Ufunguzi wa Mlango wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Mkuu:Maria ni Kitovu cha Wakati
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kuguswa kwa kengele ya kwanza ni ile iitwayo "Sperduta", kengele ya kihistoria ambayo imerejea kulia tena huko Mtakatifu Maria Mkuu baada ya kuvunjwa mnamo 1884 na kuwekwa kwenye Makumbusho ya Vatican na Papa Leo XIII. Ni kengele hii iliyotangaza kufunguliwa kwa Mlango Mtakatifu katika Basilika ya Mtakatifu Maria Mkuu ambayo kwa juu inatazama Roma yote. Kwa njia hiyo: "Nifungulieni milango ya haki, nitaingia kumshukuru Bwana,” ndiyo sala ya hitimisho ambapo baada ya kusomwa iliwezekana kufunguliwa Mlango Mtakatifu wa nne jijini Roma uliofunguliwa tangu mwanzo wa Jubilei (baada ya Milango: Mtakatifu Pietro(24 Desemba, Kanisa la gereza la Rebibbia(26 Desemba, lililofunguliwa na Papa Francisko, na Basilika ya Mtakatifu Yohane Laterano 29 Desemba) na kwa njia hiyo katika Mwaka mpya tarehe 1 Januari 2025 sambamba na siki kuu ya Maria Mama wa Mungu. Kardinali Rolandas Makrickas, Mkuu wa Kanisa la Kipapa la Mtakatfu Maria Mkuu amelifungua. Kardinali Rolandas Makrickas, baada ya masomo na Injili alitoa mahubiri yake kwa kuanza kusema kuwa Hatua za kwanza za mahujaji wa Mwaka wa Jubilei, katika Kanisa hili la Kipapa lililowekwa wakfu kwa ajili ya Mama wa Mungu, ziliambatana na sauti ya kengele ya kale ya patakatifu hapa ijulikanayo kama "della Sperduta".
Sauti ya Mama wa Mungu anayetuita– “La Campana della Sperduta” yaani “Kengele iliyopotea”
Kardinali Rolandas Makrickas, aliendelea kusema kuwa “ Kutoka juu ya (Esquiline)kilele, sehemu ya juu kabisa katikati ya Roma, tangu Jubilei ya kwanza ya Kanisa inaendelea kueneza sauti yake katika Mji wa Milele, kwa faraja ya kila mhujaji. Sauti ya kengele hii haiashirii saa na nyakati za maombi tu, bali inabadilisha kuwa sauti taswira ya kimapokeo inayohusishwa na Maria, ile ya mwongozo na alama, Stella Maris, (Nyota ya Bahari ambayo huangaza njia katika giza la usiku. Si tu sauti ya yule Aliyepotea bali pia maneno ya mtume Paulo: “Hata ulipotimia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe aliyezaliwa na mwanamke” (Gal 4:4). Leo tunagaangazwa na kuongoza tafakari yetu katika Ekaristi hii Takatifu, katika Maadhimisho ya Maria Mama wa Mungu na katika hali ya ajabu ya kufunguliwa kwa Mlango Mtakatifu wa Kanisa hili la Kipapa.
Wakati - kiumbe mkuu wa Mungu
Mkuu wa Kanisa la Mtakakatifu Maria Mkuu alisisitiza kuwa Usemi “mtimilifu wa wakati” unashangaza. Huu ndio utimilifu wa wakati: Mungu anapofanyika mwili na kufanya hivyo ndani ya tumbo la mwanamke, Maria. Yeye ndiye njia iliyochaguliwa na Mungu; Yeye ndiye mahali pa kuwasili kwa watu wengi na vizazi ambavyo vimetayarisha ujio wa Bwana ulimwenguni. Wakati unapata utimilifu wake unapounganishwa na umilele, yaani, na wakati usio na mwisho wa Mungu. Wakati ni kiumbe mkuu wa Mungu. Mara nyingi na kwa njia tofauti binadamu alitaka kuongeza au kukamilisha wakati na teknolojia mpya, lakini kila jaribio mwisho wake ni katika hasara yake au katika kile ambacho tunaweza kufafanua kama "wakati wa uchovu". Inatosha kufikiria kompyuta au simu za mkononi: iliyoundwa ili kuokoa na kuimarisha muda, mara nyingi huwa adui zake mbaya zaidi. Hata hivyo, mtu hawezi kamwe kuhisi amepotea au amechoka kwa muda uliotumiwa na Mungu. Mama Bikira ndiye kiini cha wakati huu: Mungu alifurahi kubadilisha historia na wakati wetu kupitia Yeye, Mwanamke Msafi wa watu waliochaguliwa.
Picha ya Salus Populi Romani - Mama anayejua nyakati na dharura za watoto wake
Kardinali Roland aliendelea kusema kuwa “ Leo tunaheshimu kwa namna ya pekee sanamu ya Maria Mama wa Mungu iliyoitwa katika Kanisa hili kwa jina la Salus Populi Romani. Ni ibada ya Roma na ya kila mwamini wa ulimwengu kuelekea kwa Bikira Maria. Miaka saba iliyopita, wakati wa Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa katika Kanisa Kuu hili, Baba Mtakatifu Francisko alikumbusha kwamba: “…Mama hulinda imani, hulinda mahusiano, huokoa katika hali mbaya ya hewa na hulinda dhidi ya uovu. Mahali ambapo yupo Mama, nyumbani shetani haingii. Mahali ambapo Mama yuko, usumbufu haushindi, hofu haishindi. Ni nani kati yetu asiyehitaji hili, ni nani kati yetu wakati mwingine hana shida au wasiwasi? Ni mara ngapi moyo ni bahari ya dhoruba, ambapo mawimbi ya matatizo yanaingiliana na upepo wa wasiwasi hauacha kuvuma!”
