杏MAP导航

Tafuta

Sote tunaona jinsi gani kuanzia vipindi vya mazungumzo ya televisheni hadi mashambulizi ya maneno kwenye mitandao ya kijamii kuna hatari kwamba dhana ya ushindani,upinzani,nia ya kutawala na kumiliki,na upotoshaji wa maoni ya umma itashinda. Sote tunaona jinsi gani kuanzia vipindi vya mazungumzo ya televisheni hadi mashambulizi ya maneno kwenye mitandao ya kijamii kuna hatari kwamba dhana ya ushindani,upinzani,nia ya kutawala na kumiliki,na upotoshaji wa maoni ya umma itashinda.  (Hermínio José)

Siku ya Upashanaji Habari Ulimwenguni:kupokonya silaha na mawasiliano yasiyoleta mvutano!

“Ninapotafakari juu ya Jubilei tunayoadhimisha mwaka huu kama wakati wa neema katika nyakati hizi za taabu,ningependa katika Ujumbe huu kuwaalika kuwa'wanamawasiliano wa matumaini,'kuanzia upyaishaji wa kazi na utume wenu katika roho ya Injili.”Ni kutoka Ujumbe wa Siku ya Upashanaji Habari ulitolewa na Hayati Papa Francisko,Januari 24,katika kumbukizi ya Msimamizi wa Waandishi wa Vyombo vya habari kwa ajili ya kilele cha Siku hiyo tarehe 1 Juni 2025.

Na sarah Pelaji - Vatican.

Wawasilianaji wa upole katikati ya vita vilivyotengenezwa kwa maneno ambayo mara nyingi huwasha cheche za vita vinavyotengenezwa na mabomu na damu. Wanawake na wanaume sawa na kwa wachimba dhahabu kuwinda “cheche za mema” za kihistoria zinazopanua moyo na kuzalisha udugu huku zikiondoa kutojali, kutoaminiana na chuki. Kwa kifupi wawasilianaji wa matumaini popote walipo wanaweza kuweka kiota. Hivyo ndivyo ndoto ya kuona wataalamu wa vyombo vya habari katika mwaka wa Jubilei 2025. Baba Mtakatifu Fransisko alisema  hayo katika ujumbe wake wa siku ya 59 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni uliochapishwa siku ya Ijumaa tarehe 24 Januari 2025, katika siku ambayo Mama Kanisa anafanya kumbukumbu ya Mtakatifu Francis wa Sales, Msimamizi wa Waandishi wa Vyombo vya Habari. Na ujumbe wake kwa Mwaka huu  unaoongoza na kauli mbiu iliyotolewa katika kifungu cha Barua ya Kwanza ya Mtakatifu Petro kisemacho: “Shirikishaneni kwa upole matumaini yaliyomo moyoni mwenu (IPt3;15-16).”

Kutumia vyombo vya habari hata kwa simu
Kutumia vyombo vya habari hata kwa simu   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Jubilei ni Mwaka wa neema

Ni katika ujumbe  wa  kilele cha Siku hiyo ya Upashanaji habari, ambayo kwa mwaka huu ni  tarehe 1 Juni 2025 ambapo, pamoja na mambo mengine Papa Fransisko alisisitiza kuhusu mawasiliano yeletayo matumaini. “Katika nyakati hizi zinazotawaliwa na upotoshaji wa habari na mgawanyiko, ambapo vituo vichache vya mamlaka vinadhibiti wingi takwimu na taarifa, ningependa kuzungumza nanyi kama mtu anayejua na kuthamini  umuhimu wa kazi yenu kama wanahabari na wataalamu wa mawasiliano. Juhudi zenu za ujasiri za kuweka uwajibikaji binafsi na wa pamoja kwa wengine katikati ya mawasiliano ni muhimu sana,” alibainisha Papa Francisko. Kwa kuongeza: “Ninapotafakari juu ya Jubilei tunayoadhimisha mwaka huu kama wakati wa neema katika nyakati hizi za taabu, ningependa katika Ujumbe huu kuwaalika kuwa  “wanamawasiliano wa matumaini”, kuanzia upyaishaji wa  kazi na utume wenu katika roho ya Injili,” alisema.

Habari za upotoshaji zinaharibu sura ya kila kitu.Tutoe habari zinazostahili bila kusababisha mivutano
Habari za upotoshaji zinaharibu sura ya kila kitu.Tutoe habari zinazostahili bila kusababisha mivutano

Mawasiliano ya kupunguza mvutano

Baba Mtakatifu Francisko alizidi kukazia kuwa “Leo hii, Katika nyakati hizi mara kwa mara mawasiliano yetu hayaleti wala kuzalisha tumaini, bali hofu na kukata tamaa, chuki na hasira, upendeleo na hata uhasama. Mara nyingi, mawasiliano ya sasa huondoa  ukweli ili kuchochea majibu ya kihisia; hutumia maneno ambayo ni kama kisu; hutumia taarifa za uongo au zilizopotoka kutuma ujumbe unaokusudiwa ili  kuchochea, kuchukiza au kuumiza. Mara kadhaa, nimezungumzia kuhusu haja yetu ya "kupokonya silaha yaani kufanya mawasiliano yasiyoleta mvutano ambayo yanayolenga kufuta uhasama. Hakusaidii kamwe kupunguza ukweli kuwa misamiati rahisi.  Sote tunaona jinsi gani - kuanzia vipindi vya mazungumzo ya televisheni hadi mashambulizi ya maneno kwenye mitandao ya kijamii - kuna hatari kwamba dhana ya ushindani, upinzani, nia ya kutawala na kumiliki, na upotoshaji wa maoni ya umma utashinda.”

