杏MAP导航

Tafuta

Ni katika muktadha wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Ndoa na Familia, Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles, kuanzia tarehe 7 hadi tarehe 14 Februari 2025, Sikukuu ya Mtakatifu Valentino. Ni katika muktadha wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Ndoa na Familia, Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles, kuanzia tarehe 7 hadi tarehe 14 Februari 2025, Sikukuu ya Mtakatifu Valentino.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Maadhimisho ya Juma la Ndoa na Familia: Tunu Msingi za Kifamilia

Maisha ya ndoa na familia ni chemchemi ya matumaini na nguvu ya pekee kwa wanandoa, ni kielelezo cha imani, mapendo na matumaini na mwanzo wa ujenzi wa familia, Kanisa dogo la nyumbani, mahali ambapo imani, matumaini na upendo vinamwilishwa, chachu ya mabadiliko katika maisha. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha utamaduni unaothamini na kuenzi ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maisha ya ndoa na familia yanayojikita katika upendo kamili kati ya Bwana na Bibi ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa, kwani wanandoa kimsingi wanashiriki katika kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi binadamu. Agano la ndoa, ambalo kwa njia yake, mwanaume na mwanamke huunda kati yao jumuiya kwa maisha yote, kwa tabia yake ya asili liko kwa ajili mafao yao na kwa ajili ya kuzaa na kulea watoto. Agano hili kati ya wabatizwa, limeinuliwa na Kristo Bwana kwa hadhi ya Sakramenti. Ni agano ambalo linajikita katika uaminifu na udumifu mambo msingi katika upendo unaohimizwa na Mama Kanisa kwa watoto wake. Hii ndiyo changamoto kubwa inayotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kufanya maamuzi machungu katika maisha yao kwa kuchagua na kuamua kufunga Sakramenti ya ndoa, inayodumu hadi pale kifo kitakapowatenganisha, hapa watu wanapaswa kuachana na tabia ya kubabaisha bila ya kuwa na msimamo thabiti wa maisha, kwa kutambua kwamba, uaminifu na udumifu ni mambo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Leo kuna watu wengi wanaosita kufanya maamuzi magumu katika maisha yao, kwa kuogopa kushindwa katika maisha; kwa kugubikwa na ubinafsi pamoja na uchoyo unaohofia kuharibu uhuru wa mtu. Hapa Mama Kanisa hana budi kujiwekea mikakati ya kichungaji itakayosaidia kuwahudumia waamini waliotalakiana na kuamua kuoa au kuolewa tena. Maaskofu waangalie uwezekano wa waamini hawa kuruhusiwa kushiriki katika maisha pamoja na Mafumbo ya Kanisa. Mikakati hii iwasaidie wanandoa watarajiwa kujiandaa kikamilifu katika utume na maisha ya ndoa na familia. Matunda ya muungano kati ya bwana na bibi ni watoto, ambao wote hawa wanaunda na kujenga familia, tayari kurithisha zawadi ya uhai, imani, maadili na utu wema. Familia ina umuhimu wa pekee kwani huu ni urithi wa binadamu. Bila familia, matumaini ya mwanadamu yako mashakani kama anavyobainisha Kardinali Walter Kasper, Rais mstaafu wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo.

Bila familia, matumaini ya mwanadamu yako mashakani
Bila familia, matumaini ya mwanadamu yako mashakani   (Vatican Media)

Idadi ya wazee Barani Ulaya inazidi kuongezeka maradufu, lakini watoto wanaozaliwa ni wachache sana. Hii ni changamoto kubwa kwa familia nyingi Barani Ulaya. Hii ni kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, kiasi kwamba, wazazi wenyewe hawana matumaini, kumbe wasingependa watoto wao baadaye kuteseka na kuhangaika. Lakini, waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kufanya maamuzi yanayowawajibisha, kwa kuwa na matumaini pamoja na ujasiri wa kurithisha zawadi ya uhai, maadili na utu wema kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya kizazi cha sasa na kile kijacho. Familia nyingi Barani Ulaya zina idadi ndogo sana ya watoto, changamoto na mwaliko kwa Wakristo kuendelea kutangaza Injili ya Familia kwa njia ya ushuhuda wa maisha ya imani inayomwilishwa katika matendo. Ubaridi kwa ajili ya maisha ya ndoa na familia unasababisha changamoto kubwa katika maisha ya kijamii, kiasi kwamba, leo hii familia ni kati ya taasisi zinazoshambuliwa na kukashifiwa sana na zenye changamoto nyingi. Uhuru, uaminifu na udumifu ni chanda na pete, kwani gharama ya uhuru ni kubwa kwa mtu ambaye ni mwaminifu na kwamba, uhuru ni zawadi ya uaminifu. Mababa wa Kanisa wanasema, Familia ni Kanisa dogo la nyumbani; ni shule ya tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kimaadili na kijamii. Familia ni tabernakulo ya Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; ni mahali pa kufundana umuhimu wa kumwilisha: huduma, upendo, ukarimu, msamaha na kuvumiliana. Hapa ni madhabahu ya sala, ibada, na tafakari ya Neno la Mungu; mambo msingi yanayowawezesha wanafamilia kujivika upendo, busara, rehema, utu wema, upole na unyenyekevu. Tunu hizi msingi za maisha ya ndoa na familia kwa sasa ziko hatarini kutokana na taasisi ya familia kupigwa vita kana kwamba ni “Mbwa koko!! Lakini, Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kusimama kidete kulinda, kudumisha, kutangaza na kushuhudia Injili ya Ndoa na familia.

