Kard.Parolin:hakuna heshima kwa sheria ya kibinadamu tena,tutafute njia za mazungumzo na amani!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Vatican, alielezea kwa niaba ya Vatican wasiwasi wake juu ya "kurejeshwa" au "kuendelea" kwa mapigano mengi ulimwenguni, kuanzia yale ya siku chache zilizopita katika Ukanda wa Gaza, ambayo pia alilaaniwa na Papa Francisko katika Ujumbe wake wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 23 Machi 2025 kama ilivyokuwa kwa siku nyingine. Kardinali Paroli alisema hayo, nje ya fursa ya Mkutano kuhusu Maisha marefu. Katika wito wa Sala ya Malaika ambao ulikuwa wa mwisho wakati wa kukaa kwake hospitalini Gemelli, Papa alionesha umuhimu wa subira ambayo inawaongoza wanadamu kwenye wongofu. Papa anasisitiza wasiwasi wake na hivyo pia Maneno hayo ya Papa yalifuatiliwa na jibu la Ubalozi wa Israel kwa Vatican kupitia akaunti yake ya X, ambapo ulithibitisha kuwa unafanya kazi kwa kuzingatia sheria za kimataifa.
Kardinali Parolin pembezoni mwa tukio la alasiri tarehe 24 Machi 2025, katika Chuo cha Baba wa Kanisa Augustinianum Roma ambao ulioongozwa na mada: "Mkutano wa Maisha marefu: Changamoto ya saa ya wakati", iulioandaliwa na Chuo cha Kipapa cha Maisha, akijibu moja ya maswali ya waandishi wa habari, alisisitiza kwamba "wito wa Papa ni wito wa kuacha vita, kutafuta njia za mazungumzo na amani." Hivi majuzi," Kardinali Parolin akiripoti, "tulizungumza na Shirika la Msalaba Mwekundu na wao pia wako katika hali ngumu sana. Mashambulio ya raia, mauaji ya wafanyakazi wa kibinadamu, yote ni matendo ambayo yanakwenda kinyume kabisa na sheria za kibinadamu na leo hakuna heshima kwa sheria ya kibinadamu. Ni mojawapo ya mapungufu makubwa ya msimu huu: hakuna tena heshima kwa sheria za kibinadamu."
Afya ya Papa
Alipoulizwa kuhusu afya ya Papa Francisko, siku moja baada ya kuruhusiwa kutoka Gemelli baada ya kukaa hospitalini kwa siku 38, Kardinali Parolin alieleza kwamba Papa "sasa atahitaji kupata nafuu na kuwa mtulivu." Kulingana na Katibu wa Vatican ni mapema kutabiri jinsi ajenda ya Papa na ratiba ya mikutano na sherehe mbalimbali zitakavyoandaliwa. "Kazi ya ofisi itaendelea, lakini kwa sasa hali muhimu zaidi zitawasilishwa kwa Papa, na masuala ambayo yanahitaji maamuzi kwa upande wake, pia ili tusimchoshe sana. Kisha, atakapopata nafuu hatua kwa hatua, tutarudi kwenye programu ya kawaida," alisisitiza Papa Francisko.
Hotuba katika Mkutano huo
Katika hotuba yake kwenye mkutano huo, Kardinali Parolin alisisitiza kwamba “maisha marefu ni mojawapo ya changamoto kubwa za wakati wetu” kwa sababu si suala la kimatibabu pekee, bali ni suala linaloathiri jamii kwa ujumla, linalohusisha uchumi, utamaduni, maadili na hali ya kiroho. "Tunaishi katika enzi ambayo mapungufu na udhaifu huelekea kukataliwa, kana kwamba uzee ni shida ya kufichwa," alielezea Kardinali Parolin. "Lakini maisha ni zawadi na huhifadhi thamani yake katika kila awamu ya maisha - aliongeza - hatuwezi kuanguka katika udanganyifu wa maendeleo yanayofuata kutokufa kwa kibiolojia, tukisahau kwamba utimilifu wa kweli hupatikana, si kwa wingi wa miaka, lakini katika ubora wa mahusiano, katika upendo unaotolewa na kupokea, kwa maana ya kina ya kuwa sehemu ya jumuiya ". Kwa sababu hii kardinali alihimiza "utafiti wa kisayansi na kiteknolojia" uelekezwe "kwa manufaa kamili ya mtu" na "kutumikia utu wa binadamu na udugu wa ulimwengu wote". "Maisha marefu hayawezi kuwa fursa iliyohifadhiwa kwa wachache, au aina mpya ya usawa wa kijamii," alisisitiza, pia akinukuu maneno ya Papa Francisko juu ya mada hiyo. Hatimaye, Kardinali Parolin alisisitiza umuhimu wa mahusiano kati ya vijana na wazee ili kuleta mshikamano kati ya vizazi na kuepuka utamaduni wa ubinafsi na wa kutupa."