Ukraine,Reina:watu walioteswa Ukraine warudi kuwa na amani
Na Isabella H. de Carvalho – Vatican.
Kardinali Baldo Reina, Makamu wa Papa Jimbo kuu la Roma, akiwa katika Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane huko Laterano, ambako asubuhi tarehe 24 Februari 2025 aliadhimisha Misa Takatifu kwa ajili ya kumbukizi ya miaka mitatu tangu Urusi ilipovamia Ukraine kwa kiasi kikubwa alisema: Katika "siku hii ya uchungu na ya aibu" tunawaombea waathirika na kwamba watu wa Kiukraine wanaoteswa warudi kwa amani.”
Hafla hiyo, iliyoandaliwa na Ubalozi wa Ukraine kuwakilisha nchi yake Vatican, ilihudhuriwa na wawakilishi wengi wa kidiplomasia, ambao baadhi yao walisali sala katika lugha zao za asili ili kuonesha msaada wao. Waamini wengi walikusanyika katika Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane, wakiwa na bendera na rozari mikononi mwao na machozi machoni mwao, ili kuombea amani katika nchi hiyo ambayo Baba Mtakatifu Francisko ameitaja siku zote kuwa "inateswa." Kardinali alikumbuka mara kadhaa wakati wa mahubiri yake kujitolea na maneno ya mara kwa mara ya Baba Mtakatifu kwa ajili ya amani nchini Ukraine.
Hebu turudie wito wa Papa wa amani
Wakati wa mahubiri yake, Kardinali Reina alihakikishia kusanyiko hilo ukaribu wake na sala kwa Papa Francisko, ambaye amelazwa katika hospitali ya Gemelli tangu Februari 14. Licha ya ugonjwa wake, katika maandishi ya Sala ya malaika wa Bwana Februari 23, iliyotolewa na Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Vatican, Papa hakukosa kueleza ukaribu wake juu ya kumbukumbu hii ya huzuni kwa Ukraine. Makamu huyo alimshukuru Papa, "kwa maneno yake mazito katika miaka mitatu, maneno ambayo kiukweli tuliyapokea kama ya kinabii. Maneno yanayouliza na yameomba zawadi ya amani. Ni mara ngapi Baba Mtakatifu amesema: ‘Inatosha! Acha silaha zisimame. Leo hii hatuwezi kujizuia kurudia maneno haya ya Askofu wetu, mchungaji wetu,” Kardinali Reina alisema. Kwa kuongezea alisema "Asante, Papa Francisko kwa sababu mara nyingi umeomba njia za amani zichukuliwe, na kwa hangaiko lako hili la ubaba, ili watu wa Ukraine wanaoteswa warudi kuwa na amani."
Umuhimu wa maombi
"Nikifikiria nyuma kuhusu miaka hii mitatu ya vita, nadhani sote tumetiwa alama na picha zinazofika katika nyumba zetu kila siku, hasa za watoto, wanaume, wanawake, askari ambao wamepoteza maisha yao. Palipo na vita, hakuna hekima,” Kardinali huyo aliongeza. Palipo na migogoro na uvamizi, hakuna akili ya busara,” alisisitiza, akiibua juu ya somo la kwanza wa liturujia, lililochukuliwa kutoka katika kitabu cha Sira. "Tunahitaji kumwomba Bwana kurejesha uwezo huu wa kutafakari ili kukabiliana na hali hii ya migogoro kwa kuunda utamaduni wa amani".
Kutafuta njia za upatanisho
Mkuu wa Jimbo Kuu la Roma kisha alisisitiza umuhimu wa maombi katika wakati huu wa mvutano mkubwa. "Tumepitia, na bado tunapitia, kushindwa kwa majaribio ya wanadamu. Tunahitaji kumwambia Yesu… tusaidie katika kutoamini kwetu.” Kwa hivyo sala yetu nu kwamba "Mungu wa amani, Mungu wa uzima, aweze kutatua yale ambayo wanadamu hawakuwa, na hawawezi kusuluhisha, na atusaidie kupata njia za upatanisho, huruma na amani. Kardinali huyo alimaliza kwa sala kwa ajili ya waathiriwa wa vita na familia zao, akimsihi Mungu awape kila mtu nguvu na tumaini ili amani iweze kusitawishwa na kufuatwa.
Balozi wa Ukraine anayewakilisha nchi yake mjini Vatican
Andrii Yurash, Balozi wa Ukraine anayewakilisha nchi yao Vatican, pia alikumbuka hili wakati, mwishoni mwa Misa, alimshukuru Papa kwa "kujitolea kwake binafsi" kwa nchi, akiomba kuombea "wahanga wa vita, amani, na kupona haraka kwa Baba Mtakatifu. Leo, miaka 3 imepita wakati Ukraine imekuwa ikipinga, tunatoa wito kwa ajili ya amani ya haki na ya kudumu," Yurash alisema.