Familia Kanisa Dogo la Nyumbani, Kanisa la Kisinodi na Kimisionari
Familia Kanisa Dogo la Nyumbani, Kanisa la Kisinodi na Kimisionari   (Vatican Media)

Waamini hawana budi kusimama kidete katika misingi ya imani, maadili na utu wema sanjari na kukataa kishawishi cha utengano na kinzani katika maisha ya ndoa na familia kwani waathirika wakuu ni watoto. Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Amoris laetitia” uwe ni dira na mwongozo katika utume na maisha ya familia ya Kikristo hatua kwa hatua. Kanisa litaendelea kuwa na jicho la kichungaji kwa ajili kuzisaidia familia za Kikristo kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wake katika malezi na makuzi ya watoto wao pamoja na kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zinazojitokeza katika maisha na utume wa familia katika mwanga wa Injili na utu wema! Familia ya Kikristo inasimikwa katika Sakramenti ya Ndoa; muungano imara kati ya bwana na bibi, alama ya upendo wa Mungu kwa binadamu, ambao Kristo Yesu, ameukabidhi kwa Kanisa lake kuumwilisha katika maisha na utume wake. Agano la ndoa linajikita katika upendo usiogawanyika na endelevu; malezi na makuzi ya watoto; umoja na udugu kama chachu ya ujenzi wa jamii inayojikita katika udugu, upendo na mshikamano. Ni katika muktadha wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Ndoa na Familia, Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles, kuanzia tarehe 7 hadi tarehe 14 Februari 2025, Sikukuu ya Mtakatifu Valentino. Hii ni siku ambayo Kanisa linamkumbuka na kumuenzi Mtakatifu Valentino aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya malezi na makuzi ya vijana wa kizazi kipya, akiwafunda na kuwaelekeza katika maadili na utu wema. Aliwataka vijana kuachana na tabia ya “uchumba sugu” na badala yake akawaelekeza wafunge ndoa takatifu na kuishi maisha adili yanayompendeza Mungu na jirani. Vijana wengi walihamasika kufunga ndoa takatifu, jambo lililomtia “kichefuchefu” Mfalme Aureliona na hivyo “kuchafua hali ya hewa” kiasi cha kuamuru akatwe kichwa kunako mwaka 273, ili kutoa nafasi kwa vijana wengi kujiunga na Jeshi. Mtakatifu Valentino alijitosa kuwatetea vijana kuwa na wenzi wao wa ndoa, ili hata wao waweze kujenga familia, Kanisa dogo la nyumbani! Baba Mtakatifu Francisko anawatakia wanandoa watarajiwa heri na baraka pamoja na kuwahakikishia wote wanaopendana sala na maombezi yake! Katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anakaza kusema, mwanadamu ameumbwa ili kupenda na kupendwa. Katika Ndoa Takatifu, huu ni umoja ambao ni chimbuko la maisha na utimilifu wa maisha!

Familia ni Kanisa Dogo la Nyumba, shule ya sala, haki na amani
Familia ni Kanisa Dogo la Nyumba, shule ya sala, haki na amani   (Vatican Media)

Sikukuu ya Wapendanao iwakumbushe walimwengu kwamba, upendo una ganga na kuponya na hizi zinapaswa kuwa ni hisia za kweli. Kwa mtu asiyefahamu kupenda, kupendwa kwake kunageuka kuwa ni janga katika maisha. Upendo wa kweli ni amana na utajiri mkubwa katika maisha ya mwanadamu! Inapendekezwa: Kuongeza ufanisi katika kutambua ukatili wa kijinsia unaofanywa na wenza katika maisha ya ndoa na familia. Kutoa taarifa pale unapoona unafanyiwa ukatili mapema iwezekanavyo na kuomba msaada kwa kupaza sauti, ili sheria iweze kuchukua mkondo wake, haki, amani na utulivu kuweza tena kutawala. Elimu itolewe kwa jamii kuhusu Haki Msingi za Binadamu, haki za wanawake na ukatili wa kijinsia. Huu ni mwaliko wa kuachana kabisa na mila potofu na imani zinazoathiri usawa wa kijinsia na kuwafanya wanawake kuonekana dhaifu. Umefika wakati wa kuongeza madawati ya jinsia na kuongeza pia muda wa kuhudumia. Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles, linasema, maisha ya ndoa na familia ni muhimu sana kwa familia na jamii katika ujumla wake, na hasa mwaka huu 2025, Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji wa Matumaini”, ndoa na familia iwe ni chemchemi ya uaminifu na udumifu unaofumbatwa katika Sakramenti ya Ndoa kati ya Bwana na Bibi; kielelezo cha Agano kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu, kwa ajili ya wokovu wa wanandoa na jamii katika ujumla wake. Maisha ya ndoa na familia ni chemchemi ya matumaini na nguvu ya pekee kwa wanandoa, ni kielelezo cha imani, mapendo na matumaini na mwanzo wa ujenzi wa familia, Kanisa dogo la nyumbani, mahali ambapo imani, matumaini na upendo vinamwilishwa, chachu ya mabadiliko katika maisha. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha utamaduni unaothamini na kuenzi ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu, chimbuko la jamii yenye furaha. Maadhimisho ya Juma la Ndoa na Familia nchini Uingereza na Walles imekuwa ni fursa kwa wanandoa kupyaisha tena maagano yao, muda wa sala na tafakari; malezi ya awali na endelevu kwa wanandoa wapya; umuhimu wa kusamehe na kusahau bila kusahau wajibu wa kupyaisha upendo wao siku kwa siku!

Juma la ndoa na familia
13 Februari 2025, 14:26