Tanzania:Papa amemteua Padre Josaphat Jackson Bududu kuwa Askofu mpya Msaidizi,Jimbo Kuu Tabora
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe 26 Februari 2025 amemteua Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora nchini Tanzania, Mheshimiwa Padre Josaphat Jackson Bududu, wa Jimbo kuu hilo hilo, ambaye hadi uteuzi huo alikuwa ni Makamu Msimamizi wa Baraza la Maisha ya Wakfu la Jimbo Kuu Katoliki la Taboara na Paroko wa Mtakatifu Yosefu huko Kipalapala, kwa kumpatia makao yake Vegesela ya Numidia.
Wasifu wake
Mheshimiwa Padre Josaphat Jackson Bududu alizaliwa tarehe 6 Machi 1977, huko Kaliua (Tabora). Majiundo yake: Falsafa katika Seminari Kuu ya Kibosho (Moshi) na Taalimungu katika Seminari Kuu ya Kipalapala(Tabora). Aliendelea na mafunzo ya Shada ya Udaktari wa Mafunzo ya Kiroho huko Tamil Nadu, katika Taasisi ya Kiroho na Taasisi ya Kipapa ya Mtakatifu Petro huko Bangalore (India).
Alipewa daraja Takatifu la Upadre, kunako tarehe 9 Julai 2009 kwa ajili ya Uklero wa Tabora.
Alifunika nyadhifa mbali mbali kama vile: Makamu Paroko(2009-2011) na Paroko (2015-2018) wa Parokia ya Mtakatifu Theresa, Tabora. Kuanzia 2019 alikuwa Mlezi katika nyumba ya Malezi ya Mario Mgulunde, kwa waseminari wa Jimbo kuu; Profesa katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Paulo Kipalapala; Paroko wa Mtakatifu Yoseph huko Kipalapala; Baba wa Kiroho wa Shirika la Mabinti wa Maria huko Tabora na Makamu Baraza la Watawa katika Jimbo Kuu la Tabora.