Gallagher akutana na makamu rais wa Zimbabwe
Vatican News
Katika taarifa tunayosoma kutoka katika Ofisi ya vyombo vya habari vya Vatican imerejea juu ya mkutano wa asubuhi ya tarehe 3 Mei 2025 mjini Vatican, kati ya Jenerali Constantino Guveya Dominic Nyikadzino Chiwenga, makamu wa rais wa nchi ya Zimbabwe na Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu wa Vatican wa Mahusiano na Mataifa na Mashirika ya Kimataifa kwamba: “Wakati wa majadiliano ya dhati, uhusiano mzuri kati ya Vatican na Jamhuri ya Zimbabwe ulibainishwa.”
Mkutano huo pia ulijadili baadhi ya vipengele vya hali ya kisiasa na kijamii na kiuchumi ya nchi, hasa kuhusu ushirikiano na Kanisa mahalia katika nyanja ya elimu na afya. Kulikuwa na mabadilishano ya maoni pia kuhusu masuala ya kikanda na kimataifa, yakionesha umuhimu wa kukuza mazungumzo na maridhiano kati ya watu.