杏MAP导航

Tafuta

Mwenyeheri Giovanni Merlini, wanakuwa wa kwanza kutangazwa katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Miaka 152 tangu alipofariki dunia. Mwenyeheri Giovanni Merlini, wanakuwa wa kwanza kutangazwa katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Miaka 152 tangu alipofariki dunia. 

Giovanni Merlini Mwenyeheri Wa Kwanza Katika Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo

Mwenyeheri Giovanni Merlini, anakuwa wa kwanza kutangazwa katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Dominika tarehe 12 Januari 2025. Huyu ni mmisionari hodari na mwaminifu kwa ibada ya Damu Takatifu ya Yesu. Ni mhubiri mahiri. Ni Mwenyeri wa matumaini, aliyekita maisha yake katika sala kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Ni Mwenyeheri aliyekuwa na uwezo wa kugeuza hofu na wasi wasi kuwa ni chemchemi ya matumaini.

Na Padre Chesco Peter Msaga, C.PP.S na Padre Innocent Miku, C.PP.S. – Roma.

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” (Mt. 5:12) anakazia kuhusu mwaliko wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo. Kristo Yesu anawaalika wote wanaoteseka au kudhulumiwa kwa ajili yake, kufurahi na kushangilia, kwani yeye ni chemchemi ya maisha na furaha ya kweli. Kristo Yesu anataka waja wake kuwa kweli ni watakatifu, mwaliko na changamoto inayojionesha katika sehemu mbalimbali za Maandiko Matakatifu. Baba Mtakatifu anasema, lengo la wosia huu ni mwaliko wa kuwa watakatifu kila mtu kadiri ya hali na wito wake; kwa kutambua vizingiti, changamoto na fursa ambazo zinaweza kutumiwa na waamini kufikia utakatifu wa maisha. Kristo Yesu anawaalika waja wake ili wawe watakatifu, watu wasiokuwa na hatia mbele zake katika upendo. (Rej. Ef. 1:4). Utakatifu ni hija ya mapambano dhidi ya dhambi kwa kuendelea kupyaisha ile neema ya utakaso ambayo waamini wameipokea katika Sakramenti ya Ubatizo! Utakatifu unawawezesha waamini kuguswa na mahangaiko ya jirani zao, kwa kutambua na kuthamini: haki msingi, utu na heshima yao kama watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Waamini wanaitwa kuwa watakatifu kwa sababu Mwenyezi Mungu ni Mtakatifu na ni kiini na utimilifu wa utakatifu wenyewe. Utakatifu ni changamoto inayopaswa kupaliliwa kila kukicha na kamwe haitoshi kuwa Mkristo na mwamini kuanza kubweteka, bali daima ajitahidi kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika: haki, amani, upendo na mshikamano unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanapozungumzia kuhusu Fumbo la Kanisa wanakazia umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa. Wanasema, waamini kwa kuimarika na misaada mingi ya wokovu namna hii na ya ajabu, waamini wote wa kila hali na hadhi wanaitwa na Kristo Yesu kila mmoja kwa njia yake, kwenye ukamilifu wa utakatifu kama Mwenyezi Mungu alivyo mtakatifu!

Mwenyeheri Giovanni Merlini, shuhuda wa matumaini
Mwenyeheri Giovanni Merlini, shuhuda wa matumaini

Baba Mtakatifu Francisko anakazia pamoja na mambo mengine: Mapambano ya maisha ya kiroho, kukesha na kusali pamoja na kufanya mang’amuzi ya maisha. Kanisa ni Sakramenti ya wokovu inayowajalia waamini kusikiliza Neno la Mungu, kushiriki Sakramenti za Kanisa; kusimika maisha yao katika kanuni maadili na utu wema pamoja na kuonja shuhuda za watakatifu mbalimbali. Changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo ni utakatifu wa Jumuiya ya waamini, dhamana na utume ambao unapaswa kutekelezwa kwa ari na moyo mkuu: kwa kukubali mahusiano na mafungamano mapya yanayoletwa na Kristo Yesu; kwa kuondokana na woga usiokuwa na mvuto wala mashiko; kwa kujenga utamaduni wa kukutana na kushirikiana na wengine; kwa kumwilisha imani katika matendo; kwa kuwa ni vyombo vya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Waamini wajitahidi kuwa wamisionari katika hali na mazingira yao! Wajifunze kuteseka na kufurahi pamoja na jirani zao ili kujenga umoja, udugu na mshikamano wa dhati! Wakristo wanaitwa na kutumwa kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa ulimwengu kwa kuishi kiaminifu kweli za Kiinjili! Mambo yote haya ni kielelezo cha mapambano ya maisha ya kiroho, yanayohitaji kufanyiwa mang’amuzi ya kina, ili kusonga mbele katika hija ya utakatifu wa maisha! Ni mwaliko wa kukumbatia neema ya Mungu, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwakoa waja wake kutoka katika vishawishi na mitego ya Shetani na Ibilisi. Waamini wawe wepesi kusoma alama za nyakati, kuchunguza dhamiri zao mbele ya Mwenyezi Mungu na kukimbilia huruma na upendo wake, pale wanapoelemewa na dhambi pamoja na udhaifu wa moyo!

