Kumbukumbu Marehemu Wote: Matumaini, Kumbukumbu na Heri za Mlimani
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Tangu Kanisa la Mwanzo, Wakristo walijijengea utamaduni wa kuwakumbuka, kuwaenzi na kuwaombea waamini wote Marehemu. Hii ni Ibada inayopata chimbuko lake katika asili ya mwanadamu. Kumbukumbu hii inanogeshwa na Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Rej. Kol 1:18. Waamini kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanajiunga na Kristo Yesu na kuanza kutembea katika mwanga wa Pasaka. Rej. Rum 6:3-4. Huu ni ushirika na Kanisa ambalo bado linasafiri huku bondeni kwenye machozi na watakatifu wa mbinguni Rej. LG 49. Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 2 Novemba, anawakumbuka na kuwaombea waamini wote marehemu “Commemoratio Omnium Fidelium Defunctorum” waliotangulia mbele ya haki wakiwa na alama ya imani na sasa wanapumzika kwenye usingizi wa amani. Kumbukumbu inawasaidia waamini kuwatambua na kuwakumbuka wale waliowatangulia mbele za haki, wakiwa na imani na tumaini la ufufuko wa wafu. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya kumbukumbu ya kuwaombea waamini wote marehemu, tarehe 2 Novemba 2024, majira saa 4:00 kwa Saa za Ulaya sawa na Saa 6:00 Mchana kwa Saa za Afrika Mashariki na Kati, anatarajia kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Makaburi ya Laurentino. Hii ni mara ya pili kwa Baba Mtakatifu kutembelea na kusali katika Makaburi haya, mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 2018 alipokazia kuhusu: Kumbukumbu, Matumaini na Heri za Mlimani, Muhtasari wa mnafundisho makuu ya Kristo Yesu, dira na mwanga wa maisha ya mwamini!
Mama Kanisa anakiri na kufundisha juu ya “Ufufuko wa wafu na uzima wa milele.” Kumbukumbu ya Waamini Marehemu Wote kwa upande mmoja inagubikwa na huzuni na kwamba, makaburini ni mahali ambapo panaonesha huzuni ya moyo. Ni mahali ambapo waamini wanawakumbuka na kuwaombea ndugu, jamaa na marafiki zao waliotangulia mbele ya haki wakiwa na tumaini la ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Makaburi yanawakumbusha waamini kwamba, hapa duniani wao ni wasafiri na wala hawana makazi ya kudumu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kumbukumbu ya waamini Marehemu ni tukio la matumaini katika ufufuko wa wafu, ndiyo maana waamini wanaendelea kuyapamba makaburi kwa maua. Ni kumbukumbu ambayo imechanganyika kati ya huzuni na matumaini; mambo msingi yanayogubika nyoyo za waamini wanapowakumbuka na kuwaombea Marehemu wao. Matumaini ya ufufuko wa wafu yanawasaidia waamini kuendelea na hija kuelekea katika Fumbo la kifo, hapa kila mtu anashiriki “kivyake vyake.” Kuna baadhi watakabiliana na Fumbo la kifo kwa mateso na mahangaiko makubwa, lakini daima wakiwa na maua ya matumaini ya ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Imani kwamba kuna maisha baada ya kifo ni ya kale kabla hata ukristo haujaja. Wahehe kwa mfano waliamini baada ya kufa watu wanaishi katika ulimwengu wa mahoka na mizimu. Huko wanaendelea kuwa na hadhi zao kama hapa duniani ndio akina babu, bibi, mtoto, chifu/mtwa... Huko nako kuna hukumu kwa walioishi vibaya na zawadi kwa walioishi vizuri.
