Kard.Semeraro,Mwenyeheri Merlini:Kuchanganya tafakari na vitendo
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Watakatifu akiwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yohane in Latareno katika fursa ya Kumtangaza kuwa Mwenyeheri, Giovanni Merlini Mmisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Dominika tarehe 12 Januari 2025 katika Kanisa Kuu hilo ambalo lilikuwa limejaa wanashirika na waamini Watu wa Mungu ambapo Kardinali Semeraro katika mahubiri yake mara baada ya masomo alisema kwamba “Leo, Kanisa linaadhimisha sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, ambamo anatangazwa kuwa Mwana wa Mungu, mpendwa, maji yanatakaswa, mwanadamu ametakaswa na viumbe vyote vinafurahi. "Ndivyo kitabu cha Kirumi kinaeleza katika Dominika hii ambayo inafunga Kipindi cha Noeli.”
Merlini ni mfano wa sala
Kardinali Semeraro akiendelea mahubiri yake alisema: Leo Bwana anajionesha kwetu si kwa matendo na maneno, kwa miujiza na mafumbo, bali kwa ishara iliyojaa ukimya ambayo hata hivyo ndiyo yenye ufasaha zaidi ya yote: sala! Kama tulivyosikia hivi punde wakati wa kusomwa Injili, watu wote walipokuwa wakibatizwa, ambapo Yesu, mara tu alipopokea ubatizo, alikuwa katika maombi(rej. Lk 3:21). Kutoka katika historia za Injili hasa kutoka katika Injili ya Luka, tunajua kwamba sala kwa Yesu ndiyo tabia ya kawaida, mahali muafaka ambapo anaishi fumbo la nafsi yake na utume wake, nafasi muhimu ambayo anaweka mahusiano yake na Baba na wanafunzi. Yesu alimwomba Baba yake daima; na hatimaye huko Gethsemane na msalabani. Aliwaombea wanafunzi wake alipowachagua na alipowafundisha kusali... Haya yote yanatuambia kwamba Yesu ni mwalimu wa maombi; Hakika, kama tunavyosoma katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki, yeye, anaposali ... tayari anatufundisha kusali" (n. 2607).
Katika hilo, Kardinali Semeraro alisema “leo tunatambua kwa furaha, Mwenyeheri Giovanni Merlini kuwa alikuwa mfuasi wake bora. Shuhuda zilizokusanywa katika Mchakato wa kutangazwa kuwa mwenyeheri na kuwa mtakatifu zinakubaliana kwa pamoja kwa kutuambia kwamba Bwana alikuwa amemtajirisha kwa karama ya maombi: sala ambayo ndani yake ilikuwa ni tafakari. Kuhusu Merlini, Mkuu wa Baraza la Kuwatangaza Watakatifu aliendelea kusema kuwa Shahidi mmoja alisema: “Nilibisha hodi nikiomba ruhusa ya kuingia hata hakunijibu. Nilipoingia chumbani, nikamsogelea alipokuwa akisali masifu na kumkuta akiwa amechangamka, bila yeye kuona chochote, hivyo nikalazimika kutoka nje ya chumba kile kwa kunyata bila ya kuongea naye. Niliona kuwa uso wake ulikuwa kama unatabasamu, na mzuri kwa njia isiyo ya kawaida"(Summ. §129, p. 45). Kardinali Semeraro aliongeza kusema anavyofikiri kuhusu Mwenyeheri kuwa itawezekana kurudia kwa njia fulani kile ambacho Thomasi wa Celano aliandika kuhusu Mtakatifu Francis, wa Assisi yaani, kwamba alikuwa mwanadamu aliyefanya maombi(Maisha 61, 95: FF 682).
Matendo na utume
“Hata hivyo, alikuwa pia mtu wa vitendo na utume, hasa katika mahubiri ya kimisionari(ambayo kwa ajili yake aliheshimiwa sana na Mtakatifu Gaspari), na pia alikuwa mtu mwenye ujuzi bora wa kutawala na zaidi ya yote, aliyetajirishwa na wema wa busara. Kiukweli, hii ndiyo fadhila kuu ambayo ni muhimu zaidi kwa wale ambao wana majukumu ya uongozi: kipengele hiki, ambacho Mtakatifu Thomas wa Akwino alisisitiza hasa kwa sababu alisema kuwa ‘mwenye busara ni yule ambaye anajua jinsi ya kuamua nini cha kufanya kwa uthabiti na anajua jinsi gani kufanya hivyo kwa hekima.’ Kwa hiyo Mashahidi wa mchakato wa kutangazwa mwenyeheri wanabainisha kwamba Mwenyeheri Giovanni Merlini alitumia wema wa busara kwa njia isiyo ya kawaida: alisoma hali, alishauriana na kuingilia kati kwa njia zinazofaa na hii, hasa katika maamuzi magumu kwa watu, kwa upendo (Summ. §492-495, pp. 191-192). Miongoni mwa shuhuda nilizosoma kwa mshangao huu Kardinali aliongeza: "Mtumishi wa Mungu aliunganisha pamoja maisha kama yale ya Martha na Magdalene, kwa namna ambayo ilionekana kuwa shujaa katika wote wawili" (§924, p. 370). Wakati huo huo (tuko katika muktadha wa kawaida uliyofanyika huko Albano kati ya 1880 na 1905) kama vile ilikuwa ni desturi kumfananisha Maria, dada yake Martha na Lazaro, na Maria Magdalene; Lakini mshangao wangu hautoki hapa; badala yake, ni katika utambuzi wa uhusiano kati ya aina mbili za maisha ya kiutamaduni: moja ya "kutafakari" na nyingine ya "kutenda.”
