Mama Evaline Malisa Ntenga: Ujumbe Siku ya Wanawake Duniani 2025
Na Mama Evaline Malisa Ntenga, Dar es Salaam, Tanzania.
Kauli mbiu inayonogesha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Kwa Mwaka 2025 ni: “Kwa Wanawake na Wasichana Wote. Usawa. Haki na Uwezeshaji.” Wapendwa Wanawake Wenzangu, Tunapoadhimisha Siku ya Wanawake Duniani tarehe 8 Machi 2025, tunatafakari wajibu wetu wa kujenga jamii yenye usawa wa kijinsia, haki kwa wanawake na wasichana, na uwezeshaji wa kweli kwa wote. Kauli mbiu ya mwaka huu wa 2025, "Kwa Wanawake na Wasichana Wote. Usawa, Haki, Uwezeshaji," inatuhimiza kuhakikisha kuwa wanawake na wasichana wanapata nafasi sawa ya kushiriki, kuendelezwa, na kulindwa dhidi ya aina zote za unyanyasaji. Licha ya hatua kubwa zilizopigwa duniani kote, bado wanawake na wasichana wanakumbana na changamoto kubwa, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia, ukosefu wa fursa, na ubaguzi wa kijinsia. Katika dunia ya kidijitali, unyanyasaji wa mtandaoni umekuwa tishio kubwa kwa usalama wa wanawake na wasichana, ambapo vitisho vya udukuzi wa taarifa binafsi, matusi, kudhalilishwa, na kusambazwa kwa habari za faragha bila idhini vinawaathiri wengi. Ni muhimu kwa jamii kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha kuwa wanawake wanalindwa dhidi ya unyanyasaji huu na kwamba wahalifu wanawajibishwa ipasavyo na kwa wakati, ili kudhihirisha kuwa haki haikutolewa tu, bali ni lazima pia ionekane kuwa imetolewa.
Wajibu wa Mwanamke katika Ulinzi na Malezi ya Watoto kwa Ustawi wa Jamii: Katika jitihada za kujenga jamii yenye usawa, heshima, na mshikamano wa kijinsia, tunapaswa kutambua kuwa wanaume wengi wanaowanyanyasa wanawake ni wale waliowahi kuwa watoto waliotunzwa na wanawake. Hii inatufanya kutafakari kwa kina juu ya jukumu kubwa la mwanamke katika malezi na ulinzi wa watoto wote—wa kike na wa kiume—kwa misingi ya maadili, utu, na heshima. Hii ina umuhimu maana, watafiti wa sayansi ya jamii, wanatuambia kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya matendo ya ukatili ukubwani – na wahanga wa vitendo hivyo utotoni – yaani kuna uwezokano mkubwa aliyetendewa vitendo vya ukatili akiwa mtoto, akikua mtu mzima naye akawa mtandaji wa aliyotendwa. Kwa maantiki hii, ukatili unaweza kuwa na mkondo mrefu ambao mwanamke ana uhusika muhimu wa kuutokomeza.
Kanisa Katoliki ni moja kati ya Makanisa makubwa duniani ambayo yamejikita katika kufundisha na kuhubiri umuhimu wa kulinda: Utu, heshima na haki msingi za binadamu. Katika mafundisho yake, Kanisa Katoliki linaamini kuwa kila binadamu ana thamani sawa mbele za Mungu, na hivyo kila mtu anastahili kulindwa, kuheshimiwa na kupewa nafasi ya kuishi maisha yenye haki na amani. Kwa mujibu wa Katekisimu ya Kanisa Katoliki, haki ni "sifa za haki ya kila mtu kupewa nafasi ya kuishi, kupata chakula, mavazi, makazi, elimu, afya, na huduma nyingine muhimu kwa ajili ya maisha yake."yaani Kanisa Katoliki linasisitiza kuwa haki hizi zinastahili kupewa kipaumbele na kuhakikishwa na serikali na jamii kwa ujumla. Katika Injili, Yesu Kristo pia alisisitiza umuhimu wa haki na kulinda haki za wengine. Kwa mfano, katika Mathayo 25:31-46, Yesu anaelezea jinsi atakavyowahukumu watu wakati wa mwisho wa dunia. Atawauliza kama walishiriki katika kuwalisha wenye njaa, kuwapa maji wenye kiu, kuwatembelea wagonjwa na kuwafariji wafungwa. Maandiko haya yanasisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa haki za wengine zinalindwa na kuheshimiwa.
