Papa amemteua Askofu Mwandamizi wa Jimbo la Meru nchini Kenya!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Alhamisi tarehe 16 Januari 2024, Baba Mtakatifu Francisko amemteua mweshimiwa Padre Jackson Murugara,(I.M.C.,) wa Shirika la Wamisionari wa Consolata, kuwa Askofu Mwandamizi wa Jimbo la Meru nchini Kenya. Hadi uteuzi huo alikuwa ni Paroko na Msimamizi wa Madhabahu ya Consolata ya Jimbo Kuu la Nairobi.
Wasifu wake
Padre Jackson Murugara, I.M.C., alizaliwa tarehe 7 Aprili 1970 huko Kamanyaki, katika Kata ya Tharaka-Nithi, Jimbo Katoliki la Meru. Baada ya kujiunga na Shirika la Wamisionari wa Consolata alihitimu mafunzo ya Falsafa katika Taasisi ya wa Consalata ya Falasa, Nairobi Kenya, na Taalimungu katika Taasisi ya Kimisionari ya London nchini Uingereza. Alifunga nadhiri za daima kunako tarehe 18 Novemba 2000 na kupewa daraja takatifu la Upadre kunako tarehe 15 Agosti 2001 katika jimbo la Meru.
Alifunika nyadhifa mbali mbali na kuendelea na mafunzo zaidi: mhudumu wa Parokia ya Kagaene na Mujwa, Jimbo la Meru (2001-2002); Paroko Msaidizi wa Parokia ya Chiga, Jimbo Kuu la Kisumu (2002-2003); Mlezi wa Wapostulanti katika Seminari ya Waconsolata huko Nairobi(2003-2009); Leseni ya Taalimungu ya Kiroho katika Taasisi ya Kiroho ya Teresianum, Roma (2011); Mkurugenzi wa Kituo cha Kichungaji cha Nyumba ya Bethania na Nyumba ya Upendo katika Jimbo Katoliki la Muranga (2011-2018). Tangu 2018 ni Paroko na Msimamizi wa Madhabahu ya Consolata, Jimbo Kuu la Nairobi.