Mtumishi wa Mungu Askofu Mkuu Eduard Profitlich, S.J. Kutangazwa Kuwa Mwenyeheri 17 Mei 2025
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Alhamisi tarehe 4 Aprili 2025 akiwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa amekutana na kuzungumza na Rais Alar Karis wa Estonia. Katika mazungumzo yao, viongozi hawa wameridhishwa na uhusiano mwema wa kidiplomasia uliopo kati ya nchi hizi mbili. Wamepongeza na kushukuru mchango unaotolewa na waamini wa Kanisa Katoliki kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Estonia.
Viongozi hawa kwa pamoja wamemshukuru Mungu kwa Mama Kanisa kutia nia ya kumtangaza Askofu mkuu Eduard Profitlich, Myesuiti, shuhuda wa imani kuwa ni Mwenyeheri, tukio ambalo litaadhimishwa huko nchini Estonia tarehe 17 Mei 2025 na Kardinali Christoph Schoenborn, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Vienna, Austria. Askofu mkuu Eduard Profitlich, S.J. ni kiongozi aliyesadaka maisha yake bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu; kiongozi jasiri na shuhuda wa imani aliyeyamimina maisha yake kama ushuhuda amini wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Askofu mkuu Eduard Profitlich, S.J. Alifariki dunia kunako mwaka 1942 akiwa kwenye gereza la Kirov katika nchi za Muungano wa Kisovieti. Anakuwa ni Mwenyeheri wa kwanza kutoka nchini Estonia, kutangazwa baada ya mchakato wake kukamilika katika kipindi cha miaka ishirini na moja. Kardinali Pietro Parolin na Rais Alar Karis wa Estonia baadaye walijielekeza katika masuala ya Kimataifa na Kikanda kwa kuonesha matumaini yao ya vita nchini Ukraine kukoma na watu kuanza tena safari ya maisha yao.