Mwenyeheri Giovanni Merlini alikuwa ni mahubiri mahiri wa Neno la Mungu
Mwenyeheri Giovanni Merlini alikuwa ni mahubiri mahiri wa Neno la Mungu

Ni shangwe, nderemo na vifijo vya sifa na utukufu kwa Mungu katika Shirika la Wamisionari wa Damu Takatifu ya Yesu, C.PP.S., Masista Waabuduo Damu Takatifu ya Yesu, ASC na waamini wote, kwa tukio la kihistoria na la kiimani kupata Mwenyeheri Giovanni Merlini, wa kwanza katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Dominika tarehe 12 Januari 2025. Huyu ni mmisionari hodari na mwaminifu kwa Ibada ya Damu Takatifu ya Yesu. Ni Mwenyeheri wa matumaini, aliyekita maisha yake katika sala kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Ni Mwenyeheri aliyekuwa na uwezo wa kugeuza hofu na wasi wasi kuwa ni chemchemi ya matumaini. Karama ya Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu ni kuinjilisha. Kunako Mwaka 1820 Mwenyeheri Giovanni Merlini alikutana kwa mara ya kwanza na Mtakatifu Gaspari dek Bufalo, Muasisi wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, akawa kwake ni kiongozi wa maisha ya kiroho na alipojiunga na Shirika, akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Ni kiongozi aliyekuwa na kipaji cha uvumilivu na alipenda kufanya mambo yake kwa uhakika, mfano bora wa kuigwa na vijana wa kizazi kipya. Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu wanaendeleza ile ndoto ya Mtakatifu Gaspari kwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Upendo, Msamaha, Haki, Amani, Huruma ya Mungu na Matumaini kwa watu waliopondeka na kuvunjika moyo. Alikuwa ni kiongozi mahiri wa maisha ya kiroho kwa watu wengi, lakini zaidi kwa Mtakatifu Maria De Mattias, Muasisi wa Shirika la Masista Waabuduo Damu Takatifu ya Yesu.

Kuna hatua tatu za kupitia hadi kufikia kutangazwa kuwa Mtakatifu
Kuna hatua tatu za kupitia hadi kufikia kutangazwa kuwa Mtakatifu   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Safari ya kutangazwa mtakatifu ina hatua kuu tatu. Hatua ya kwanza ni Mtumishi wa Mungu, hatua ya pili ni Mwenyeheri na ya tatu ni Mtakatifu. Hili tendo la imani, la sala na maombezi linalobadilisha historia ya matamanio ya mwanadamu yanapokutana na mapenzi ya Mungu. Mwenyeheri Giovanni Merlini alizaliwa tarehe 28.08.1795 huko Spoleto-Perugia, Italia. Mtoto wa tatu kuzaliwa kati ya watoto 13, katika familia ya Baba Luigi Merlini na Mama Antonia Claudi. Baada ya masomo, malezi na majiundo ya kikasisi alipewa Daraja Takatifu ya Upadre, tarehe 19.12.1818, jimboni kwake Spoleto. Giovanni Merlini akiwa na hari ya kumtumikia Mungu kwa bidii alijiimarisha kwa mazoezi ya kiroho. Kama Padri kijana alishiriki mafungo ya kiroho katika Abasia ya Mtakatifu Felix huko Giano Umbria, ambayo yalikuwa yanatolewa na Mtakatifu Gaspari del Bufalo, ambaye alianzisha Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu tarehe 15.08.1815. Umashuhuri wa Gaspari kuhubiri na kufundisha katika mafungo hayo ulimvutia sana Merlini na kuona kuwa karama yake ipo katika Shirika aliloanzisha Mtakatifu Gaspari na alitamani sana kujiunga naye. Tarehe, 15.08.1820 alijiunga rasmi na daima katika Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, akimwangalia Gaspari kama baba na mfano wake katika utume. Merlini alikuwa mchapa kazi, msikivu, mshauri mzuri na wengi walikimbilia kwake kwa maongozi hasa ya kiroho. Moja ya matunda yake ni Mtakatifu Maria De Matias, mwanzilishi wa Shirika la Masista Waabuduo Damu Takatifu ya Yesu, ASC; ambaye alimwongoza kama Baba wa maisha ya kiroho, kwa miaka 42. Katika barua zake anamwambia Maria De Matias usichukue wakandidati wepesi yaani ambao hawajakomaa kiroho, alisistiza kuwa inaweza kuwa mimea mizuri lakini siyo katika ardhi hii (Barua namba 231). Hakuwa na mchezo katika maisha ya Kiroho na Utume.

Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu wanafanya utume wao sehemu mbalimbali
Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu wanafanya utume wao sehemu mbalimbali

Tarehe 28.12.1847, Giovanni Merlini alichaguliwa kuwa mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Takatifu ya Yesu, akiwa ni wa tatu baada ya watangulizi wake Mtakatifu Gaspari del Bufalo na Biagio Valentini. Merlini aliliongoza shirika vizuri akitumia karama na vipaji vyake kwa uwezo mkubwa, mpaka kifo chake. Kwa miaka 25 yote alikuwa kiongozi imara. Alisema “Shirika linahitaji wamisionari, wafanyakazi, wasomi, watakatifu na mitume.” Hakika kwa Merlini kuna mengi ya kujifunza ni nyota ya matumaini inayong’aa kwa waamini wa milenia ya tatu ya Ukristo. Merlini alikuwa mstari wa mbele katika tasahufi ya damu, huduma ya upatanisho na kuhubiri hata katika mazingira hatarishi ya majangili, aliwahubiria bila woga akifuata mfano wa mtangulizi wake Mtakatifu Gaspari ambaye alijulikana kama “nyundo ya majangili na tetemeko la maisha ya kiroho” kwa mahubiri yake. Merlini kwa busara kubwa anasema “lazima niamke katika umimi ili niwafikirie wengine” ulimwengu wa ubinafsi ni vigumu kufikiria sisi, inahitaji sadaka kubwa. Katika mtazamo huo wa kufikiria wengine alifungua nyumba nje ya Italia, akiendeleza ndoto ya Mtakatifu Gaspari ya kutamani kuongea lugha elfu, yaani kueneza upendo wa Damu Azizi ya Yesu kwa watu wengi.Pia  Merlini aliweza kumshauri Papa Pius IX kuruhusu Sherehe ya Damu Takatifu ya Yesu kusherekewa na Kanisa zima ambapo mwaka 1849 Papa Pius IX aliweka Sherehe ya Damu Takatifu kwa Kanisa lote, na kusherehekewa kila mwaka tarehe Mosi, Julai na sasa mwezi wote wa Julai umetengwa na Mama Kanisa kwa heshima ya Damu Azizi ya kristo Yesu. Kwa hakika Damu ya Yesu ina nguvu kubwa. Giovanni Merlini alifariki tarehe 12.01.1873 akiendelea na matibabu ya majeraha ya ajali aliyopata huko Roma. Alimsamehe aliyemsababishia ajali, na alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 78.

Karama ya Shirika ni Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu
Karama ya Shirika ni Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu

Giovanni Merlini anatangazwa Mwenyeheri tarehe 12.01.2025 katika Kanisa Mama la Makanisa yote duniani, Kanisa kuu Mtakatifu Yohani, Lateran (Ecclesiarum Mater et Caput). Baada ya muujiza wa uponyaji wa Bwana Ciriaco Cefalo ambae alikuwa katika hatari ya kufa baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa damu ambapo aliongezewa mara kwa mara bila mafanikio ikawa inaisha tu. Kwa maombezi ya Giovanni Merlini ambapo waliweka masalia yake (ex indumentis) chini ya kichwa cha mgonjwa kitandani hospitalini huko Napoli. Mara ghafla mgonjwa alipata nguvu na damu kurudi kwa mujiza usioelezeka kisayansi Bwana Ciriaco Cefalo alipona na kuruhusiwa kurudi nyumbani. Mke wake anatoa ushuhuda akisema: “Mme wangu alikuwa anapoteza damu, na hawa ni wamisionari wa Damu, amepona…”  Baada ya uchunguzi wa wataalamu na tume kudhibitisha uponyaji huo kwa muujiza wa maombezi ya Merlini, anapanda hatua na kutangazwa Mwenyeheri. Sisi sote tunaitwa kuwa watakatifu na ni mahujaji wa matumaini. Watu hawa wema wanaong’aa utakatifu, Mungu anatuwekea mbele yetu, wanatufunulia ukaribu wa Mungu kati yetu kwa kuona makuu yake katika mambo madogo ya kila siku. Kwa maneno ya Mtakatifu Gaspari tufanye mambo mengi, vizuri na haraka. Padre Emmanuel Luppi, Mkuu wa Shirika la Wasionari wa Damu Azizi ya Yesu anasema, “Tukio hili ni chemchemi ya furaha na matumaini, kwani tukio la Giovanni Merlini kutangazwa kuwa ni Mwenyeheri, linawarejesha Wamisionari hawa kwenye kumbu kumbu ya miaka 152 tangu alipofariki dunia. Mwenyeri Giovanni Merlini anafahamika na watu wengi Jimbo kuu la Dodoma ambako kuna Nyumba ya Malezi ya Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu iliyoko Miyuji, Dodoma; Shule ya Sekondari Dodoma pamoja na Parokia ya Mwenyeheri Giovanni Merlini iliyozinduliwa tarehe 25 Desemba 2024 na Askofu mkuu Beatus Kinyaiya, OFM Cap. Huu ni mwendelezo wa mwaliko uliotolewa kunako mwaka 1966 na Hayati Askofu Jeremia Pesce, CP kwa Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu kwenda Tanzania kushiriki mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Leo hii, Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu wanafanya utume wao Jimbo Katoliki Singida, Mbulu, Ifakara, Rulenge-Ngara, Shinyanga, Mpanda, Morogoro, Jimbo kuu la Dodoma pamoja na Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Mwenyeheri Giovanni Merlini
11 Januari 2025, 16:06