Mtakatifu Yohane Paulo II alianza kuandika nyaraka mbalimbali kama ule uitwao “LETTER OF POPE JOHN PAUL II TO WOMEN:“Feminine Genius” uliochapishwa tarehe 29 Juni 1995. Katika waraka huu wa Kitume alitangaza mwaka huo 1995 kuwa mwaka wa wanawake ulimwenguni, lakini alianza kuandika kuhusu harakati za wanawake na thamani waliopewa kutoka kwa Mungu. Katika waraka huo yeye alielezea wajibu wa wanawake tofauti kabisa na yale ambayo yameelezwa na waliokuwa wanaharakati za wanawake wa Umoja wa Mataifa. Alielezea kuwa, Mwanaume na Mwanamke wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wameumbwa sawa, lakini tofauti sio katika kushindana, bali kukamilishana (They are created equal but different to complement each other.) Mwanamke ni njia ya kupitisha kusudi la Mungu la uzazi/uumbaji – hii ni zawadi. Pamoja na tafiti za kisayansi na gunduzi zinazofanywa duniani ili kupoka nafasi ya mama kubeba kiumbe na kukileta duniani, kila mwanadamu tunayemwona alitokana na uzao wa mwanamke. Kuzaa siyo tu kuendeleza kizazi, bali ni baraka ambayo Mungu alitubariki wanadamu ili kushiriki uumbaji pamoja naye (Mwanzo 1:28). Kushiriki kazi ya uumbaji wa Mungu (kupitia uzazi) ni sawa na kuitangaza Injili kupitia malezi bora ya uzao wa mwanamke. Kama mama, dada, bibi, na walezi, wanawake wana nafasi muhimu ya kuhakikisha kuwa kizazi kijacho kinalelewa kwa mtazamo wa haki na usawa. Kizazi kinachojengwa juu ya maadili ya huruma, heshima, na mshikamano wa kijinsia. Tukiwalea watoto wa kike kwa uthabiti, tunaweza kuwajengea ujasiri wa kutambua thamani yao, kudai haki zao, na kushiriki kikamilifu katika jamii bila hofu. Tukiwalea watoto wa kiume kwa misingi ya heshima kwa wanawake, utu, na usawa wa kijinsia, tunawajengea uelewa wa kuwa mabalozi wa haki badala ya kuwa sehemu ya tatizo. Tukiwaelimisha watoto wetu kuwa kila binadamu ana thamani sawa mbele ya Mungu, tutakuwa tumepanda mbegu za jamii yenye haki na amani.
Ni wajibu wa kila mwanamke kuhakikisha kuwa watoto anaowalea hawageuki kuwa wale wanaokuza/endeleza unyanyasaji wa kijinsia, ubaguzi wa kijinsia, au ukatili wa aina yoyote. Badala yake, tunapaswa kuwakuza katika mazingira yanayowafundisha heshima kwa kila mtu, mshikamano wa kweli, na utu kwa wote. Kwa kuelewa kuwa vizazi vya baadaye vipo mikononi mwetu, wanawake wanapaswa kuongoza jitihada za kujenga jamii ambapo kila mtoto, wa kike au wa kiume, analelewa kwa mtazamo wa usawa, haki, na mshikamano wa kijinsia. Kwa namna hili, tunashiriki moja kwa moja katika kuunda ulimwengu bora unaohakikisha kuwa wanawake wote wanaheshimiwa, wanalindwa, na wanapewa nafasi sawa katika jamii. Kwa hivyo, tunapoadhimisha Siku ya Wanawake Duniani tarehe 8 Machi 2025, naomba tujitathmini: Je, tumejenga kizazi kinachoweka utu wa binadamu mbele ya yote? Je, tumewalea watoto wetu wawe sehemu ya suluhisho badala ya kuwa sehemu ya tatizo? Jibu la haya lipo katika juhudi zetu za kila siku za malezi, makuzi na ulinzi wa watoto wetu bila kumsahau mtoto wa kiume ambaye kwa muda amesahaulika. Heko wanawake wote wa shoka wanaojibidisha katika kujenag jamii yenye maadili bila kujali changamoto wanazopitia katika wajibu huu msingi.
Ni Mama Evaline Malisa Ntenga, Rais, Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika.