Kwaresima ni Safari ya Matumaini: Katika Sala, Neno, Kufunga Na Kumwilishwa Katika Matendo
Na Padre Philemeon Anthony Chacha, - Vatican.
Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, tunapoendelea kuadhimishwa mwaka wetu wa Jubilei ya matumaini, Mama Kanisa anatualika kufungua mioyo yetu ili tuweze kupokea neema inayotoka kwa Mwenyezi Mungu tunapoanza kipindi hiki cha Kwaresima. Kanisa kama mama na mwalimu linatupatia kipindi cha tafakari na toba, maombi na kujitakasaa kiroho, pamoja na kutathmini uhusiano wetu na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani. Katika ujumbe wa Kwaresima mwaka huu wa 2025, Baba Mtakatifu Francisko anatualika sisi sote kama jumuia ya waamini inayosafiri pamoja kwa matumaini, katika safari ya kiroho kuelekea Pasaka. Safari hii ni ya ndani ya nafsi, ya kutafakari maisha yetu na kurejea kwa Mungu. Kwa kawaida huwa tunajiuliza, “Je ni nini ambacho nitajinyima katika kipindi hiki cha Kwaresima?” Hili ni swali zuri, lakini linaweza tu kutusaidia kwa kiwango fulani. Swali la msingi na la muhimu ambalo tunaweza kujiuliza katika kipindi hiki cha Kwaresima ni, “Nitawezaje kutubu na kumrudia Mwenyezi Mungu katika Kwaresima hii?” Hili linatoa swali lingine la kufikirika zaidi: “Ni sehemu gani ya maisha yangu niliyokuwa mbali na Mwenyezi Mungu, na ni nini nitaweza kufanya ili niweze kumrudia yeye?” Kumbe, tunapoanza kipindi hiki siku ya Jumatano ya Majivu hatuna budi kuwa wa kweli kadiri tuwezavyo katika kujitafakari na kujitathimini kuhusu njia ambazo tumemuacha Mwenyezi Mungu na nyakati zote ambazo roho zetu zilipoa. Zaburi ya 51 inasema: “Wewe wataka unyofu wa ndani, hivyo nifundishe hekima moyoni.” Tunapopokea hekima na ufahamu kutoka kwa Mungu kuhusu hali yetu halisi, tunaweza kuchagua nidhamu za kiroho zinazotufaa katika kurudi kwake au kurudisha bidii yetu ambapo mioyo yetu imepoa.
Sala ya mwanzo katika Ibada ya Misa Takatifu ya Jumatano ya Majivu, yaani Kolekta inatuambia kwamba: Ee Bwana, utujalie sisi waamini wako tuanze vita vya kiroho kwa mfungo mtakatifu, ili katika kushindana na jeshi la pepo wabaya, tulindwe na misaada ya kujinyima... Kumbe tunaitwa katika kuingia kwenye vita ya kiroho na kuacha baadhi ya mazoea halisi ambayo yanaweza wa kutupeleka katika mtego wa dhambi kwenye maisha yetu. Hivyo tunaitwa kujikita zaidi katika: Tafakari ya Neno la Mungu, Sala, Kufunga na Kufanya Matendo ya huruma; Kuwa wanyenyekevu, kujitathmini na kutubu, kusamehe wengine kama tulivyosamehewa, na kuweka hazina yetu mbinguni kwa kujitoa kwa ukarimu kwa wengine. Kama tungekuwa peke yetu, pengine tusingechagua kujitoa na kujinyima katika kipindi chote hiki kwa kujiwekea masharti magumu kama haya, lakini Mwenyezi Mungu anatambua kuwa tunahitaji yote haya. Tunapopokea ishara ya majivu kwenye paji la uso wetu, tunakiri udogo wetu wa kibinadamu na hali yetu ya kifo. Haijalishi tunavyofikiri kuwa sisi ni nani, majivu yanatukumbusha kuwa, “Wewe ni mavumbi, na mavumbini utarudi” (Mwanzo 3:19). Hili si jambo la kututia hofu, bali ni njia ya kutuzuia kujikweza kupita kiasi na kutufanya tutambue hali yetu halisi ya kibinadamu. Majivu yanayotiwa kwenye paji la uso yana maana sawa na ile ya Agano la Kale ya kujifunika majivu kama ishara ya toba na huzuni juu ya dhambi. Hili pia ni jambo jema kwetu kwa sababu mara nyingi tunaishi katika hali ya kuukana ukweli. Kwa kufungua mioyo yetu, tunamwomba Mungu atuchunguze, atujue, na hatimaye atuongoze kwenye maisha mapya ya ufufuo.
Lengo la kushiriki kikamilifu katika kipindi hiki cha Kwaresima ni kuzidi kuelewa tamaa yetu ya Mwenyezi Mungu ili tumtafute kwa moyo wetu wote. Mazoea ya kufunga na aina nyingine za kujinyima hutusaidia kukabiliana na mtego wa dhambi ili tuweze kuacha kila kitu kisicho cha Mungu. Tunapokabiliana na hali halisi ya jinsi tunavyoshikamana na mambo yasiyofaa, tunaingia katika huzuni ya kiroho inayopelekea kwenye toba, na kisha msamaha na uhuru. Ingawa Kwaresima ni kipindi muhimu cha kiroho, pia ni kipindi cha matumaini makubwa tunapoonja upendo mkuu wa Mungu kwetu, hata katikati ya dhambi tunazotubu. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake wa Kwaresima, anatualika kuongeza matumaini yetu kwa Kristo, licha ya changamoto za maisha. Kumbe kama mahujaji wa kiroho tunaitwa kushikilia tumaini letu kwa Yesu ambaye ameshinda dhambi na kifo kwa ajili yetu sisi wanadamu. Ni wapi katika maisha yako unahisi umemwacha mbali Mwenyezi Mungu? Ni mambo gani yanayokusumbua na kukuzuia kukuza uhusiano wako na Mungu? Anza safari yako ya Kwaresima kwa kuwa muwazi mbele ya Mungu na kutafakari juu ya kile unachoweza kuacha na kuanza upya ili kuongeza nafasi na shauku zaidi katika uhusiano wako na Mwenyezi Mungu. Kama vile Katekisimu ya Kanisa Katoliki inavyotukumbusha: “Uongofu kwanza ni kazi ya neema ya Mungu anayefanya mioyo yetu imrudie… Mungu hutupa nguvu ya kuanza upya. Katika kugundua tena ukuu wa mapendo ya Mungu moyo wetu hutikiswa na kitisho na uzito wa dhambi na huanza kuogopa kumkosea Mungu kwa dhambi na kutengwa naye. Moyo wa binadamu huongoka kwa kumtazama Yeye ambaye dhambi zetu zilimchoma” (KKK 1432). Ndugu msikilizaji na msomaji wa Radio Vatican, kila mmoja wetu anaalikwa kuitikia mwito wa Bwana wa kurekebisha maisha yetu. Kwaresima ni nafasi yetu ya kuwa bora zaidi. Usiwe na kisingizio cha kutobadilika kuwa bora! Mama Maria, Mama wa Matumaini, atuombee na atuongoze katika safari hii ya Kwaresima. Nawatakia kipindi chema na wakati mwema wa Kwaresima.