杏MAP导航

Tafuta

Waraka wa “Kristo Yesu, Mwana wa Mungu na Mkombozi: Miaka 1700 ya Maadhimisho ya Mtaguso wa Kwanza wa Kiekumene wa Nicea (325-2025.)” Waraka wa “Kristo Yesu, Mwana wa Mungu na Mkombozi: Miaka 1700 ya Maadhimisho ya Mtaguso wa Kwanza wa Kiekumene wa Nicea (325-2025.)”  

Waraka wa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu na Mkombozi: Miaka 1700 ya Mtaguso wa Nicea

Tume ya Taalimungu Kimataifa tarehe 3 Aprili 2025 imechapisha Waraka muhimu na kina unaobeba kichwa cha habari “Kristo Yesu, Mwana wa Mungu na Mkombozi: Miaka 1700 ya Maadhimisho ya Mtaguso wa Kwanza wa Kiekumene wa Nicea (325-2025.)” Lengo kuu ni kukumbuka asili na umuhimu wa Mtaguso wa Nicea lakini pia ni kuangazia amana na rasilimali za ajabu zilizohifadhiwa na kuendelea kupyaishwa kwa njia ya imani katika uinjilishaji mpya kwa sasa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

 Tume ya Taalimungu Kimataifa “The International Theological Commission (ITC)” iliyoanzishwa na Mtakatifu Paulo VI kunako tarehe 11 Aprili 1969 ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican sanjari na Sinodi za Maaskofu. Tume hii mechangia sana kuhusu: Dhana ya Sinodi; Sakramenti za Kanisa, Haki Msingi za Binadamu, Uhuru wa Kuabudu na Umoja wa Kanisa. Kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 1700 tangu Kanisa liadhimishe Mtaguso wa Kwanza wa Nicea yaani kuanzia Mwaka 325 hadi Mwaka 2025 Tume ya Taalimungu Kimataifa, tarehe 3 Aprili 2025 imechapisha Waraka unaojulikana kama “Kristo Yesu, Mwana wa Mungu na Mkombozi: Miaka 1700 ya Maadhimisho ya Mtaguso wa Kwanza wa Kiekumene wa Nicea (325-2025.) Tarehe 20 Mei 2025 Wakristo wote wanaadhimisha kumbukizi ya Miaka 1700 tangu kuzinduliwa kwa Mtaguso wa Nicea ambao ulifanyika Asia Ndogo kunako Mwaka 325.Huu ulikuwa ni Mtaguso wa kwanza wa Kiekumene kufanyika katika historia ya Kanisa na hivyo ukaibua imani ambayo ilikamilishwa na Mtaguso wa Kwanza wa Costantinopol ulioadhimishwa Mwaka 381 na hivyo kutoa dira na mwongozo wa imani ya Kanisa kwa Kristo Yesu. Maadhimisho haya yanafanyika ndani ya Mwaka wa Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo kwa kunogeshwa na mada “Kristo Tumaini Letu” na inaambatanishwa na maadhimisho ya Sherehe ya pamoja ya Pasaka ya Bwana kwa Wakristo wa Makanisa ya Mashariki na Magharibi. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusisitiza kwamba, wakati huuu wa kihistoria unaooneshwa la janga la vita pamoja na wasiwasi mkuu, kwa kutokuwa na uhakika na kile kilicho muhimu, kizuri zaidi na cha kuvutia na pia jambo la muhimu zaidi ni imani katika Kristo Yesu, iliyotangazwa huko Nicea na kwamba, kutangaza imani hii ni kazi msingi ya Kanisa.

Mtaguso wa kwanza wa Kiekumene wa NIcea ulifanyika mwaka 325
Mtaguso wa kwanza wa Kiekumene wa NIcea ulifanyika mwaka 325

Kwa kutambua hatua hii muhimu, Tume ya Taalimungu Kimataifa “The International Theological Commission (ITC)”, tarehe 3 Aprili 2025 imechapisha Waraka muhimu na kina unaobeba kichwa cha habari “Kristo Yesu, Mwana wa Mungu na Mkombozi: Miaka 1700 ya Maadhimisho ya Mtaguso wa Kwanza wa Kiekumene wa Nicea (325-2025.)” Lengo kuu si tu kukumbuka asili na umuhimu wa Mtaguso wa kwanza wa Nicea (ambao bila shaka una umuhimu mkubwa wa kihistoria kwa Kanisa lakini pia ni kuangazia amana na rasilimali za ajabu zilizohifadhiwa na kuendelea kupyaishwa kwa njia ya imani, hasa kwa kuzingatia mchakato wa uinjilishaji mpya, unaotekelezwa kwa sasa na Mama Kanisa. Zaidi ya hayo, Waraka huu unaonesha umuhimu wa utajiri wa rasilimali na amana hizi kwa njia inayowajibisha na ya pamoja ya kushughulikia mabadiliko makubwa katika historia ambayo yana athari zake: kimataifa kwa tamaduni na katika jamii. Kwa hakika imani inayodaiwa na Mtaguso wa Nicea inafugua upya macho kwa mshangao na wa kudumu wa ujio wa Mwana wa Mungu kati yetu. Ujio huu unawatia moyo waamini kupanua nyoyo na akili zao ili kukaribisha na kujihusisha na zawadi ya ufahamu huu wa kuamua juu ya maana na mawelekeo wa historia mintarafu mwanga wa Mwenyezi Mungu ambaye, kupitia kwa Mwanaye wa Pekee, kielelezo cha utimilifu wa maisha yake mwenyewe, huwafanya waamini kuwa ni washiriki katika maisha hayo kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, na hivyo kuwakirimia Roho wake Mtakatifu anayevuka vikwazo vyote: hii ni pumzi ya uhuru kutoka katika ubinafsi; uwazi katika mahusiano na mafungamano tayari kujikita katika ujenzi wa ushirika na wengine.

Ujenzi wa kanisa la Kisiondi ili kutemba kwa pamoja
Ujenzi wa kanisa la Kisiondi ili kutemba kwa pamoja   (Vatican Media)

Imani ambayo Mtaguso wa Nicea unaishuhudia na kuikabidhi kwa Kanisa ni ukweli wa Mwenyezi Mungu ambaye ni Upendo, ni Utatu Mtakatifu na anakuwa mmoja kati ya waamini wake katika Mwana. Ukweli huu ni kanuni halisi ya udugu wa kibinadamu kati ya watu wa Mataifa, na ndiyo kanuni ya mabadiliko ya historia mintarafu Sala ambayo Kristo Yesu aliielekeza kwa Baba yake wakati wa mkesha wa sadaka yake kuu kwa ajili ya uzima wa waamini wake “Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja.” Yn 17:22. Kanuni ya Imani ya Nicea ni kiini cha Imani ya Kanisa. Ni chemchemi ya maji ya uzima ili kuweza kuingia katika macho ya Kristo Yesu, mintarafu mtazamo ambao Mwenyezi Mungu, Aba, anao kwa watoto wake na katika kazi ya uumbaji, kuanzia dogo, maskini zaidi, aliyetengwa, ambaye Mwana wa Pekee wa Baba ambaye alifanyika “ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.” Rum 8:29, alijitambulisha nao kiasi kwamba, kadiri ya walivyowatendea ndugu zake walio wadogo, walimtendea yeye. Rej Mt 25:40. Waraka wa Tume ya Taalimungu Kimataifa haukusudiwi kuwa ni maandiko ya kitaalimungu tu, bali unatolewa kama kito cha thamani na muhtasari unaoweza kuwasindikiza watu kukua katika imani na kumwilishwa katika ushuhuda wa imani miongoni mwa Jumuiya ya Wakristo, unaimarisha ushiriki katika maisha ya kiliturujia pamoja na kuimarisha malezi na makuzi ya watoto wateule wa Mungu katika akili yao ya ushirikishwaji wa kitamaduni na kiimani, lakini pia kuongoza ushiriki wa imani katika tamaduni na maisha ya kijamii, hasa katika kipindi kinachoshuhudida mabadiliko makubwa. Jambo hili ni muhimu kwa Wakristo hasa wakati huu wanapopambana na changamoto za mabadiliko katika maisha.

Mungu ni upendo unaofumbatwa katika Utatu Mtakatifu
Mungu ni upendo unaofumbatwa katika Utatu Mtakatifu   (Vatican Media)

Jambo hili ni muhimu sana kwa sababu ilikuwa ni huko Nicea ambapo umoja na utume wa Kanisa ulioneshwa kwa mara ya kwanza kwa njia ya kielelezo katika ngazi ya Ulimwengu mzima. Na hiki ni kiini cha Nicea kuitwa Mtaguso wa kwanza wa kiekumene kwa njia ya “Sinodi” yaani “kutembea pamoja” ambao kimsingi ni utambulisho wa Kanisa. Ni katika muktadha huu Mtaguso wa Nicea unasimama kama kielelezo chenye mamlaka na msukumo katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, mchakato ambao leo hii Kanisa Katoliki linashiriki katika dhamiri yake ya kuishi kwa dhati kabisa wongofu wa ndani sanjari na mageuzi yakipigwa chapa na kanuni ya uhusiano na ushiriki wa utume wa Kanisa kama inavyobainishwa na “Hati ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu” iliyoridhiwa na Baba Mtakatifu Francisko. Ni katika muktadha huu, Tume ya Taalimungu Kimataifa “The International Theological Commission (ITC)” inatoa mwaliko kwa waamini kuhudhuria Siku Maalum ya kusoma Waraka huu: “Kristo Yesu, Mwana wa Mungu na Mkombozi: Miaka 1700 ya Maadhimisho ya Mtaguso wa Kwanza wa Kiekumene wa Nicea (325-2025) yanafanyika tarehe 20 Mei 2025 Kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana kilichoko Roma kwenye Ukumbi wa “Saint John Paulo II. 

Jubilei ya NICEA 1,700
03 Aprili 2025, 15:17