杏MAP导航

Tafuta

Kwaresima ni mwaliko kwa watawa kutembea kwa pamoja katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikita katika mabadiliko na hivyo kuendelea kusoma alama za nyakati kwa pamoja Kwaresima ni mwaliko kwa watawa kutembea kwa pamoja katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikita katika mabadiliko na hivyo kuendelea kusoma alama za nyakati kwa pamoja  (Vatican Media)

Ujumbe Wa Kwaresima Kwa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Kwa Mwaka 2025

Sr. Simona Brambilla, M. C. Mwenyekiti mwenza wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume katika kipindi hiki cha Kwaresima anawaalika watawa kutembea kwa pamoja katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikita katika mabadiliko na hivyo kuendelea kusoma alama za nyakati, dhamana inayopaswa kutekelezwa katika umoja na wala si katika mang’amuzi ya mtu mmoja mmoja. Papa anawaalika watu wa Mungu kutembea kwa pamoja. Matumaini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2025 unanogeshwa na kauli mbiu “Tutembee kwa pamoja katika matumaini.” Kwaresima ni kipindi cha imani na matumaini; toba na wongofu wa ndani, ili kukumbatia na kuambata huruma na upendo wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa mtu mmoja mmoja na kama Jumuiya ya waamini. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufanya hija ya imani na matumaini, kama ilivyokuwa kwa Waisraeli, waliotembea Jangwani kwa muda wa miaka arobaini, wakapata fursa ya toba na wongofu wa ndani. Hii ni safari ya pamoja kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, kwa kutoka katika ubinafsi wao na hivyo kujielekeza katika ujenzi wa umoja kwa kujitambua kwamba, wao wote wamekuwa ni wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Rej. Gal 3:26-28, mwaliko wa kuweka nia ya kuweza kufikia lengo kwa kusikilizana katika upendo na uvumilivu. Kipindi cha Kwaresima ni fursa kwa watu wa Mungu kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikilizana, kwa kutembea na kufanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu; kwa kuonesha upendo na ukarimu kwa wahitaji zaidi, kwa njia ya toba na wongofu wa ndani mintarafu ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Watu wa Mungu wanaalikwa kutembea katika mwanga wa matumaini kwani “tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5, kiini cha ujumbe wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo na kwamba, hatima ya Kipindi cha Kwaresima ni maadhimisho ya ushindi wa Pasaka, kielelezo cha upendo mkamilifu.

Watawa wajitahidi kuishi kadiri ya mwanga na tunu za Kiinjili
Watawa wajitahidi kuishi kadiri ya mwanga na tunu za Kiinjili   (Vatican Media)

Baba Mtakatifu Francisko anasema, watawa wajitahidi kuishi mintarafu mwanga wa Injili kama ilivyokuwa siku ile Kristo Yesu alipong’aa uso wake mbele ya Mitume wake, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda wa matumaini kwa watu wa nyakati hizi. Wawe tayari “kufyekelea” mbali woga na wasiwasi unaoweza kuota mizizi yake hata katika maisha ya watawa kutokana na: uhaba wa miito; ukosefu wa uaminifu kwa Kristo Yesu, Injili na Kanisa. Kwa njia hii, wataweza kujisadaka zaidi kwa ajili ya kuchuchumilia utakatifu wa maisha kwa kuthamini na kuhimiza mwelekeo chanya katika jamii; kwa kuthamini na kudumisha upya unaobubujika kutoka katika tamaduni na maisha ya watu wanaowatangazia na kuwashuhudia Injili. Ili kuwa vyombo na mashuhuda wa matumaini wanapaswa kukoleza moyo wa majadiliano, umoja na udugu wa kibinadamu kama chemchemi ya utakatifu wa maisha. Watawa wawe na ujasiri wa kupambana na changamoto mamboleo kwa kuwa na matumizi sahihi na yanayowawajibisha kwa vyombo vya mawasiliano ya jamii; vinavyoweza wakati mwingine kuharibu: haki, utu na heshima ya watu; kwa kuchafua maisha ya kiroho pamoja na kujeruhi maisha ya kidugu katika jumuiya. Watawa wajitahidi kujifunza kutumia vyombo vya mawasiliano ya jamii kwa ajili ya kuinjilisha. Jumuiya za kitawa ziwe ni maabara ya utamadunisho, kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaowafumbata watu wote bila ya ubaguzi, ili kupata maisha na uzima wa milele.

Watawa wawe ni vyombo na mashuhuda wa matumaini
Watawa wawe ni vyombo na mashuhuda wa matumaini

Maisha ya kijumuiya yanachangamoto zake, lakini inawezekana kabisa kuishi kwa umoja na upendo katika jumuiya za kitawa, ikiwa kama watamwachia nafasi Roho Mtakatifu katika maisha yao, ili aweze kuwa ni chachu ya furaha ya maisha ya kijumuiya. Jumuiya zao za kitawa ziwe ni alama ya umoja wa kidugu duniani; shule za ukarimu zinazojengeka katika msingi wa mafungamano ya kijamii. Hii ni changamoto na mwaliko wa kuondokana na kinzani, maamuzi mbele, tabia ya baadhi ya watawa kutaka “kujimwambafai” kwa kujikita katika: lugha, ukabila na utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko na hatimaye, kujenga kuta za utengano na kinzani. Watawa wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa umoja, udugu na mshikamano kama walivyokuwa waasisi wa Mashirika yao. Ni katika muktadha huu, Mheshimiwa sana Sr. Simona Brambilla, M. C. wa Shirika la Wamisionari wa Consolata, Mwenyekiti mwenza wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume katika kipindi hiki cha Kwaresima anawaalika watawa kutembea kwa pamoja katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikita katika mabadiliko na hivyo kuendelea kusoma alama za nyakati, dhamana inayopaswa kutekelezwa katika umoja na wala si katika mang’amuzi ya mtu mmoja mmoja. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu wa Mungu kutembea kwa pamoja katika matumaini, kuelekea katika maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Matumaini ambayo ni kielelezo cha Msalaba, yanakita mizizi yake katika Moyo wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa watawa kuhakikisha kwamba, wanaboresha mahusiano na mafungamano yao katika jumuiya, kwa kutembea pamoja katika matumaini.

Ujumbe kwa Watawa
10 Machi 2025, 14:44