Askofu Msaidizi Josaphat Jackson Bududu Jimbo Kuu Katoliki Tabora
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Vigezo muhimu vinavyopaswa kuzingatiwa kwa mtu kuteuliwa kuwa Askofu, kama msimamizi wa mafumbo ya Kanisa na wala si mtawala anayeelemewa na uchu wa mali na madaraka. Askofu anapaswa kuwa ni wakili wa Mungu na kiongozi anayejiaminisha na kutembea mbele ya Mungu; Mkatoliki, mkomavu wa kisaikolojia na maisha ya kiroho. Askofu anapaswa kuwa ni mtu wa Mungu; mtu wa watu na asiyependa makuu. Lakini, kimsingi Askofu anapaswa kuwa mtu: mkarimu, mnyenyekevu, mpole na ambaye yuko tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu. Huu ni mwongozo unaoobubujika kutoka katika Neno la Mungu na ambao unapaswa kufuatwa. Askofu anapaswa kuwa ni kielelezo cha ukaribu wa Mungu kwa waja wake: Ukaribu kwa watu wa Mungu, Mapadre na Maaskofu: Uongozi ndani ya Kanisa ni huduma ya huruma na upendo inayosimikwa katika mchakato wa ujenzi wa umoja, ushiriki na utume wa Kanisa, mambo msingi katika ujenzi wa Kanisa la Kimisionari na Kisinodi.
Katiba mpya ya Kitume: “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu” inabainisha umuhimu wa kuwashirikisha watu wa Mungu katika uteuzi wa Maaskofu, jambo muhimu sana na dhamana inayotekelezwa sasa na Balozi za Vatican kwenye Makanisa mahalia. Huu ni wajibu wa kuwasikiliza waamini walei na watawa ili kupata maoni yao juu ya Askofu mtarajiwa. Ni katika muktadha huu, Askofu Msaidizi Josephat Jackson Bududu wa Jimbo kuu la Tabora, Dominika tarehe 25 Mei 2025 Mwaka wa Bwana, Mwaka wa maadhimisho ya Jubilei ya matumaini, anawekwa wakfu kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu la Tabora. Hili ni tukio linalotanguliwa na Masifu ya jioni, yatakayofanyika Jumamosi tarehe 24 Mei 2025 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, Jimbo kuu la Tabora. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican Askofu Msaidizi Josaphat Jackson Bududu anasimulia historia ya maisha na wito wake, Shukrani zake za dhati na kwamba, Daraja Takatifu ni wito wenye madai yake. Askofu Msaidizi Josaphat Jackson Bududu anaongozwa na kauli mbiu: “Mapenzi yako yatimizwe”: na kwa lugha ya Kilatini: "Fiat voluntas tua" Mt 26:42. Anasema, amepokea dhamana na wajibu huu kwa mshangao mkubwa, kwa hofu na kutetemeka kutoka na utakatifu wa utume wenyewe, lakini anaendelea kujikabidhi mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Anayakumbuka maneno ya Askofu mkuu Angelo Accattino, Balozi wa Vatican nchini Tanzania kwamba, yeye ni kati ya Maaskofu wenye umri mdogo sana, yaani miaka 48 kwenye Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, changamoto ni kuendelea kujisadaka zaidi katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa: Kufundisha, Kuongoza na Kuwatakatifuza watu wa Mungu.
Askofu Msaidizi Josaphat Jackson Bududu katika historia ya maisha na wito wake anasema, alivutiwa sana kuwa ni Mwanasheria, Hakimu na Polisi, lakini kadiri ya miaka ilivyokuwa inayoyoma, kiu na hamu ya kutaka kuwa Padre ilizidi kushika kasi. Hii inatokana na mazingira ya Parokiani kwake, yaani Parokia ya Mtakatifu Anthony wa Padua, Jimbo kuu la Tabora, iliyokuwa ikiendeshwa wakati huo na Wamisionari wa Afrika, “White Fathers” kiasi cha kuvutiwa kuhudhuria Ibada na hatimaye, akawa ni mtumishi Altareni. Kristo Yesu katika maisha na utume wake alijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kushuhudia na kutangaza Habari Njema ya Wokovu na hatimaye kusimika Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano. Akawachagua Mitume wake kumi na wawili ili kusaidia mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, huku wakisaidiwa na wafuasi wengine 72 waliotumwa kwenda kumwandalia Kristo Yesu, mazingira ya uinjilishaji. Alhamisi Kuu, siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, Kristo Yesu aliweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Daraja Takatifu, kielelezo cha huduma makini inayomwilishwa katika Injili ya upendo na huduma. Yesu aliwapatia Mitume wake jukumu la kuwa ni: Manabii ili wahubiri Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa; Makuhani ili waweze kuwatakatifuza Watu wa Mungu kwa sala, sadaka na ushuhuda wa maisha yao; na Wafalme kwa kuwaongoza watu wa Mungu.
Askofu Msaidizi Josaphat Jackson Bududu anasema, Upadre ni wito unaodai sadaka na majitoleo, chemchemi ya upendo na huduma kwa watu wa Mungu. Kumbe, vijana wanapaswa tangu mwanzo kutambua misingi, miiko na nidhamu ya maisha na wito wa Kipadre, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu. Askofu Msaidizi Josaphat Jackson Bududu anawahimiza watu wa Mungu kutumia kwa busara mitandao ya kijamii kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji, lengo likiwa ni kuwafikia watu wengi zaidi. Ili kufikia lengo hili, kuna haja kwa Maaskofu kuhakikisha kwamba, wanajinoa kikamilifu, wawe na busara ya kupima kile wanachotaka kurusha kwenye mitandao ya kijamii. Matumizi ya mitandao ya kijamii ni fursa ya uinjilishaji mpya lakini pia kuna hatari zake. Mawasiliano haya yanaweza kuleta hatari kwa ushirika wa Kanisa, ndiyo maana kuna haja ya kuwa na busara katika matumizi ya mitandao ya kijamii.Itakumbukwa kwamba, Askofu Msaidizi Josaphat Jackson Bududu alizaliwa tarehe 26 Machi 1977, huko Kaliua, Jimbo kuu la Tabora. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 25 Januari 2009 akapewa Daraja Takatifu ya Ushemasi kwa ajili ya Jimbo kuu la Tabora na Askofu mkuuPaulo Runangaza Ruzoka. Tarehe 9 Julai 2009 akapewa daraja takatifu ya Upadre na Askofu mkuu Paulo Runangaza Ruzoka. Tarehe 26 Februari 2025, Hayati Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu la Tabora. Amekwisha litumikia Kanisa kama Padre kwa muda wa miaka 15 na ushehe.