Balozi Cavalli:Medjugorje ni mahali pa neema iliyochaguliwa na Bwana ili kukutana
Andrea Tornielli
"Medjugorje ni mahali pa kawaida, bila kitu chochote maalum na kwa neema pamekuwa mahali pa kiroho ambapo watu hutoka ulimwenguni kote. Wanakuja, na hapo wanaanza kusali.” Hayo yalisemwa katika mahojiano na vyombo vya habari vya Vatican na Askofu mkuu Aldo Cavalli, mwenye umri wa miaka 78, kutoka Lecco nchini Italia na ambaye ametumia maisha yake, katika huduma ya Vatican akiwa katika Balozi za kitume na ambaye mnamo Novemba 2021 alitumwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Mjumbe wa kitume katika nchi ndogo ya Bosnia na Herzegovina ambayo imekuwa moja ya vituo vya Maria vilivyotembelewa zaidi ulimwenguni kwa miaka arobaini iliyopita.
Mwaka 2024 ulikuwa mwaka muhimu kwa Medjugorje: Mei iliyopita Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa ilichapisha kanuni mpya juu ya matukio yanayodaiwa kuwa ya kimbinguni ambayo yanawezesha nuru ya kijani kwa ibada bila Baraza la Vatican kutangaza rasimi hali isiyo ya kawaida. Na mnamo Septemba mwaka huo barua yenye kichwa: "Malkia wa Amani" ilichapishwa iliyoweka uzoefu wa kiroho wa Medjugorje, ambayo ilikuwa inatoa ruhusa kwa kuwa na utambuzi wa juu zaidi kati ya yale yaliyotarajiwa na kanuni mpya. Tangu wakati huo, "ujumbe unaodaiwa" kupokelewa na waonaji huchapishwa "kwa idhini ya kikanisa."
Umekuwa ukiishi katika Parokia ya Medjugorje kwa miaka kadhaa sasa na na unakutana na mahujaji. Uzoefu wako ulikuwaje?
Sikuwahi kwenda Medjugorje. Lakini mimi ni Mwitaliano, na kama watu wengi kutoka nchi yangu nilikuwa na mawasiliano na wale ambao walikuwa wamekwenda huko. Siku zote niliona, kwamba waliporudi kutoka Medjugorje, watu hawa walikuwa wamejitolea zaidi katika ngazi ya kiroho na ya kibinadamu: kanisani, katika katekisimu, katika kutenda mema. Walikuwa na shughuli nyingi zaidi kuliko hapo awali. Kwa sasa nimekuwa huko kwa miaka mitatu: ni mahali pa kawaida, bila kitu chochote maalum na kwa neema pamekuwa mahali pa kiroho ambapo watu hutoka ulimwenguni kote. Wanakuja na kuanza kusali hapo. Wanaingia katika ushirika na Bwana Yesu na Bikira Maria anasindikizana nao. Ni maombi rahisi: wanataka kubadilisha maisha yao, kuishi vizuri zaidi kuliko hapo awali, wanataka kutatua au kushughulikia vizuri shida walizo nazo. Mabadiliko yanayoitwa uwongofu, ambao hufanyika hasa katika sakramenti ya kitubio. Hii hufanyika kawaida huko Medjugorje.
Ni kitu gani kinakushangaza unapowatazama mahujaji wengi?
Vijana na wazee wanafika. Wanakuja bila udhamini wowote. Wote wanakuja kwa kusudi moja: kukutana na Bwana na Bikira Maria. Hawapati chochote cha kuona au kutembelea: kuhusu utalii wa kidini, pale ni sifuri. Lakini hapa vijana na watu wazima wanaanza kusali. Nilikuwa nimewasili tu, mnamo Februari miaka mitatu iliyopita, na nilijikuta nikiwa miongoni mwa mabenchi ya nje nyuma ya Kanisa. Familia ya Amerika Kusini ilikuja, na mvulana wa miaka kumi na tano ambaye alikuwa muasi, yaani muasi wa kweli! Baada ya dakika tano tu akaja kutubu... na wazazi wake wakamtazama kwa mshangao. Ni mahali pa neema ambayo Bwana amechagua kukutana nao. Kibali cha Papa kinamaanisha: kwenda, nenda, nenda! Nenda huko kwa sababu ni mahali pa neema, ambapo unakutana na Bwana na Bwana anakutana nawe.
Shukrani kwa sheria mpya zilizopendwa na Papa Francisko, utaratibu wa kuchunguza na kutoa uamuzi juu ya kesi hizi sasa zinalenga zaidi matunda ya kiroho.
Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa imechunguza mambo mawili ambayo yanaweza kuandikwa. La kwanza linahusu matokeo. Maelfu na maelfu ya watu wanafika Medjugorje kutoka ulimwenguni kote. Mwaka 2024 watu milioni mbili, watu wazima na vijana, walikuja. Karibu makuhani 50,000 walikuja kusali, kuongoka. Kisha matunda mengine muhimu sana ni miito mingi. Watu wengi wanaomba. Kipengele cha pili kilichochunguzwa kilikuwa ni ujumbe. Kila ujumbe ulilinganishwa na imani yetu na ikabainika kuwa jumbe hizo zinalingana nayo. Matunda chanya sana, na ujumbe chanya kwa imani: hii imeturuhusu kusema kwamba Medjugorje ni mahali pa neema.
Wewe binafsi unahusika katika kuchapisha jumbe ambazo hutolewa mara moja kwa mwezi. Nini hasa hutokea?
Ni rahisi sana: kunapokuwa na ujumbe, mtu aliyeupokea huandika na kunitumia kwa lugha anayoandika, ambayo ni Kikroeshia. Wananitafsiria kwa Kiitaliano mara moja. Mchakato huu ni wa kufurahisha sana: kuna angalau upatanisho wa aina mbili muhimu sana wa wanadamu: ndiyo sababu tunazungumza kila wakati juu ya "ujumbe wa madai" hata kama ikiwa tunapendelea hadi mwisho wa ujumbe tunaandika: "kwa idhini ya kikanisa”. Lakini kuna umakini, ujumbe hufafanuliwa kama "kudhaniwa" kwa sababu hupitia njia mbili za upatanisho wa wanadamu: Maria haandiki, mtu anayepokea anaandika. Upatanisho wa pili ni tafsiri kutoka Kikroeshia hadi Kiitaliano: ni lugha mbili tofauti kabisa. Tunasema kwamba ujumbe ni mzuri, kwamba unaendana na imani na tunaalika usomwe na kuutafakari kwa sababu ni chanya. Hauongezwi chochote katika Ufunuo wake bali unautajirisha. Husaidia kuishi imani yetu vizuri zaidi leo.
Tunajua kwamba hakuna ufunuo wa kibinafsi, kwa hivyo hakuna hata moja ya maonesho ya Maria, yanayoongeza chochote kwenye Ufunuo. Je tunapaswa kuwa na mtazamo gani na ni hatari gani tunapaswa kuepuka? Kwa sababu wakati mwingine kuna hatari ya kuchukuliwa na ziada ya udadisi kuelekea "siri", udadisi fulani wa apocalyptic (Ufunuo).
Mnamo mwezi Mei, Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa ilichapisha kanuni kadhaa ambazo ni za msingi kwa kuelewa uamuzi juu ya Medjugorje. Lilikumbusha kwamba kwanza kabisa Ufunuo, Neno la Mungu, ni Biblia tu na kwamba Ufunuo huo uliisha na Ufunuo. Hii haimaanishi kwamba Roho Mtakatifu hawezi kutumia jumbe na mafunuo ya faragha yaliyokabidhiwa kwa watu na ambayo yanatumika kutekeleza vyema Ufunuo pekee wa kweli. Haya yote hayaongezi chochote kwenye Ufunuo, lakini inawezekana kuwa na manufaa. Huu ndio umuhimu wa ujumbe. Unaweza kuwa na manufaa kutekeleza leo hii Ufunuo ambao Bwana aliufanya mara moja na milele.
Je uliwahi kukutana walitokewa huko Medjugorje?
Ndiyo, na ninaweza kusema kwamba wao ni watu rahisi, wana familia zao, wana matatizo ambayo kila familia inakabiliwa nayo.
Samahani kwa kukatiza: mtu fulani alikuwa ametoa pingamizi kwa sababu hakuna hata mmoja wao ambaye amekuwa padre au mtawa...
Lakini kila mtu ana wito wake! Ni watu rahisi, watu wazuri. Sina la kusema. Tunaonana mara nyingi, tuna kunywa kahawa pamoja. Ni watu wanaokua katika imani, kila mmoja kwa njia yake mwenyewe, na kuwa na hekima zaidi. Ninawasiliana nao: hawajawa mapadre au watawa na kila mmoja ana utume wake, na maisha yake ya familia.
Umejifunza nini katika miaka hii mitatu uliyokaa katika Parokia ya Medjugorje?
