa liko hai na linazaa matunda linapozalisha miito mipya; kwa hakika ulimwengu unatafuta mashuhuda wa matumaini, wanaothubutu kutangaza na kushuhudia kwa njia ya maisha yao kwamba, kumfuasa Kristo Yesu ni chanzo cha furaha na kwamba, Bwana wa mavuno anaendelea kuwaita vijana wengi kwa upendo, changamoto na mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya ni kuendelea kutembea kama mahujaji wa matumaini katika tunu msingi za Kiinjili. Tunawakaribisha akina dada wote ambao wanavutwa katika kumtumikia Mungu na jirani kupitia Shirika letu la Wamisionari Wabenediktin wa Tutzing karibu sana hasa Tanzania katika nyumba ya Peramiho na Ndanda njooni kwa pamoja tuutafute utakatifu na ukamilifu wa maisha.

Wabenediktini Tutzing
21 Mei 2025, 14:26