Hekima ya moyo:kuchanganya tafakari na vitendo
Kardinali Semeraro alisisitiza kuwa bado kuna wale ambao leo hii wanazitaja kuwa ni aina mbadala za maisha, na ambazo kwa hakika zinakamilishana, zenye matokeo. Julian Pomerius - mwalimu wa kiroho wa karne ya 5, aliandika kwamba "katika maisha ya kazi ya mtu huendelea na katika maisha ya kutafakari na hufikia kina chake" ( The Contemplative Life XII, 1). Kwa hiyo Papa Francisko leo hii anafundisha kwamba “hekima ya moyo ipo katika kujua jinsi ya kuchanganya vipengele hivi viwili: kutafakari na kutenda. Martha na Maria wanatuonesha njia. “Ikiwa tunataka kufurahia maisha kwa furaha, ni lazima tuunganishe mitazamo hii miwili: kwa upande mmoja, “tukikaa miguuni” pa Yesu, ili kumsikiliza anapotufunulia mafumbo ya kila kitu; kwa upande mwingine, kuwa makini na tayari katika ukarimu, anapopita na kubisha hodi kwenye mlango wetu, tukiwa na uso wa rafiki anayehitaji muda wa kuburudishwa na udugu,” (rej. Tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana tarehe 21 Julai 2019). Mwenyeheri Merlini pia alitekeleza "ukarimu" huo. "Katika kila hitaji na ulazima - alisema shahidi mmoja kuwa- ilitosha kumgeukia kuwa na uhakika wa utunzaji wake wote na nia ya kuwasaidia kana kwamba ni jambo lake mwenyewe, na hata bora zaidi" (Summ §583, p. 228).
Kuishi vema katika familia ya kitawa
Kardinali Semeraro vile vile alisema kuwa haya yote ni baadhi ya vipengele vya maisha na hali ya kiroho ya Mwenyeheri mpya ambaye Kanisa linatupendekeza kuanzia leo kwa ajili ya maombi na kuiga mfano wake. Hata hivyo, “lipo jambo jingine ambalo sitaki kukosa kulikumbuka, nalo ni urafiki alioishi hasa na ndugu zake katika familia ya kitawa na watu waliokabidhiwa kwake kwa ajili ya mwongozo wa kiroho,” alikumbuka Kardinali Semeraro. “Majina ya Mtakatifu Gaspar del Bufalo na Mtakatifu Maria de Mattias ni ishara kwa dhamana yao maalum na Mwenyeheri Giovanni Merlini”. Kuna msemo wa enzi za kati unaosema hivi: Ubi est charitas et dilectio, ibi est sanctorum congregatio, yaani “Mahali palipo na upendo na furaha, kuna kusanyiko takatifu.” Kwa hiyo inajitokeza hara kwake kumfikiria kwamba: “ikiwa ni kweli kuwa watakatifu hufanya urafiki na kila mmoja, lazima iwe kweli kwamba kuna urafiki (umoja uliounganishwa na upendo) ambao hufanya watakatifu,” alibainisha Mkuu wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Watakatifu.
Tunahitaji kuwa na tumaini ili kutoa ushuhuda wa kuaminika na kuvutia kwa imani na upendo
Kwa kuhitimisha Kardinali Semeraro alisema kuwa “Bwana atujalie, labda kwa wakati ufaao kwa huu "mwaka Mtakatifu,” ambao Papa pia alituandikia kwamba: "tunahitaji 'kuzidi kuwa na tumaini' ili kutoa ushuhuda wa kuaminika na wa kuvutia kwa imani na upendo ambao tunabeba mioyoni mwetu; ili imani iwe na furaha, upendo wenye shauku; ili kila mtu aweze kutoa hata tabasamu tu, ishara ya urafiki, sura ya kidugu, kusikiliza kwa dhati, huduma ya bure, tukijua kwamba, katika Roho ya Yesu, hii inaweza kuwa mbegu yenye kuzaa matunda kwa wale wanaoipokea"(rej. Spes non confundit, n. 18). Alihitimisha mahubiri yake.