Papa amteua Mons.Gilbert Ndyamukama kuwa Mratibu wa Kitengo cha Baraza la Kipapa la Uinjilishaji
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Jumanne tarehe 14 Januari 2025, Baba Mtakatifu Francisko amefanya teuzi mbali mbali katika ofisi za Curia Romana. Kwa njia hiyo amemtetua, Mheshimwa, Monsinyo Gilbert Ndyamukama Gosbert, kuwa Mratibu ndani ya Kitengo cha Kwanza cha Uinjilishaji na Makanisa Maalum cha Baraza la Kipapa la Uinjilishaji, na ambaye hadi uteuzi huo, alikuwa ni afisa wa Taasisi hiyo ya(Curia Romana) inayojishughuliza na shughuli za umisionari Ulimwenguni kote.
Wasifu
Monsinyo Ndyamukama alizaliwa tarehe 23 Aprili 1977 huko Bukoba Tanzania. Baada ya Masomo ya Sekondari katika Seminari Ndogo ya Katoke (Jimbo la Rulenge - Ngara) na Nyegezi, (Jimbo Kuu la Mwanza,) alijiunga na mafunzo ya Falsafa katika Seminari Kuu ya Ntugamo, (Jimbo la Bukoba Tanzania, kuanzia mwaka 2001-2004. Baadaye Monsi. Ndayemukama aliendelea na masomo ya Taalimungu katika Chuo cha Kipapa cha Msalaba, Jijini Roma kuanzia 2004-2009.
Alipewa daraja la Upadre kunako tarehe 2 Agosti 2009 kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Kayanga Tanzania. Baada ua utume mfupi wa Uchungaji katika Parokia ya Mtakatifu Paulo, Jimbo la Kayanga, alirejea Roma kwa kujikita zaidi katika masomo ya Taalimungu ya Maadili kwa ngazi ya Shahada ya Udaktari 2010 -2012 pia na stashahada ya Usimamizi wa masuala ya Kanisa.
Kunako 2013 hadi 2015, alifundisha Taalimungu ya Maadili katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Karoli Lwanga,(Segerea, Dar Es Salaam,) Tanzania. Na ni katika mwezi Septemba 2015 ambapo Monsinyo Ndyamukama alirejea tena Roma kufanya kazi katika Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu hadi uteuzi huu wa tarehe 14 Januari 2025, lakini pia amekuwa msimamizi wa Parokia ya Maria Mpalizwa huko, Borgo Pineto, Jimbo la Civita Castellana mkoa wa Lazio (2023-2024)
Uteuzi wa Monsinyo Tomasz Kubiczek
Baba Mtakatifu Jumanne tarehe 14 Januari 2025 amemteua kuwa Mkaguzi Mkuu wa Mahakama ya Rota Romana Monsinyo Tomasz Kubiczek, hadi uteuzi huo alikuwa ni Msimamizi wa Haki katika Mahakama hiyo hiyo.
Balozi wa Vatican huko Palau,katika Shirikisho la Mikronesia na huko Vanuatu
Baba Mtakatifu Francisko amemteua, Balozi wa Vatican kuwa wa Palau, katika Majimbo ya Shirikisho la Mikronesia na Vanuatu, Mhashamu Askofu Mkuu Gábor Pintér, Askofu wa Velebusdo, na ambaye hadi uteuzi huo alikuwa ni Balozi wa Vatican huko New Zealand na Visiwa vya Fiji.
Maombi ya kung'atuka na uteuzi wa msimamizi wa Visiwa vya Marshall
Papa Francisko, Jumanne tarehe 14 Januari 2025 amekubali maombi ya kung’atuka katika shughuli za Uchungaji kwa Msimamizi wa Kitume kwenye Visiwa vya Marshall, kwa maombo yaliyowakilishwa na Mheshimiwa Padre Ariel A. Galido, (Wamisionari wa Moyo Mtakatifu wa Yesu M.S.C.) Na wakati huo huo akamteua Msimamizi wa Kitume, Mheshimiwa Padre Tamati Alefosio Sefo, M.S.C., ambaye hadi uteuzi huo alikuwa ni Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Petro Chanel huko Samoa.
Wasifu
Padre Tamati Alefosio Sefo, M.S.C.,alizaliwa tarehe 28 Aprili 1972 huko Tafitoala Safata, Samoa. Baada ya mafunzo ya falsafa na taalimungu katika Seminari ya Kanda ya Pasifiki, Suva, Fiji, alipewa daraja la Upadre tarehe 27 Novemba 2004. Katika maisha yake ameshika nyadhifa mbali mbali na kuendelea pia na masomo: Paroko kwa muda mfupi wa Parokia ya Mtakatifu Andrea huko Faleula, Samoa (2005); Paroko wa Mtakatifu Agnes huko Samabula, Fiji (2006-2009); Kozi ya Mafunzo katika Kituo cha Mlima wa Maria wa Huruma (NSW,)Australia (2010); Mkufunzi na kisha Mkurugenzi wa Mafunzo katika Taasisi yao ya Kitawa
M.S.C. (2011-2014); Mwenyekiti wa Bodi ya Dhamana ya Vijana ya Chevalier (2015-2023); Mkuu wa Umoja wa Shirika la Wamisionari wa Moyo Mtakatifu wa Yesu wa Visiwa vya Pasifiki M.S.C. (2015-2021); Mkuu wa Shirika la M.S.C. katika Visiwa vya Pasifiki (2021-2023). Tangu 2023 amekuwa Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Petro Chanel huko Samoa.