杏MAP导航

Tafuta

Vatican imetoa mwongozo juu ya matumizi ya Akili Mnemba. Vatican imetoa mwongozo juu ya matumizi ya Akili Mnemba. 

Vatican.Miongozo ya AI:hadhi ya binadamu,maadili,usalama na uwazi!

Kanuni za miongozo ya masuala ya Akili Mnemba(AI)inayojikita katika hadhi ya binadamu,maadili,usalama na uwazi kwa mujibu wa Serikali ya Mji wa Vatican, iliyochapishwa hivi karibuni.Matumizi ya kimaadili na ya uwazi ya data yamesisitizwa,ikiwa ni pamoja na ulinzi wa data za kibinafsi.Kanuni za faragha lazima ziheshimiwe, bila kusababisha ubaguzi au kudhoofisha hadhi ya binadamu.Lugha lazima iwe wazi na inayoeleweka kwa watumiaji,ikihakikisha haki ya kupinga uchakataji wa data.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kuheshimu hadhi na utu, usalama, uwazi na maadili ya binadamu. Hizi ndizo kanuni zilizoongoza kuandikwa kwa Miongozo kuhusuana na suala la Akili Mnemba(AI), iliyochapishwa tarehe 16 Januari 2025 katika Tovuti ya Mji wa Vatican. Siku kumi na tano baada ya kuanza kutumika, pamoja na Amri kifungu cha(702) cha Tume ya Kipapa kwa ajili ya Serikali ya Vatican, na inasubiri utekelezaji wa sheria na kanuni kwa ajili ya matumizi yake, ni fursa ya kupitia  tena mambo ya msingi. Mwongozo huu unaweka kanuni na sheria za matumizi ya kimaadili, kuwajibika na kudhibitiwa  kuhusu masuala ya Akili Mnemba (AI) katika Serikali ya Mji wa  Vatican. Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba utafiti, maendeleo na matumizi ya Akili Mnemba yanaelekezwa kuelekea manufaa ya wote, ambayo huwaweka watu katikati ya kila matumizi yake. Miongozo inashughulikia masuala kadhaa ya sasa. Miongoni mwa haya ni maadili na uwazi. Hii inahusisha sio tu ulinzi wa utu wa binadamu, lakini pia kupitishwa kwa mifumo ambayo inapatikana kwa urahisi na kudhibitiwa na watumiaji. Katika muktadha huo, uwazi ni muhimu kabisa ili kukuza uaminifu katika matumizi ya Akili Mnemba na kuhakikisha kuwa maamuzi yanayochukuliwa na mifumo ya kiotomatiki ni wazi na yanaambatana na kanuni za maadili.

Kipengele kingine ambacho hati inashughulikia ni mwelekeo wa kumweka mwandamu katikati na kuegemea. Akili Mnemba, kamwe haiwezi kuchukua nafasi ya mwanadamu na lazima iheshimu uhuru wake. Kiukweli, ni lazima iwe katika huduma ya mtu na si kumtawala, ili maamuzi ya mwisho daima yawe ni ya mwanadamu. Kipengele muhimu sana ni usalama wa data na ulinzi. Miongozo inasisitiza haja ya usalama na usiri wa data, hasa data ya kibayometriki.( biometrici). Kwa maana hiyo, kupitishwa kwa Akili Mnemba lazima kila wakati kuwe katika jina la ulinzi ili kuepuka matumizi yasiyofaa ya data. Kisha kuna haja ya kutokuwa na ubaguzi na uendelevu. Kutobagua kunalenga kuepusha chuki dhidi ya watu. Zaidi ya hayo, uendelevu wa kiuchumi na kimazingira ni uwekezaji muhimu ili kupitisha teknolojia mahiri, ambazo zina matokeo chanya kwa muda mrefu.

Kipengele kingine cha kuzingatia ni usimamizi na udhibiti. Katika muktadha huo, ufuatiliaji unaoendelea wa usimamizi na usindikaji wa data unahitajika. Lengo ni kuhakikisha kuwa matokeo yaliyopatikana ni sahihi na yanafaa, kwa kuzingatia kanuni za uwazi na uwiano. Kuhusu utangamano na utume wa Kanisa na Utawala wa Vatican, ni jambo la kufurahisha kuona jinsi ambavyo miongozo inavyoweka kwamba matumizi ya Akili Mnemba yasiharibu utume wa kichungaji wa Papa, wala kuathiri Kanisa, wala kuingia katika mgogoro na shughuli za kitaasisi za Vatican. Kwa sababu hiyo, tahadhari maalum inahitajika katika matumizi ya teknolojia katika muktadha ambao una mahitaji maalum ya maadili ya kimaadili. Mwongozo pia unajumuisha baadhi ya makatazo katika matumizi ya Akili Mnemba.

