Idadi Ya Wakatoliki Duniani Ni Bilioni 1.406 Katika Kipindi Cha Mwaka 2025
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Takwimu zilizotolewa na Idara ya Takwimu za Kanisa Katoliki Ulimwenguni “Annuarium Statisticum Ecclesiae” zinaonesha kwamba, idadi ya Waamini wa Kanisa Katoliki katika kipindi cha Mwaka 2025 imeongezeka kutoka bilioni 1. 39 za Mwaka 2024 hadi kufikia bilioni 1.406 katika kipindi cha Mwaka 2025. Katika kipindi hiki, Baba Mtakatifu ameunda majimbo makuu matatu; ameunda majimbo mapya saba, likiwemo Jimbo Katoliki la Bagamoyo “Dioecesis Bagamoyensis” pamoja na kuunda Jimbo jipya la Kitume. Lengo kuu ni kusogeza huduma za kichungaji kwa watu wa Mungu. Itakumbukwa kwamba, Idadi ya waamini wa Kanisa Katoliki kati ya mwaka 2022 hadi mwaka 2023 ilikuwa ni bilioni 1.39. Bara la Afrika linachukua asilimia 20% ya Waamini wote wa Kanisa Katoliki duniani na kwamba, nchi zinazoongoza kwa idadi kubwa ya waamini wa Kanisa Katoliki Barani Afrika ni: DRC, ikiwa ni wakatoliki milioni 55, Nigeria waamini milioni 35 na kuna nchi ambazo pia zina idadi kubwa ya waamini wa Kanisa Katoliki ni kutoka Afrika Mashariki yaani: Uganda, Tanzania na Kenya.
Ukuaji wa waamini wa Kanisa Katoliki Barani Afrika ni sawa na asilimia 3.31%. Idadi ya Maaskofu wenye dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu imeongezeka kwa asilimia 1.4% kutoka Maaskofu 5, 353 hadi kufikia Maaskofu 5, 430. Idadi ya Maaskofu Barani Afrika imeongezeka kutoka asilimia 13.8% hadi asilimia 14.2% ya Mwaka 2023. Kanisa Katoliki lina Majimbo makuu 3, 041 na Majimbo 406, 996. Idadi ya Mapadre Barani Afrika imeongoza kwa asilimia 2.7%. Idadi ya Mashemasi wa kudumu katika kipindi cha Mwaka 2023 imeongezeka kutoka Mashemasi 50, 150 hadi kufikia Mashemasi 51, 433. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna idadi ndogo sana ya Mashemasi wa kudumu Barani Afrika.
Idadi ya watawa wa kiume na wa kike inaendelea kupungua, ingawa idadi hii Barani Afrika inaendelea kuongezeka, lakini athari kubwa inajionesha Barani Ulaya. Idadi ya watawa imepungua kutoka watawa 599, 228 katika kipindi cha mwaka 2022 hadi kufikia watawa 589, 423 katika kipindi cha Mwaka 2023 ikiwa ni pungufu ya asilimia 1.6%. Barani Afrika kuna ongezeko la asilimia 2.2%. Idadi ya waseminari walioko Seminari kuu imepungua kwa asilimia 1.8% yaani kutoka kwa Waseminari 108.481 hadi kufikia idadi ya waseminari 106, 495, lakini Barani Afrika idadi ya waseminari imeongezeka kwa asilimia 1.1% kutoka waseminari 34, 541 hadi kufikia waseminari 34, 924.