杏MAP导航

Tafuta

2025.03.01 Jubilei ya Gemelli 2025.03.01 Jubilei ya Gemelli 

Jubilei ya Gemelli:Jubilei ni wakati wa kuwa watoto tena wa kugundua furaha!

Madaktari,wauguzi,wafanyakazi wa afya,wafanyakazi wa kiufundi na utawala wa Hospitali ya Chuo Kikuu na Hospitali ya "kisiwa cha Gemelli,Roma iliyounganishwa na Chuo Kikuu Katoliki cha Moyo Mtakatifu wamekuwa katika hija Machi Mosi katika Kanisa Kuu la Vatican na sala kwa ajili ya Papa ambapo Mons.Giulidori msaidizi wa Kikanisa alisema:Jubilei kwa hakika ni wakati wa neema ya kugundua upya kipimo sahihi cha maisha yetu na kitovu cha kweli cha uzito wa kila kitu.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Askofu Claudio Giuliodori, Msimamizi Mkuu wa Chuo Kikuu Katoliki cha Moyo Mtakatifu  aliongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Jubilei ya Chama cha Mfuko wa Hospitali ya Agostino Gemelli, Roma, iliyojumuisha Madaktari, wauguzi, wafanyakazi wa afya, wafanyakazi wa kiufundi na utawala wa Hospitali ya Chuo Kikuu na Hospitali ya "kisiwa cha Gemelli ,Roma iliyounganishwa na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu, Jumamosi tarehe 1 Machi 2025 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro. Katika mahubiri yake baada ya masomo ya siku kutoka (Sir 17, 1-13; Sal 102; Mc 10, 13-16), Monsi Giuliodori alisema ni zawadi kubwa kwao wote kuweza kuadhimisha Ekaristi katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro na kitovu cha Kikristo. Wazo letu kwanza kabisa  linamwendea Baba Mtakatifu Francisko ambaye tulikuwa tunafikiria kukutana naye asubuhi katika Ukumbi wa Paulo VI,  ili kusikiliza Katekesi ya Jubilei, lakini alitushangaza kuja yeye kwetu katika Hospitali ya Gemelli. Wazo  letu kwanza linamwendea Yeye na sala zetu zinanuliwa kwa mtindo wa pamoja wa kina katika makao ya Mfuasi wa Petro, kwa sababu Papa Francisko aweze kupata nafuu kamili na kwa muda mfupi.

Kuelekea Mlango Mtakatifu
Kuelekea Mlango Mtakatifu

Askofu Giuliodori alisema tunatambua utaalamu wa juu wa madaktari wetu na tuwasaidie wao kwa sala , ili waweze kufanya maamuzi ya kimatibabu yanayofaa na muafaka. Kutoka Ulimwenguni kote zimefika sala bila kukoma kwa Baba Mtakatifu ambayo ni manukato yenye thamani. Hata hiyo hatujapoteza tumaini kwamba Papa anaweza kushinda kipindi hiki kigumu na kurudisha kikamilifu nguvu zake za lazima na huduma yake ya juu ya kitume. Tunakumbuka kwa upendo na shukrani hata kwa maneno ambayo yalitangaza na kuongoza Jubilei hii, kipindi cha neema kweli ambacho kila mmoja wetu, kwa ajili ya Kanisa na kwa ajili ya ubinadamu wote. Tuko hapa hata sisi, “ mahujaji wa matumaini:” Kile tunachotafuta kwa ajili ya maisha na kile ambacho sisi tunaitwa kutoa kwa wengine katika hali nzito na ngumu ya maisha. Askofu Claudio Giuliodori aliendelea kusema kuwa ni kwa njia hiyo walipitia Mlango Mtakatifu, ule wa Basilika, ishara yetu ya kwenda kukutana na Kristo, ambaye anafungulia watu mlango kwa wote wa moyo wake na kukaribisha kwa mkumbatio wake wa huruma. Hiki ndicho chanzo cha tumaini fulani, ambalo halidanganyi wala halikatishi tamaa. "Kila mtu anatumaini - Papa alisema katika Tangazo la Jubilei: Katika moyo wa kila mtu kuna tumaini kama hamu na matarajio ya mema, hata bila kujua kesho italeta nini. […] Jubilei iwe fursa kwa kila mtu kufufua matumaini. Neno la Mungu hutusaidia kupata sababu za hili” (Spes non confundit, n. 1). Tuko hapa, pia, leo, "kufufua tumaini," ili kuifanya ikue katika familia zetu na, zaidi ya yote, kushiriki na wale ambao wamechoka na kujaribiwa na maisha.