Kwamba kuna neema hapo. Nilijifunza kwamba Bwana, kwa neema yake, hutufuata daima. Nilijifunza kwamba Bwana ana mpango katika maisha yetu na hutusindikiza. Anatupenda.
Huko Medjugorje, Mama Yetu alijielezea kama "Malkia wa Amani". Ujumbe ambao ni muhimu zaidi kuliko hapo awali katika wakati wetu.
Moja ya ujumbe wa kwanza unaodaiwa, kutoka 1981, ni wa kina sana katika suala hili. Anasema: amani, amani, amani, amani itawale. Jihadharini: si kati yetu, bali kati ya Mungu na sisi, na kisha kati yetu wenyewe. Hii ni muhimu. Wayahudi walipotoka Misri, Mungu alisema kupitia nabii Musa: ukitaka kuishi huru, kuna kanuni za kufuata, ni Amri. Mungu ni muhimu kwa amani. Katika amri tunaambiwa mambo machache ya kuishi kwa kuheshimu maisha na usiue, familia ni rejea ya msingi, tuheshimiane. Tukiishi hivi tunaishi kwa amani. Ikiwa hatuishi hivyo, kuna vita.
Kipengele kingine kinachofanya ujumbe wa Medjugorje kuwa wa wakati unaofaa ni ukweli kwamba uzushi unaodaiwa ulifanyika katika nchi ambayo huishi dini tofauti pamoja na ambayo imekuwa alama katika siku za hivi karibuni na vurugu isiyelezeka. Kuna ujumbe unaogusa mada hii. Unaweza kusema nini kuhusu hili?
Neno tunalotumia ni mazungumzo. Dia logos, mazungumzo kati yetu, lakini logos yaani neno inamaanisha: Ninawasilisha kwako utambulisho wangu, ninawasilisha kwako njia yangu ya kuishi, ya kufikiria, ya kuamini, ya kufanya. Unanitambulisha kwa utambulisho wako. Kwa kuzungumza tunafahamiana, kila mmoja akidumisha utambulisho wake. Tukipoteza utambulisho wetu, hatuna tena mazungumzo. Na kisha janga linakuja. Kuna dini tofauti huko, njia tofauti za maisha. Tunahitaji kuzungumza. Na sisi huko Medjugorje tuna utambulisho wazi: Bwana Yesu Kristo ndiye Bwana wa pekee kwetu.
Kanuni mpya zilizochapishwa mnamo Mei 2024 na Baraza la Kipapa la mafundisho Tanzu ya Kanisa ni kielelezo cha moyo wa uchungaji wa Papa Francisko na zinalingana na mtazamo wa umakini mkubwa kuelekea imani ya ibada rahisi na inayopendwa na wengi. Je, kipengele hiki ni muhimu kwa kiasi gani?
Tunahitaji kuweka kiini cha marejeo ya imani. Imani inayopendwa na watu wengi hutajirishwa kwa kumweka Mama wa Mungu kama sehemu ya kumbukumbu na sehemu kamili ya marejeo, Bwana Yesu Kristo. Mama wa Mungu ambaye anayekuongoza kwenye mkutano huo. Wakati watu rahisi wanakuja na shida zao zote, wanakutana na Mama wa Mungu ambaye aliteseka kama wao. Picha ya Mama Yetu wa Huzuni iko karibu katika parokia zote: yeye aliyeteseka kama wewe, na kukusindikiza kwa Bwana Yesu anayekupa nguvu za kuishi vizuri. Kubadilisha maisha sio kuacha familia yako, kuacha kazi yako ... ukirudi kwenye maisha yako ya zamani, unabadilishwa ndani. Unajua kwamba kwa Bwana ninaweza kukabiliana na matatizo. Hapa kuna imani ya walio rahisi. Hapa kuna Rozari, Ekaristi na kuabudu Ekaristi. Msimu kiangazi uliopita nilikuwa na vijana 30/40 elfu ambao walikuwa wakiabudu kwa ukimya kabisa. Hapo, katika mkate huo uliogeuzwa, ni uwepo halisi, wa hakika wa Bwana Yesu Kristo. Ananitazama, ninamtazama, anazungumza nami, nazungumza naye. Ni watu wangapi wameniambia: Nilimsikia Bwana akizungumza nami pale.
Kutokana na yale uliyotuambia na kutokana na yale tuliyosoma katika Dokezo la Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kuhusu tukio la Medjugorje, je, tunaweza kuhitimisha kwa kutoa mwaliko kwa kila mtu ili kuhiji?
Hati hiyo inasema wazi: nenda Medjugorje kwa sababu ni mahali pa neema.