Kwanza, kuhusu ubaguzi na madhara ya kisaikolojia. Ni marufuku kabisa kuitumia kufanya vitendo vya kibaguzi, kama vile kauli zinazoweza kudhuru haki za binadamu au kusababisha madhara ya kisaikolojia au kimwili.  Jambo lingine muhimu linahusu upatikanaji wa Akili Mnemba kwa watu wenye ulemavu. Matumizi yake ni marufuku madhubuti ikiwa inazuia ufikiaji wa aina hii ya watu. Zaidi ya hayo, jambo la msingi, matumizi ya Akili Mnemba lazima yaheshimu usalama wa Serikali, utulivu wa umma na haiwezi kuwa na mgongano na utume wa Kanisa Katoliki. Miongozo pia inatoa sura iliyowekwa kwa Kanuni za Jumla kulingana na mada.

Kuanzia habari na kushughulikia data. Kwa maana hiyo, matumizi ya kimaadili na ya uwazi ya data yanasisitizwa, ikiwa ni pamoja na ulinzi wa data ya kibinafsi. Kanuni za faragha lazima ziheshimiwe, bila kusababisha ubaguzi au kudhoofisha hadhi ya binadamu. Zaidi ya hayo, lugha lazima iwe wazi na inayoeleweka kwa watumiaji, ikihakikisha haki ya kupinga uchakataji usio sahihi wa data. Katika uwanja wa utafiti wa kisayansi na huduma ya afya, Akili Mnemba inapaswa kutumika kuboresha huduma za afya na ulinzi wa afya. Lakini, bila kuathiri uhuru wa kufanya maamuzi wa madaktari. Jambo lingine la kuzingatia ni katazo la kukiuka umilikaji katika kazi za ubunifu na kisanii. Mwongozo unasisitiza kwamba maudhui yanayozalishwa kupitia Akili Mnemba lazima yatambulike na kwamba Serikali ishikilie haki za kiuchumi na uandishi kuhusu maudhui kama hayo yaliyoundwa katika eneo lake.

Eneo lingine ni la urithi wa kiutamaduni. Kuanzishwa kwa Akili Mnemba katika usimamizi wa urithi wa kiutamaduni lazima kuheshimu uadilifu wa mali na kanuni za kimataifa za urejeshaji na uhifadhi. Katika eneo la miundombinu na huduma, AI inaweza kutumika kuboresha uendelevu wa kiuchumi na kimazingira, lakini haipaswi kamwe kuathiri usalama au kupunguza maamuzi ya wataalam. Katika taratibu za utawala, inaweza kutumika kurahisisha na kuboresha ufanisi wao, lakini chaguo la kufanya maamuzi daima ni la kibinadamu. Ufuatiliaji wa athari za kanuni zinazohusiana na matumizi yake pia hupangwa.

Mahali pa kazi. Akili Mnmba inaweza kutumika kuboresha mafunzo ya wafanyakazi na usalama mahali pa kazi. Zaidi ya hayo, ni lazima iwe wazi katika uteuzi wa wafanyakazi, kuepuka ubaguzi na kuheshimu utu wa binadamu. Katika uwanja wa shughuli za mahakama, Akili Mnemba inaweza tu kutumika kwa shirika na kurahisisha kazi ya mahakama na kwa utafiti wa kisheria. Kwa hakika, haiwezi kamwe kuwa na jukumu katika maamuzi ya mwisho na kamwe haiwezi kuchukua nafasi ya hakimu katika hukumu yake.

Katika eneo la usalama, imeanzishwa kuwa utumiaji wa Akili Mnemba  utadhibitiwa na kanuni maalum ya utekelezaji. Hii ina maana kwamba kutakuwa na kanuni maalum ya kusimamia matumizi yake katika muktadha wa ulinzi na usalama. Katika suala hili, Mwongozo unaweka utaratibu wa kuundwa kwa Tume ya Akili Mnemba, ambayo huteuliwa na Gavana na inaundwa na wajumbe watano, wakiwemo maofisa kutoka Ofisi ya Sheria, Mifumo ya Mawasiliano na Habari, na Idara ya Usalama wa Habari na Ulinzi wa Raia. Kazi kuu za Tume ni pamoja na kuandaa sheria na kanuni za matumizi ya Akili Mnemba; maoni juu ya mapendekezo ya majaribio na matumizi ya mifumo katika eneo la Vatican. Lakini pia kuripoti hatari zinazowezekana kwa Serikali ya Mji wa Vatican. Pia inahitajika kuandaa ripoti ya kila miezi sita kuhusu athari za matumizi ya Akili Mnemba katika Serikali ya Mji wa Vatican. Muda wa kuhudumu kwa wajumbe wa Tume ni miaka mitatu, kukiwa na uwezekano wa kufanywa upya au kubadilishwa na Rais Mtawala wa Mji wa Vatican. Masharti mapya yanathibitisha wazi kwamba Akili Mnemba  katika  mji wa Vatican lazima utumike kwa tahadhari kubwa na mdogo kwa sekta fulani, kama vile shirika la kazi ya mahakama na utafiti, lakini kamwe isichukue nafasi ya maamuzi ya binadamu. Ni muhimu kwa Miongozo wa Akili Mnemba kwamba iwe msaada kwa maamuzi ya binadamu na si mbadala, kulingana na utume wa kitaasisi wa Mji wa Vatican. Taharifa hii unaweza kuipata pia kwenye mji wa Vatican kwa kubonyeza hapa:.

Mwongozo wa AI katika mji wa Vatican
21 Januari 2025, 15:08