UFAFANUZI: Wakristo tunaamini pia maisha ya uzima wa milele. Makanisa matatu ya mbinguni, duniani na toharani yanashirikiana yakisaidiana sala ili siku moja liwe kundi moja tu la wateule wa mbinguni. Shairi 1 – ‘Hapa we msafiri simama na tazama, nimekufa leo kesho ni yako zamu…’ kumbe sisi tu wasafiri, duniani sio kwetu, saa ikifika tutakufa, marehemu watarajiwa. Kwamba tu wasafiri laeleza somo I (Hek 3:1-9) “roho zao wenye haki wamo mikononi mwa Mungu...” kadiri ya somo hili mauti haitakuwako tena. Maneno haya yanafanana na yale yaliyoandikwa katika makaburi ya wamonaki wabendiktini huko Peramiho jimbo kuu la Songea. Nchini Tanzania yanayosomeka katika lango la kuingilia “Jana tulikuwa kama ninyi na kesho nanyi mtakuwa kama sisi” maneno yanayotukumbusha kuwa hapa sisi ni wapitaji tu. Somo la Pili kutoka katika Kitabu cha Ufunuo (Ufu 21:1-7) linasisitiza jambo hilo, maisha bila kufa “ukamilifu wote katika maskani ya Mungu, naye atafuta machozi yao, wala mauti haitakuwapo tena, wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu. kila kitu kitakuwa kipya katika Mungu aliye Alfa na Omega, mwanzo na mwisho.” Ikiwa sote tutakufa kwa nini tusipendane tu? Shairi 2 “nilikuja peke, narudi peke yangu, kwa herini ndugu tutaonana kesho, ona vema nilivyokuwa humu na nilivyoacha mali na jamaa…” ukweli mchungu huu!! Mtu nimekuja peke yangu na nitaondoka peke yangu kwa nini namnyanyapaa mwenzangu? Kwa nini nanyanyua mabega na kujiona bora kuliko mwingine, ninamfahamu atakayenizika? tupendane tu. Shairi 3 “nilitoka uchi tumboni mwa mamangu, ninarudi uchi tumboni mwa udongo, ona vema…” maana yake tulikuja duniani bila kitu na tutaondoka bila kitu... “sikieni ninyi nyote mnaokaa duniani, watu wakuu na wadogo wote pia, tajiri na masikini wote pamoja… hakuna mtu awezaye kumkomboa ndugu yake wala kumpa Mungu fidia ili aishi siku zote, asipate kuonja kaburi... hata wenye hekima hufa, mpumbavu na mjinga hupotea pamoja, na kuwaachia wengine mali zao.
Makaburi ni makao yao hata milele… usiogope mtu atakapopata utajiri na fahari ya nyumba yake itakapozidi, maana atakapokufa hatachukua chochote, utukufu hautashuka kumfuata, ajapo jibariki nafsi yake alipokuwa hai, na watu watakusifu ukijitendea mema, atakwenda kwenye kizazi cha baba zake, mwanadamu hatadumu katika fahari yake, atakufa tu kama mnyama” (Zab 49). Ouh jamani, ukweli huu unatuelemea!... wote, japo tumetofautiana vyeo na madaraka, umri, mali, akili, vipaji, umaarufu tunafanana makaburi yetu... nyumba ndogo futi 6 tu. haijalishi umezikwa na watu wangapi, jeneza la dhahabu, la mabanzi au bila jeneza ukweli unabakia kwamba umekufa na umezikwa... TanzaniNinapokumbuka nitakufa na kuzikwa nakosa nguvu, najiona mnyonge nisiye na ujanja. Namkimbilia Bwana anijaliaye kila kitu, huruma yake tu ndio tegemeo langu. Kila mmoja aone leo namna anavyoitikia wito wa Kristo wa kumtumikia ipasavyo. Kristo anatuita, shime tumwendee, tusijicheleweshe njiani... “Wapenzi waitwa juu wasema harakisha... Wapenzi Yesu atuita, kwani tunachelewa acheni ya duniani amini yake Yesu… mbinguni kwa Bwana Yesu ndiko hazina yetu, malaika nipelekeni Yesu unipokee...” Tunaitwa kila mmoja kwa namna yake, tunaitwa kuitafuta amani kwa kila hali. tunaitwa tuutafute wokovu, tuziinue nyuso zetu kwa Bwana tukiomba huruma yake, msamaha wa dhambi na heri ya milele mbinguni. “Mtu akinitumikia na anifuate, nami nilipo ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo” (Yn 12:26). utumishi huo ni wito wa kimapendo... tunaitwa kupenda mapatano kuliko ugomvi, maridhiano kuliko ubabe, tabasamu kuliko chuki, umoja kuliko utengano. Migogoro na chuki za kidini, kisiasa na kiitikadi, ugomvi na manyanyaso vitatuweka muda mrefu toharani… kiburi na majivuno vitatuweka muda mrefu toharani, ulevi na ulafi na yanayofanana na hayo yatatuweka muda mrefu zaidi toharani. Kwa vile hatujui siku yetu tujiweke tayari, kuwa na hali njema kiroho na zaidi sana kumkabidhi Mungu maisha yetu na kutenda yanayopasa Injili... Ee Mungu Mwenye huruma utuhurumie sisi marehemu watarajiwa, amina.