OSCE,Mons.Vitolo:Kukabiliana na chuki za mtandaoni na uwongo unaoendeshwa na AI
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Monsinyo Domenico Vitolo, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican katika Kanda za Shirikisho la Ushirikiano wa Kimataifa, Usalama na Maendeleo Barani Ulaya,(OSCE), tarehe 11 Februari 2025, alitoa hotuba yake katika kikao kuhusu kukomesha ubaguzi wa Kiyahudi katika Kanda hiyo. Kwa niaba ya Vatican alipenda kushukuru Uenyekiti wa OSCE wa nchini Finland kwa kuandaa, kwa kushauriana na Ofisi ya OSCE ya Taasisi za Kidemokrasia na Haki za Kibinadamu(ODIHR), Mkutano huu wa Kushughulikia Mapambano dhidi ya Wayahudi katika kanda za (OSCE). Mtazamo mpana wa Mkutano unaakisi mbinu kamili iliyochukuliwa na OSCE na Mataifa yake 57 yanayoshiriki kupigana na aina hii mbaya ya kutovumilia na ubaguzi. Mtazamo huo wa kina ni muhimu ili kupambana na aina zote za kutovumiliana na ubaguzi unaochochewa na chuki dhidi ya dini, huku ukizingatia umaalumu wa kila aina yake tofauti.
HESHIMA: Kushughulikia Kupinga ubaguzi wa kiyahudi katika kanda za OSCE:mwelekeo, vitisho na changamoto
Vatican bado ina wasiwasi mkubwa kuhusu kuongezeka kwa chuki dhidi ya Wayahudi katika maeneo mbalimbali ya Shirikisho la Ushirikiano wa Kimataifa, Usalama na Maendeleo Barani Ulaya,(OSCE). Mielekeo hii inadhihirishwa kwa njia mbalimbali, kama vile kukana Mauaji ya Wayahudi, kuhalalisha matukio ya chuki dhidi ya Wayahudi, vuguvugu linalokua likiwalenga Wayahudi na kuchochea hisia za chuki dhidi yao, na mbaya zaidi, mauaji. Viashiria vyote vilivyopo vinathibitisha ongezeko, Mashariki na Magharibi mwa Vienna, la kutovumiliana na ubaguzi unaochochewa na chuki dhidi ya Wayahudi. Kwa hakika, mashambulizi ya Hamas kote Israel tarehe 7 Oktoba na ghasia zilizofuata katika Mashariki ya Kati yameibua wimbi la ubaguzi na chuki dhidi ya Wayahudi na Waislamu.
Papa Francisko aliathibitisha kwamba, “ulinzi wa mahali pa ibada […] ni wajibu wa mamlaka ya kiraia, bila kujali ushawishi wao wa kisiasa au imani ya kidini.” Kiukweli, mashambulizi yote dhidi ya mahali pa ibada na maeneo ya kidini yanapingana na kanuni na roho ya haki ya uhuru wa mawazo, dhamiri, dini, au imani. Kwa hiyo Vatican inasisitiza uungaji mkono wake kwa kazi ya ODIHR katika kushughulikia mahitaji ya usalama ya jumuiya za Kiyahudi na zile za jumuiya nyingine za kidini. Njia nyingine inayotia wasiwasi ni kupunguzwa na matumizi mabaya ya mauaji ya kimbari, hasa kuhusiana na migogoro inayoendelea katika Kanda la OSCE na zaidi. Watu wa Kiyahudi wameteseka sana kwa nyakati tofauti na katika maeneo mengi, lakini mauaji ya kimbari hakika yalikuwa mateso mabaya zaidi ya yote. Unyama ambao Mayahudi waliteswa nao na kuuawa wakati huo ni zaidi ya uwezo wa maneno. Kwa hiyo, umoja na upekee wa Kumbu kumbu ya mauaji ya kimbari hufanya aina yoyote ya ulinganisho na matukio kama hayo kutokubalika.