Migawanyiko iliyopangwa

Baba Mtakatifu alisisitiza kuwa pia kuna jambo jingine la kusikitisha: kwa kile tunachoweza kuita “mgawanyiko uliopangwa ama ulioratibiwa kwa umakini  kupitia mifumo ya kidijitali ambayo, kwa kutuchanganua kulingana na mantiki ya soko, hubadilisha mtazamo wetu wa uhalisia. Matokeo yake ni kwamba tunashuhudia, mara nyingi bila msaada, aina fulani ya mgawanyiko wa maslahi unaoishia kuhujumu misingi ya uwepo wetu kama jamii, uwezo wetu wa kushirikiana katika kutafuta manufaa ya pamoja, kusikilizana, na kuelewana kutoka mitazamo tofauti.” Mwasilishaji mzuri huhakikisha kuwa wasikilizaji, wasomaji au watazamaji wanaweza kushiriki, wanaweza kusogea karibu, wanaweza kuguswa na sehemu bora zaidi ya nafsi zao na kuingia katika hadithi zinazoelezwa wakiwa na mitazamo hii. Mawasiliano ya namna hii hutusaidia kuwa “mahujaji wa matumaini”, ambao ndiyo kauli mbiu ya Jubilei ya sasa.

Kuandika na kuhabarisha taarifa za matumaini
Kuandika na kuhabarisha taarifa za matumaini

Matokeo mengi ya Jubilei

Jubilei ina athari nyingi za kijamii. Tunaweza kufikiria, kwa mfano, ujumbe wake wa huruma na tumaini kwa wale wanaoishi magerezani, au wito wake wa ukaribu na upole kwa wale wanaoteseka na walioko pembezoni mwa jamii. Yubilei inatukumbusha kuwa wapatanishi wataitwa wana wa Mungu” (Mathayo 5:9), na kwa njia hii inatia tumaini, inatuelekeza kwenye hitaji la mawasiliano makini, yenye upole na tafakuri, yenye uwezo wa kuonesha njia za mazungumzo. Kwa sababu hii, ninawahimiza kugundua na kutangaza simulizi nyingi za wema zilizojificha katika mifumo ya habari, kwa kuiga wale wanaotafuta dhahabu ambao kwa bidii huchuja mchanga wakitafuta chembe ndogo ya dhahabu.  Ni jambo jema kutafuta mbegu kama hizo za tumaini na kuzitangaza. Husaidia dunia yetu kuwa na usikivu zaidi kwa kilio cha masikini, kuwa na huruma zaidi, na kuwa na uwazi zaidi. Daima mpate mng’ao huo wa wema unaotutia moyo kuwa na tumaini. Mawasiliano ya aina hii yanaweza kusaidia kujenga muungano, kutufanya tuhisi sisi wenyewe kidogo, na kutufanya tugundue tena umuhimu wa kutembea pamoja, alisisitiza

Muitunze mioyo yenu ambayo ni maisha yenu ya ndani

Papa Fransisko alisema kuwa, licha ya kuwa maendeleo na faida za teknolojia, anawahimiza wana mawasiliano kuitunza mioyo ambayo ni maisha yao  ya ndani. Hii inamaanisha nini? Kuwa wapole na kamwe wasisahau wengine; wazungumzie kuhusu mioyo ya jamii (wanawake na wanaume) mnaowahudumia katika kazi zao. Msiruhusu hisia za kisilika kuongoza   mawasiliano yenu. Daima mueneze  matu maini, hata katika nyakati  ngumu, hata pale hali inapogharimu maisha yenu na  kuonekana kutokuwa na matokeo chanya. Jaribuni kukuza mawasiliano yanayoweza kuponya majeraha ya ubinadamu wetu. Toeni nafasi ya uaminifu kutoka moyoni mwenu  ambayo ni kama ua jembamba lakini imara, linalostahimili ambalo halishindwi wala kuharibiwa na dhoruba za maisha, bali huchanua na kukua katika sehemu zisizotarajiwa.

Papa Francisko daima alizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara zake za kitume
Papa Francisko daima alizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara zake za kitume

“Ni pale lilipo tumaini la akina mama wanaoomba kila siku kuwaona watoto wao wakirejea salama kutoka vitani na katika tumaini la akina baba wanaohatarisha maisha yao kwa kusafiri na kuwa wahamiaji katika maeneo mbalimbali ili kutafuta maisha bora. Lipo pia tumaini la watoto wanaoendelea kucheza, kucheka, na kuamini katika maisha hata katikati ya madhara ya vita na katika kuishi kwenye jamii iliyojawa na umasikini,” alikazia katika ujumbe huo. Kwa kuhitimisha, Baba Mtakatifu ujumbe huo alibainisha kuwa, “kuweni mashuhuda na waendelezaji wa mawasiliano yasiyo na fujo; saidieni kueneza utamaduni wa kujali, kujenga madaraja na kubomoa kuta zinazonekana na zisizoonekana za nyakati hizi. Simulieni historia zilizojaa tumaini, mjali hatima yetu ya pamoja na jitahidini kuandika kwa pamoja historia ya maisha yetu ya baadaye. Haya yote mnaweza kufanya, nasi tunaweza kufanya, kwa neema ya Mungu, ambayo Jubilei hutusaidia kuipokea kwa wingi. Hili ndilo ombi langu, na pamoja nalo, nawabariki kila mmoja wenu na kazi yenu.”

Waandishi wa habari wa Vatican katika moja ya tamasha la Mediteranea
Waandishi wa habari wa Vatican katika moja ya tamasha la Mediteranea
Siku ya upashanaji habari
31 Mei 2025, 09:47