Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo Ni Chemchemi ya Matumaini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 9 Januari 2025 amekutana na kuzungumza na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika mbalimbali ya Kimataifa yenye uhusiano wa kidiplomasia na Vatican. Balozi Georgios F. Poulides kutoka Cyprus, Dekano wa Mabalozi kwa niaba ya Mabalozi wenzake pamoja na wawakilishi wa Mashirika mbalimbali ya Kimataifa mjini Vatican, amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuzindua maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu: “Mahujaji wa Matumaini.” Huu ni ujumbe wa mabadiliko unaopania kuwaletea binadamu imani na ujenzi wa udugu wa kibinadamu, ulioonekana kana kwamba, umeanza kutoweka kutokana na madhara ya vita, athari za mabadiliko ya tabianchi, upweke hasi unaomwandama mwanadamu na kwamba, binadamu wote wanayo kiu ya matumaini yanayosimikwa katika amani inayopata chimbuko lake katika majadiliano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu.
Huu ni mwaka ambao waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanaitwa na kuhamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini na kwamba, kimsingi binadamu wote ni mahujaji wa matumaini. Haya ni matumaini ambayo wanapaswa kushirikishwa wagonjwa na maskini; wafungwa, wakimbizi na wahamiaji; wazee kwa vijana, ili watu waweze kufarijiana na kuendelea kujenga familia kubwa ya binadamu. Kristo Yesu ni mlango unawaohamasisha waamini kujikita katika upendo kwa Mungu na jirani kwa kuambata Injili ya furaha, daima wakimwangalia Kristo Yesu waliyemtoboa kwa mkuki ubavuni, kimbilio la wakosefu na wadhambi; watu wanaohitaji msamaha, amani na utulivu wa ndani. Kristo Yesu ni mlango wa huruma na faraja, wema na uzuri usiokuwa na kifani. Huu ndio mlango wanamopita watu wenye haki. Kristo Yesu ni mlango wa mbingu, unaowaalika wote kushiriki furaha ya uzima wa milele.
Ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika haki, amani na maendeleo endelevu unahitaji subira na uvumilivu ili hatimaye, kutoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji, tayari kutembea kwa pamoja katika umoja, ili kujenga na kudumisha haki, amani na maridhiano. Diplomasia ya kweli haina budi kuwa na ujasiri wa kujikita katika kipaji cha ubunifu ili kuimarisha umoja katika tofauti, tayari kushirikiana katika matumizi bora ya rasilimali za dunia, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ili kujenga na kudumisha jamii inayosimikwa katika haki, uhuru, ukweli na uwazi, kuna haja kwa nchi tajiri zaidi duniani kuzifutia deni kubwa linalozielemea nchi changa zaidi na kwamba, hii ni kanuni ya haki na maadili. Baba Mtakatifu anasema, hili ni deni ka kiikolojia ambalo linapaswa kulipwa na nchi tajiri zaidi duniani. Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ni fursa kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumfungulia malango ya nyoyo zao Kristo Yesu ili apate kuingia. Mwishoni, Balozi Bwana Georgios F. Poulides Dekano wa Mabalozi kwa niaba ya Mabalozi wenzake pamoja na wawakilishi wa Mashirika mbalimbali ya Kimataifa mjini Vatican, amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kuwa ni chemchemi ya matumaini kwa watu wengi wa Mungu. Wanamtakia heri, baraka na afya njema katika kipindi cha Mwaka 2025.