Askofu Ni Mtetezi na Shuhuda Wa Kweli za Kiinjili
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Askofu anaalikwa kuwa ni mtetezi na mtangazaji wa kweli za Kiinjili katika maisha na huduma yake kwa kutambua kwamba, kama Askofu ni msaidizi wa karibu sana wa Askofu wa Roma. Hayo yamesemwa na Kardinali Claudio Gugerotti, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki, Jumatano jioni, tarehe 19 Februari 2025 wakati wa Ibada ya Misa Takatifu ya kumweka wakfu Monsinyo Filippo Ciampanelli aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki. Ibada hii ya kuwekwa wakfu imehudhuriwa na mahujaji kutoka Jimbo Katoliki la Novara, waliokuwa wanahitimisha hija ya matumaini kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Katika maisha na utume wake Askofu Filippo Ciampanelli ametekeleza maisha na utume wake wa kidiplomasia nchini: Georgia, Armenia, Azebaigian na Belarus. Kardinali Claudio Gugerotti amesali na kumwombea Baba Mtakatifu Francisko ili aweze kupona haraka na hivyo kuendelea na maisha pamoja na utume wake. Kristo Yesu katika Sala yake ya Kikuhani aliwahimiza wafuasi wake kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na Fumbo la Utatu Mtakatifu na kati yao wenyewe.
Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kujitambua kwamba, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, mwaliko kwa watu wa Mungu kujikita katika: Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na ushuhuda unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili na hivyo wanakuwa ni wawezeshwaji wa Mungu yaani “Capax Dei.” Ni changamoto kubwa kwa Askofu kuwa ni mtetezi na mtangazaji wa kweli za Kiinjili na matokeo yake anaweza kujikuta akijifungia katika ulimwengu na ubinafsi wake. Kumbe huu ni mwaliko wa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Aendelee kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa ajili ya maskini, wagonjwa na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani wote hawa wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Askofu Filippo Ciampanelli aendelee kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu. Ajitahidi kuwa ni ufunuo wa Mungu katika huduma yake licha ya kutumia muda mwingi akiwa ofisini.
Itakumbukwa kwamba, Uaskofu ni utimilifu wa Daraja Takatifu ya Upadre, ambamo Askofu aliyewekwa wakfu anapewa dhamana ya: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Askofu ni kielelezo cha ukuhani mkuu, kilele cha huduma takatifu. Maaskofu kwa namna iliyo ya juu kabisa, hushika nafasi ya Kristo Kristo Yesu mwenyewe, aliye mwalimu, mchungaji na kuhani na kwamba, Maaskofu wanatenda kazi yao katika nafsi yake. Kwa njia ya Roho Mtakatifu, Maaskofu wanafanywa walimu kweli na halisi wa imani, makuhani na wachungaji. Maaskofu wamewekwa wakfu ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Kristo Yesu sanjari na kuendeleza kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Kristo, Kuhani mkuu na wa milele. Kristo kwa njia ya Maaskofu, anaendelea kutangaza Habari Njema na kuwatakatifuza waja wake kwa njia ya Sakramenti za imani, kiasi hata cha kuliwezesha Kanisa kupata watoto wapya wanaozaliwa kwa Maji na Roho Mtakatifu. Kristo Yesu anaendelea kuliongoza Kanisa lake kwa busara na hekima, kazi inayopaswa kutekelezwa na Maaskofu wanapowaongoza watu wa Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani, ili hatimaye, waweze kufikia furaha ya maisha ya uzima wa milele. Maaskofu wanatakiwa kuonesha nidhamu na heshima kubwa kwa Daraja waliyoipokea kama wagawaji wa Mafumbo ya Mungu, mashuhuda wa Injili ya Kristo na Mitume wa Roho Mtakatifu anayetakatifuza, mwaliko kwa waamini kuwasikiliza Maaskofu wao kwa dhati kabisa kama ushuhuda wa kumsikiliza Kristo mwenyewe!
Maaskofu wanakumbushwa kwamba, wameteuliwa kutoka miongoni mwa watu wa Mungu na hivyo kuwekwa wakfu kwa ajili ya mambo ya Mungu. Hili si Daraja kwa ajili ya kujitafutia mali na malimwengu yake, wala si jukwaa la kisiasa, bali Uaskofu ni kwa ajili ya huduma na kwamba, wanapaswa kukikimbia kishawishi cha kutaka kuwa Wafalme na watawala. Maaskofu watangaze Neno la Mungu; wawaonye watu na kufundisha kwa ari na moyo mkuu tunu msingi za Kiinjili. Kwa njia ya sala na sadaka yao, wawatakatifuze watu wa Mungu ili hatimaye, waweze kupata utimilifu wa utakatifu katika Kristo Yesu. Dhamana ya kwanza ya Askofu ni kusali, kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kumbe, ni wajibu wa Maaskofu kuhakikisha kwamba, wanasali daima kama sehemu ya utekelezaji wa wito wao. Wamekabidhiwa na Mama Kanisa dhamana ya kuwa ni walinzi na waadhimishaji wa Mafumbo ya Kanisa; wakuu wa familia ya Mungu, changamoto na mwaliko wa kumfuasa Kristo Yesu, Mchungaji mwema anayewafahamu Kondoo wake kwa majina na wao wanamtambua kiasi kwamba, akawa tayari kuyamimina maisha yake kwa ajili yao! Maaskofu wanapaswa kuwapenda na kuwathamini watu wao kwa dhati, lakini zaidi waoneshe umoja na mshikamano na wakleri, wadau wakuu katika utume wao kama Maaskofu.
Wakleri wawe na fursa ya kuweza kukutana na kuzungumza na Maaskofu wao bila mizengwe mizengwe. Maaskofu wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii; watu wanaohitaji kuonjeshwa huruma pamoja na kupewa msaada wanaohitaji. Maaskofu wajitahidi kushirikiana na kushikamana na waamini walei katika maisha na utume wao; kwa kuwasikiliza na kuwathamini. Waoneshe ari na moyo wa majadiliano ya kiekumene na kidini; kwa kujali na kuguswa na mahangaiko ya Makanisa mengine yanayohitaji pia msaada wa hali na mali. Baba Mtakatifu Francisko daima anawataka Maaskofu kukesha na kusali katika upendo kama mashuhuda wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, ambao wamewekwa wakfu ili kuwa waalimu, makuhani na wachungaji. Roho Mtakatifu awasaidie Maaskofu kudhibiti udhaifu wao wa kibinadamu kwa kuambata huruma na neema ya Mungu!