JIBU: enzi za teknolojia, Akili Mnemba (AI) na mitandao ya kijamii
Maneno dhidi ya Wayahudi yalikuwepo muda mrefu kabla ya enzi ya kidijitali, lakini mtandao na utumizi mkubwa wa mitandao ya kijamii umesababisha mabadiliko makuu. Hakika, maudhui ya chuki dhidi ya Wayahudi kwenye mitandao ya kijamii yana hadhira ya kimataifa na yanaweza kusambazwa kwa urahisi kupitia upanuzi wa mwenendo wa kimashine kukiwa na athari ya kuzidisha kusiko kifani. Zaidi ya hayo, waundaji wa maudhui wanaweza kuficha utambulisho wao, na hivyo kufanya iwe vigumu kwa mamlaka kuwashtaki waliohusika. Jambo hili la kutisha linazidishwa na Akili Mnemba, ambayo inaweza kuzalisha "maudhui yaliyodanganywa na habari za uwongo ambazo zinaweza kupotosha watu kwa urahisi kutokana na kufanana kwake na ukweli" kwa lengo la kudanganya au kusababisha madhara.
Vatican imesisisitiza mara kwa mara kwamba uhuru wa kujieleza, kama haki nyingine zote za binadamu, unabeba majukumu ambayo hayawezi kupuuzwa. Iwapo haki zile zile ambazo watu wanazo nje ya mtandao zinalindwa mtandaoni, wajibu na majukumu yanayolingana ambayo watu wanayo nje ya mtandao lazima pia yadaiwe mtandaoni. Ili kukabiliana na chuki ya mtandaoni na uwongo unaoendeshwa na AI “si kazi ya wataalam wa tasnia pekee, inahitaji juhudi za watu wote wenye nia njema. Iwapo teknolojia itatumikia hadhi na si kuidhuru, na ikiwa ni kuendeleza amani badala ya vurugu, basi jumuiya ya binadamu lazima iwe makini katika kushughulikia mielekeo hii kwa heshima ya hadhi na uendelezaji wa wema.” Katika muktadha huu, umakini maalum unapaswa kulipwa kwa jukumu la watoa huduma za mtandao na huduma za mitandao ya kijamii. Kanuni za maadili zinaweza kuwa na jukumu muhimu, alimradi zimekusudiwa kwa uzito na kutekelezwa kwa uangalifu, lakini hali wakati mwingine zinaweza kuhitaji kuingilia kati kwa Serikali .
Kujiandaa: Jukumu la elimu, ufahamu wa umma na mazungumzo
Vatican ina hakika kwamba hakuwezi kuwa na dhamira ya ufanisi wa chuki dhidi ya Wayahudi, isipokuwa tathmini ya makini ya tatizo na hisia ya heshima kwa jumuiya za Kiyahudi zitaendelezwa kupitia elimu. Ni kwa njia ya mbinu ifaayo tu ya kielimu ndipo chuki dhidi ya Wayahudi na ubaguzi vitaweza kupigwa vita ipasavyo na endelevu. Ujinga, chuki na dhana potofu huchangia chuki dhidi ya Wayahudi katika jamii zetu; elimu inaweza kujenga ngome dhidi yao kwa kuifanya jamii yetu - na hasa watoto na vijana - kufahamu wajibu wa pamoja wa kulinda utu wa watu wote. Vatican imejitolea kwa dhati kukuza mazungumzo ya kiekumene na ya kidini katika ngazi mbalimbali.
Kwa kuzingatia hasa uhusiano kati ya Kanisa Katoliki na watu wa Kiyahudi, ambayo inashiriki urithi wa pamoja wa kiroho, Tume ya Mahusiano ya Kidini na Wayahudi inahakikisha nafasi ya mazungumzo, ya kuheshimiana, ya kukua kwa urafiki, na kwa ushuhuda wa pamoja katika kukabiliana na changamoto za wakati wetu, ambazo zinatusukuma kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya ubinadamu. Kwa kumalizia, Vatican inapenda kurudia shukurani zake kwa Uenyekiti wa Shirikisho la Ushirikiano wa Kimataifa, Usalama na Maendeleo Barani Ulaya, (OSCE) wa Finland kwa kuandaa Mkutano huo, katika mwaka huu ambao unaadhimisha miaka 80 ya ukombozi wa kambi ya maangamizi ya Auschwitz-Birkenau. Katika kuadhimisha ukumbusho huu, Papa Francisko hivi karibuni alisisitiza kwamba: “kutisha la kuangamizwa kwa mamilioni ya Wayahudi na watu wa imani nyinginezo katika miaka hiyo haliwezi kusahaulika wala kukataliwa.”