Injili:tumaini lina uso wa watoto na inalishwa na upole wao

Neno la Mungu linatuongoza na kutusindikiza katika hija hii ya matumaini. Leo Injili inatukumbusha kwamba tumaini lina uso wa watoto na inalishwa na upole wao. Yesu anawakumbatia na kuwaonyesha kuwa vielelezo vya kufuata: “Ufalme wa Mungu ni wao; Jubile ni wakati wa kujipyaisha ambapoo kwa kuzingatia fundisho hili la Yesu tunaweza kufafanua kama "wakati wa kuwa watoto tena", yaani, kuanza tena na kugundua tena furaha, shauku, hali ya kawaida ya utoto wetu, ikiwa sio ya kimwili, bila shaka ya kiroho. Maisha huleta misalaba mingi na mizigo, ambayo hatari zaidi ni ile inayosababishwa na dhambi. Kwa sababu hii, Jubilei inatupa fursa ya kujitakasa na kujifanya upya, kugundua upya wa ubatizo, wa kuunganishwa kwetu kwa karibu na kwa kina na Kristo. Sio kurudi nyuma. Hatuwezi kurudisha nyuma mkanda wa maisha yetu. Badala yake, ni lazima kuzaliwa upya, kama Yesu anavyomfundisha Nikodemo ambaye anamwuliza: “Mtu awezaje kuzaliwa akiwa mzee? Je, anaweza kuingia tumboni mwa mama yake na kuzaliwa mara ya pili?” Yesu akajibu, “Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu, na kilichozaliwa kwa Roho ni roho” (Yh 3:4-6). Leo tunapewa tena mwaliko huu wa kuanza tena kwa nguvu maisha ya kiroho ambayo yanamaanisha kurejesha ujana wa Roho, katika ufahamu kwamba ustawi wa kweli, unaotafutwa sana, na ambao mara nyingi huondolewa na wanawake na wanaume wa wakati wetu, kwanza kabisa ni hali ya nafsi.

Kuelekea Mlngo Mtakatifu
Kuelekea Mlngo Mtakatifu

Ustawi wa kweli hutoka moyoni na hutokeza furaha ya kweli, si wa muda mfupi au wa kitambo tu, ambapo unaweza kupatikana kwa kurudi kwenye usahili na ubinafsi wa watoto. Kama vile Papa anavyosema zaidi katika Tangazo la Jubilei: "Tunahitaji furaha ambayo inapata utimilifu wake wa uhakika katika kile kinachotukamilisha, yaani, katika upendo, ili tuweze kusema, tayari sasa: “Napendwa, kwa hiyo nipo; na nitakuwepo milele katika Upendo ambao haukatishi tamaa na ambao hakuna chochote na hakuna mtu atakayeweza kunitenganisha” (SnC, n. 21). Viunga  vya maisha vinavyoundwa na upendo vinaweza kupatikana kutoka katika usomaji wa somo la kwanza kutoka kitabu cha Sira. Ni maandishi ya hekima kuu ambayo yanaelezea hali ya mwanadamu na yanaonesha njia ya utambuzi kamili. Katika hilo, Askofu aliakisi mambo matatu muhimu: Kwanza ni utambuzi wa ukomo wa mtu mwenyewe bila kupoteza utu na thamani kubwa ya kila maisha ya mwanadamu. Mwandishi mtakatifu anatualika tusisahau hali ya wanadamu duniani ilivyo, ambayo anasema: "Akawawekea siku zilizohesabiwa na wakati mdogo, akiwapa mamlaka juu ya yote yaliyomo."

Jubilei kwa hakika ni wakati wa neema ya kugundua upya “kipimo sahihi” cha maisha yetu na kitovu cha kweli cha uzito wa kila kitu ambacho ni Yesu Kristo, tukiepuka, kwa upande mmoja, mkanganyiko wa uweza na, kwa upande mwingine, dharau kwa ubinadamu. Blaise Pascal anatusaidia kuwa na mtazamo huu, kama vile Baba Mtakatifu Francisko alivyosisitiza waziwazi katika Waraka wa Kitume Sublimitas et miseria hominis (19 Juni 2023), uliochapishwa katika miaka mia moja ya kuzaliwa kwa mwanasayansi na mwanafalsafa mkuu wa Ufaransa.Pascal anasema hivi: “Si kwamba hatumjui Mungu tu ila kwa njia ya Yesu Kristo, bali hatujitambui wenyewe isipokuwa kupitia Yesu Kristo. Hatujui uzima, kifo, isipokuwa kwa njia ya Yesu Kristo. Nje ya Yesu Kristo hatujui maisha yetu ni nini, wala kifo chetu, wala Mungu wala sisi wenyewe” (Fikra, n. 36) na hata kwa uwazi zaidi: “Kumjua Mungu pasipo kujua taabu ya mtu mwenyewe hutokeza kiburi. Kujua taabu yako mwenyewe bila kujua taabu ya Mungu huleta kukata tamaa. Ujuzi wa Yesu Kristo huzalisha maana sahihi ( le milieu ), kwa sababu huko tunampata Mungu na taabu zetu” ( Mawazo, n. 75). Ni hekima ile ile ambayo zaburi inayoitikia inatukumbusha: “Mwanadamu: siku zake ni kama majani! Kama ua la shambani, ndivyo yeye husitawi… Bali upendo wa Bwana una tangu milele hata milele juu yao wamchao.”

