Kutabarukiwa Kwa Kanisa la Ubatizo wa Bwana: Haki, Amani na Matumaini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kutabarukiwa kwa Kanisa maana yake ni kutenga Kanisa kwa ajili ya maadhimisho ya Mafumbo Matakatifu ya Kanisa, kwa ajili ya sifa, utukufu na ukuu wa Mungu. Na ni katika mantiki hii, Kanisa linaitwa Nyumba ya Mungu, Makao ya watu wa Mungu, mahali ambapo watu wa Mungu wanakutanika kusali, kuabudu, kumtukuza, kumwomba na kumshukuru Mungu kwa wema, huruma na ukarimu wake wa daima. Hapa ni mahali ambapo Mwenyezi Mungu anasubiri kukutana na waje wake, lakini inasikitisha kuona kwamba, kuna Kanisa lililojengwa vizuri na la kupendeza, lakini hakuna waamini wanaokwenda kusali ndani mwake. Hivyo basi, Liturujia inayoadhimishwa kila siku, iwajenge waamini waliomo katika Kanisa ili wawe ni Hekalu Takatifu la Bwana, Makao ya Mungu katika Roho, mpaka kuufikia utimilifu wa Kristo Yesu. Maadhimisho ya Liturujia yawaimarishe waamini kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa njia ya maisha adili na matakatifu. Rej. SC, 2. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwenda Kanisani ili kuchuma, neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kumbe, uwepo wa waamini Kanisani humo, itakuwa ni baraka na neema tosha kabisa. Ujenzi wa jengo kama Kanisa unakamilika kwa haraka, lakini inachukua muda mrefu kujenga na kuimarisha Jumuiya ya waamini, wenye tabia, ari na mielekeo tofauti. Kumbe, huu ni mwaliko kwa waamini kujenga na kudumisha Jumuiya ya waamini inayoimarishwa kwa Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unaosimikwa katika: Umoja, Ushiriki na Utume.”
Altare inaonesha: sadaka na meza ya Bwana. Mababa wa Kanisa wanasema, Altare ni alama ya Kristo mwenyewe aliye kati ya kusanyiko la waamini wake, papo hapo akiwa kafara inayotolewa kwa ajili ya upatanisho kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu. Altare ni sura ya mwili wa Kristo Yesu anasema Mtakatifu Ambrosi na kwamba, mwili wa Kristo uko juu ya Altare. Kumbe, Kanisa linafundisha kuhusu umoja kamili kati ya Sadaka na Altare. Altare hai ni Kristo Yesu mwenyewe, hivyo, wanapoiangalia Altare wamwone Kristo aliyejitoa sadaka Msalabani kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Vivyo hivyo kama mwamini ni kiungo cha Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, anapaswa kutambua kuwa yeye ni sehemu ya Altare ambacho kimsingi ni kielelezo makini cha Kristo Yesu katika hali yake yote. Ni Kristo Yesu: anayeganga na kuponya, anayesamehe na kutakasa; Kristo anayefundisha, kuonya na kuongoza. Ni katika maadhimisho ya Kutabaruku Kanisa la Ubatizo wa Bwana, lililoko nchini Yordani, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Pietro Parolin Katibu mkuu wa Vatican, kuwa ni mwakilishi wake katika Sherehe za Kutabaruku Kanisa la Ubatizo wa Bwana, Ijumaa tarehe 10 Januari 2025. Hapa ni mahali panaposadikiwa kwamba, ndipo Yohane Mbatizaji alimpombatizia Kristo Yesu. Yohane Mbatizaji katika maisha na utume wake, alitangaza na kushuhudia Ubatizo wa toba na maondoleo ya dhambi. Akawataka watu kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu na hivyo, kuanza kutembea katika mwanga wa maisha mapya, kama njia makini ya kuweza kumpokea Masiha wa Bwana, atakayetambulika kwa uwepo wa Roho Mtakatifu juu yake na huyu ndiye atakayebatiza kwa Roho Mtakatifu. Wakati ulipotimia Yesu akajitokeza hadharani kando ya Mto Yordani, baada ya kukaa nyumbani kwao mjini Nazareti kwa muda wa miaka thelathini, ili aweze kubatizwa.
Kardinali Pietro Parolin Katibu mkuu wa Vatican katika mahubiri yake alikazia kuhusu umuhimu wa mchakato wa kujenga na kudumisha matumaini yanayosimikwa katika amani ya kudumu na kwamba, uwepo wake ni kielelezo cha ukaribu wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kanisa huko Mashariki ya Kati hasa kutokana na vita, ghasia na ukosefu wa amani na utulivu. Baba Mtakatifu anawataka watu wa Mungu huko Mashariki ya Kati wawe ni mbegu ya matumaini kwa kuendelea kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Kwa hakika Mungu ndiye anayeongoza historia ya maisha ya mwanadamu, hata kama bado kuna vita, dhambi na kifo. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Wakristo kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika usawa, haki na amani na kwamba, huu ni wakati wa kusitisha vita ili watu waanze kujielekeza katika ujenzi wa nchi yao. Kanisa la Ubatizo wa Bwana, ni eneo lenye umuhimu wa pekee kabisa, kwani hapa ni kielelezo cha mateso na dhambi za binadamu; mahali ambapo mbingu na dunia zilifunguka, sasa watu wanahimizwa kuombea amani. Hii ni sehemu ya hija ya watu wa Mungu. Jiwe la msingi lilibarikiwa na Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika hija yake ya kitume Nchi Takatifu kunako mwaka 2009. Kanisa hili ni kielelezo cha uwepo endelevu na angavu wa Kristo Yesu kwa njia ya: Neno na Sakramenti zake, tayari kuchuchumia maisha na uzima wa milele. Kanisa la Ubatizo wa Bwana ni mahali muafaka kwa waamini kupyaisha tena ahadi zao za Ubatizo. Kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Kardinali Parolin anasema, huu ni mwaka wa matumaini unaokita mizizi yake katika toba, wongofu wa ndani na msamaha wa dhambi, tayari kuambata na kukumbatia upendo na huruma ya Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini kufanya hija ya matumaini katika Kanisa la Ubatizo wa Bwana.
Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee, amewashukuru viongozi wa Serikali ya Yordan. Mwezi Februari 2025 kunafanyika maonesho ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na nchi ya Yordani. Amewashukuru pia wafadhili mbalimbali waliowezesha Kanisa la Ubatizo wa Bwana kukamilika katika mwonekano wake huo. Mwaka 2025 Vatican na Serikali ya Yordani zinaadhimisha kumbukizi ya miaka 30 ya mahusiano ya kidiplomasia baina ya nchi hizi mbili, sanjari na kumbukizi ya miaka 60 tangu Mtakatifu Paulo VI alipotembelea Nchi Takatifu kunako mwaka 1964. Kwa upande wake Kardinali Pierbattista Pizzaballa wa Kanisa la Yerusalemu Madhehebu ya Kilatini, amekazia kuhusu utulivu na amani huko Mashariki, ili watu wa Mungu waweze kujielekeza katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika mahojiano maalum na Kardinali Pietro Parolin amekazia kuhusu: Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji wa Matumaini.” Wakristo huko Mashariki ya Kati wanayo dhamana na mchango muhimu sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote wa Mungu katika haki na usawa mbele ya Sheria, hali inavyopaswa kuwa hata nchini Siria, kwa kuzingatia haki msingi kwa wote. Uchaguzi mkuu wa Lebanon uliofanyika hivi karibuni ni kielelezo cha matumaini katika kukuza na kudumisha umoja na mshikamano kati ya nchi ambayo inakita mizizi yake katika tofauti msingi za kijamii, kisiasa na kidini, kwa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene. Ni wakati wa kutenda haki kwa waathirika wa mlipuko wa Bandari ya Beirut nchini Lebanon. Kwani ilikuwa ni tarehe 4 Agosti 2020 mlipuko mkubwa ulipotokea kwenye bandari ya Beirut nchini Lebanon na hivyo kusababisha watu zaidi ya 2,000 kupoteza maisha, watu 6, 500 kujeruhiwa vibaya sana pamoja na uharibifu mkubwa wa miundo mbinu. Taarifa za awali zilionesha kwamba chanzo ni kulipuka kwa “Ammonium Nitrate” Tani 2750 iliyokuwa imehifadhiwa bandarini hapo. Mkataba wa Helsinki wa Mwaka 1975, ulitiwa mkwaju na Mataifa 35 baada ya kuhitimishwa kwa mkutano uliojadili kuhusu masuala ya usalama na ushirikiano Barani Ulaya, uliofanyika mjini Helnsiki huko nchini Finland kati ya mwezi Julai na Agosti 1975. Huu ni mkutano uliolenga kuboresha mahusiano na mafungamano kati ya Ulaya ya Mashariki na Ulaya ya Magharibi kwa wakati huo.
Mkataba wa Helsinki wa Mwaka 1975 uliweka kanuni 10 ambazo zinafafanua mambo msingi katika uhusiano na ushirikiano yaani: Nchi zote zina mamlaka sawa, kuheshimu haki zilizo katika mamlaka husika; kutotumia nguvu; ukiukaji wa mipaka; uadilifu; utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani; kutokuingiliwa katika mambo ya ndani ya nchi; kuheshimu haki za binadamu pamoja na kudumisha; usawa na haki ya watu kudhibiti hatima ya maisha yao wenyewe; ushirikiano wa kimataifa; kutimiza majukumu ya kisheria ya kimataifa. Kardinali Parolin anakaza kusema, kuna haja ya kujenga jamii inayosimikwa katika haki ya kweli mintarafu Sheria za Kimataifa. Haki inayofumbata misingi ya msamaha. Mkataba wa Kihistoria wa Muda Mfupi kati ya Vatican na China Kuhusu Uteuzi wa Maaskofu Mahalia ulitiwa saini kwa mara ya kwanza tarehe 22 Septemba 2018; ukapyaishwa tena tarehe 22 Oktoba 2020, 22 Oktoba 2022 na hatimaye 22 Oktoba 2024. Mkataba umeongezwa tena kwa muda wa miaka minne yaani hadi mwaka 2028. Papa Francisko anapenda kuonesha uvumilivu unaosimikwa katika matumaini, ili kuwapatia watu wa Mungu wachungaji wema na watakatifu. Kardinali Pietro Parolin anasema, diplomasia ya Vatican imejikita katika majadiliano kwa kuanzia na yale mambo msingi yaliyokuwa mezani, yaani uteuzi wa Maaskofu mahalia, ili kuwa na umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwamba, huu ni msingi wa Kanisa Katoliki. Baba Mtakatifu Francisko anakazia diplomasia ya uvumilivu inayokiza mizizi yake katika matumaini. Hii ni safari ya neema ya Mungu itakayozaa matunda yake kwa wakati.