Maria ni safina salama katikati ya gharika
Haitakuwa mawazo au teknolojia ambayo yanaleta faraja na matumaini, lakini uso wa Mama wa Mungu." Mikono ya Maria inabembeleza maisha yetu, vazi lake hutulinda, kama vile alivyotulinda mikononi mwake - mikono ya mmoja wetu! - Mtoto Yesu katika hori. Kila hujaji atakayevuka kizingiti cha Mlango Mtakatifu wa mahali patakatifu pa Maria wa Magharibi katika Mwaka wa Jubilei, atasali mbele ya Picha ya Mama wa Mungu, Salus Populi Romani, na mbele ya Utoto Mtakatifu wa Yesu na Yeye, hutaweza kuondoka hapa bila kuhisi msisimko fulani. Hisia na uhakika kwamba Mama wa mbinguni yuko pamoja naye. Kila mtu ataanza kutoka hapa akiwa na uhakika wa kusindikizwa na neema, ulinzi, matunzo na huruma ya kimama ya Maria.” Mkuu wa Kanisa la Kipapa alisema Mwishowe, kwenda kwetu Kwake kunakuwa kuja kwake kwetu na pamoja nasi. Hisia hii ya kiroho pia inawasilishwa na usemi wa kisanii wa Picha inayoheshimiwa ya Maria. Sanamu takatifu ya Salus inabebwa na Malaika. Ingawa picha ya Maria bado ina sifa, yeye yuko katika harakati kila wakati: Malaika humleta kwetu na anataka kutusindikiza na kila hatua ya maisha yetu. Kama vile alivyomsindikiza Mwanawe Yesu - tangu kuzaliwa hadi kufa, katika nyakati za furaha na saa za giza za uchungu -Yeye, kama Mama, husindikiza Kanisa zima na kila mwamini kuelekea Mwanawe. Bikira Maria, Mama wa Mungu na Mama yetu, kama vile alivyoamua katika utimilifu wa wakati, ndivyo anavyoamua kwa maisha ya kila Mkristo. Kwa sababu hakuna anayejua nyakati na dharura za watoto wake kuliko Mama.
Kitanda kitakatifu - Shahidi wa kimya wa kuzaliwa kwa Yesu
Hatua za mahujaji wa matumaini wa Jubilei hii, katika Kanisa hili la Kipapa, linaloitwa pia Bethlehemu ya Magharibi, zitasimama pia mbele ya masalia ya Utoto Mtakatifu, nyumba ya kwanza ya unyenyekevu na maskini ya Yesu. Kutokana na ushuhuda huu wa kimya wa kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu, ubinadamu ulianza kuhesabu miaka ya enzi ya Ukristo. Kwa njia hiyo Kardinali alisisitiza kuwa “tufikirie juu yake: wakati wetu unafafanuliwa hasa kuanzia kwenye kitanda kitakatifu hicho! Wakristo wa kwanza kuhiji kwenye hori la Yesu walikuwa wachungaji. Kuanzia mashambani kuelekea kwenye zizi dogo la Bethlehemu, wachungaji, katika usiku ule mtakatifu, wana kiini cha Ukristo: wakitoka kwenda kumlaki Bwana, wakiifuata nyota yake. Madhabahu hii ya kale ya Maria iko katikati ya Roma, katikati ya muundo wa barabara yenye umbo la nyota ambayo huamsha Nyota ya Bethlehemu. Inajumuisha kikamilifu utume wa Basilika ya Mtakatifu Maria Mkuu: kuwa nyota angavu, katika huduma ya Nuru ya Kweli, inayoonesha Mwokozi, Mungu wa kweli na mtu kweli, aliyezaliwa na Bikira Maria. Kwa muda wa miaka 1600, Kanisa hili la Kipapa limependekeza kuwa kama nyota ya Bethlehemu, ambayo inaeneza tangazo la kimalaika lililoelekezwa kwa wachungaji: msiogope, bali nendeni kwa Bwana.
Neema ya Jubilei
Tunaomba neema ambayo Mwaka huu wa Jubilei utusogeze na kutusukuma kutembea kumwelekea Bwana tukiwa na wasiwasi wa kweli na wa dhati kwa wapendwa wetu, kwa maskini, kwa wagonjwa, kwa wale ambao wamepoteza njia ya ukweli, furaha na ya amani. Sote tumeitwa kwa tumaini hili sawa, bila tofauti. Sote tunaweza kutembea kwenye njia hii ya tumaini la furaha. Kila mtu! Na Maria yuko karibu na kila mtu, bila ubaguzi. Kama mama, yeye huwapenda watoto wake wote na huwatunza kila wakati. Tunakaribisha maneno ya Baba Mtakatifu Francisko aliyotuelekeza katika Tamko la kutangaza Mwaka Mtakatifu: Spes non confundit akisema kuwa: "Ninawaalika mahujaji wanaokuja Roma kusimama kwa ajili ya maombi katika Maeneo Matakatifu ya Maria ya mji huo ili kumheshimu Bikira Maria na kusali ili kupata ulinzi wake. Nina hakika kwamba kila mtu, hasa wale wanaoteseka na kufadhaika, wataweza kufanya uzoefu wa ukaribu wa upendo wa mama ambaye kamwe hatelekezi watoto wake, yeye ambaye kwa Watu watakatifu wa Mungu ni “ishara ya tumaini hakika na faraja" (SNC, 24)." Kwa kuhitimisha alisema “Leo, mwanzoni mwa Mwaka wa Jubilei, tuyakabidhi maisha yetu, wakati wetu, kwa Mama wa Mungu, ili atuongoze kwa Yesu: utimilifu wa wakati, wa kila wakati, wa wakati wa kila mmoja wetu. Amina. “