Kuelekea Mlango Mtakatifu
Kuelekea Mlango Mtakatifu

Mungu akawajaza ujuzi na ufahamu

Askofu alikazia kusema kuwa  katika mtazamo huu wa kikomo, hata hivyo, ufahamu wa ukuu wa mwanadamu haupungui kwa sababu maandishi ya Sira bado yanasema: [Mungu] "akawajaza ujuzi na ufahamu na akawaonesha mema na mabaya". Hili ni jambo la pili ambalo limeongoza, tangu kuanzishwa kwake miaka 60 iliyopita, kujitolea kwa Hospitali ya Gemelli, iliyotamaniwa na Mwanzilishi wa Chuo Kikuu, kwa kuchanganya kwa ukali na matunda kwa sayansi na imani, utafiti wa juu zaidi na kujitolea kwa kina zaidi kwa watu wagonjwa, majaribio ya ujasiri zaidi na wajibu mkali zaidi wa maadili.  Sisi ni Hospitali ya Chuo Kikuu ambacho ni kielelezo cha Chuo Kikuu cha Kikatoliki na hasa, katika tawi la Roma, cha Kitivo chenye jukumu la kufundisha vizazi vipya katika sekta ya afya. Si rahisi wala si dhahiri kuwafundisha na kuwaelimisha vijana kupambanua mema na mabaya na kukuza roho ya utumishi halisi na ya ukarimu inayochochewa na tunu za mshikamano na utunzaji, mfano wa Ukristo. Katika jamii iliyo na ubinafsi na kutawaliwa na utamaduni wa kutojali, hii ni changamoto kubwa leo na vijana wanatarajia kupata  kutoka kwetu ushuhuda wa uwazi na ujasiri. Jubilei pia inatuomba hili: kuwa mashuhuda wa kuaminika na waelimishaji wanaofaa kwa vizazi vipya. Tuko hapa ili kugundua upya na kuzindua upya sababu kuu za kujitolea kwetu kielimu, kiini cha dhamira ya Chuo Kikuu chetu, ambayo pia kinafikiwa kutokana na umaarufu wa ajabu wa Hospitali ya Gemelli.

Misa kwa ajili ya Jubilei ya Gemelli
Misa kwa ajili ya Jubilei ya Gemelli

Kujitolea kwa huduma kwa kufanya kazi pamoja na wagonjwa kila siku

Mwelekeo wa tatu ambao unaoneshwa kwetu na maandishi ya Sira ni kujitolea kwa huduma ambayo inatuona tukifanya kazi pamoja na wagonjwa kila siku. Tunahisi kwamba onyo la Maandiko ni kweli hasa kwa kila mmoja wetu na kwa taasisi yetu ya afya: "Jihadharini na kila dhuluma na kila mmoja wenu lazima amtunze jirani yake." Pia tuko hapa ili kijipyaisha dhamira yetu ya kuwahudumia wagonjwa ambao mara nyingi ni dhaifu na wahitaji. Ni mojawapo ya ishara bainifu za safari ya Jubilei iliyoakisiwa  na Baba Mtakatifu katika Hati ya tangazo ya Jubilei  ambapo tunasoma: “Ishara za matumaini zinapaswa kutolewa kwa wagonjwa, walio nyumbani au hospitalini. Mateso yao yapate kitulizo katika ukaribu wa watu wanaowatembelea na katika mapenzi wanayopata." Wakati anatualika kuwa Wasamaria wa kweli na chanzo cha matumaini, Papa pia alitoa maneno ya shukrani ya kweli kwamba kwa wakati huu “ningependa kufanya yangu mwenyewe na hotuba kwa ninyi nyote, pia kwa niaba ya wale wanaohusika na Hospitali ya  Gemelli: "Shukrani ziwafikie wafanyakazi wote wa afya ambao katika hali ngumu mara nyingi, kutekeleza utume wao kwa huduma ya makini kwa  wagonjwa wengi," alisema Papa. Aya inahitimisha kwa ufafanuzi huu mzuri wa roho ya wafanyakazi wa afya kwamba: "Kwao, utunzaji ni wimbo wa utu wa mwanadamu, wimbo wa matumaini ambao unahitaji jamii nzima kujiunga" ( SnC, n. 11).

Kwa kuhitimisha Askofu Giuliodori alisema kuwa, kwa kufikiria Hospitali  yetu Gemelli kama mahali ambapo kila siku "nyimbo za utu" na "nyimbo za matumaini" zinakuzwa, tunaendeleza "hija yetu ya matumaini" ambayo haina mwisho na siku hii na tunakabidhi kwa mara nyingine tena kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu na kwa Mama yetu wa Mbinguni afya ya mpendwa wetu Papa Francisko. Tumsifu Yesu Kristo.

Mahubiri ya Askofu Giuliodori:Jubilei ya Gemelli
01 Machi 2025, 17:10