杏MAP导航

Tafuta

Haki ya uhuru wa dini msingi wake ni hadhi ya binadamu ijulikanayo kwa njia ya Neno la Mungu lililofunuliwa na ya akili. Haki ya uhuru wa dini msingi wake ni hadhi ya binadamu ijulikanayo kwa njia ya Neno la Mungu lililofunuliwa na ya akili.  (ANSA)

Uhuru wa Dhamiri na Uhuru wa Kidini Ni Sehemu ya Haki Msingi za Binadamu

Binadamu anayo haki ya uhuru wa dini. Uhuru huo ndio huu, kwamba, kila binadamu lazima akingiwe na shurutisho la mtu mmoja mmoja, la makundi ya kijamii, au la mamlaka yoyote ya kibinadamu. Hivyo kwamba, katika mambo ya dini mtu yeyote asishurutishwe kutenda dhidi ya dhamiri yake, wala asizuiliwe, katika mipaka inayokubalika kutenda kulingana na dhamiri yake binafsi au hadharani, peke yake au katika muungano na wengine. Msingi wake ni utu wa binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walitangaza “declarat” kwamba, binadamu anayo haki ya uhuru wa dini. Uhuru huo ndio huu, kwamba, kila binadamu lazima akingiwe na shurutisho la mtu mmoja mmoja, la makundi ya kijamii, au la mamlaka yoyote ya kibinadamu. Hivyo kwamba, katika mambo ya dini mtu yeyote asishurutishwe kutenda dhidi ya dhamiri yake, wala asizuiliwe, katika mipaka inayokubalika kutenda kulingana na dhamiri yake binafsi au hadharani, peke yake au katika muungano na wengine. Haki ya uhuru wa dini msingi wake ni hadhi ya binadamu ijulikanayo kwa njia ya Neno la Mungu lililofunuliwa na ya akili. Haki hii ya binadamu ya uhuru wa dini yatakiwa kuzingatiwa katika sheria za jamii ili iwe haki ya raia. (Rej. DH, namba 2). Mtakatifu Paulo VI alichangia sana katika maboresho na hatimaye tamko kuhusu Uhuru wa Kidini ambao alitoa ufupisho wake kwa kusema, “Nemo cogatur, nemo impediatur” yaani katika mambo ya dini hakuna mtu anayepaswa kuzuiliwa wala kulazimishwa. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulizingatia hasa: mema ya kiroho kwa kila mtu; ukweli na haki; Mapokeo na Mafundisho ya Kanisa. Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya wokovu wa mwanadamu. Kanisa linawajibu wa kutangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, linahimiza umuhimu wa kulinda dhamiri nyofu pamoja na wajibu wa kimaadili. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipania pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kwamba: Wanaendeleza Mafundisho ya Kanisa kuhusu haki msingi za binadamu zisizoondoleka, na katika sheria za muundo wa jamii. (Rej. DH. n.1). Kumbe, kuna haja ya kuendelea kufunda dhamiri za watu, ili kutambua utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Uhuru wa kidini ni sehemu ya haki msingi za binadamu
Uhuru wa kidini ni sehemu ya haki msingi za binadamu   (ANSA)

Uhuru wa kidini unafumbatwa katika misingi ya ukweli na haki na kwamba, uhuru wa kidini ni kati ya changamoto pevu inayopaswa kuvaliwa njuga katika ulimwengu mamboleo. Tamko hili ni amana na utajiri wa Mama Kanisa, mintarafu wajibu wake wa kimaadili, ulioisaidia Jumuiya ya Kimataifa kufanya mageuzi makubwa katika masuala ya kisiasa, kijamii sanjari na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa. Uhuru wa dini ni dhana inayoweza kusaidia kukuza demokrasia kwa kuzingatia tunu msingi zinazofumbatwa katika imani. Mama Kanisa anawahimiza watoto wake kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kamwe waamini wa dini mbalimbali wasitumbukie katika mchakato wa dhana ya wongofu wa shuruti. Dhamiri nyofu ni mahali patakatifu sana katika maisha ya mwanadamu, mahali ambapo sheria ya Mungu imeandikwa katika moyo wa mwanadamu. Vatican imekuwa mstari wa mbele kuhamasisha uhuru wa kidini katika medani za Jumuiya ya Kimataifa, kwa kukemea vikali misimamo mikali ya kidini ambayo imekuwa ni chanzo cha maafa kwa watu wasiokuwa na hatia sanjari na kuvuruga mchakato wa demokrasia ya kweli. Kanisa lina haki ya kushiriki katika maisha ya hadhara kwani linapania kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili. Akili ya mwanadamu inatambua uhuru wa dini kama sehemu ya haki msingi za binadamu, inayofumbata, utu na heshima yake. Uhuru wa kidini unapaswa kushuhudiwa katika maisha ya faragha na yale ya hadharani. Hii ni changamoto kubwa katika ulimwengu wa utandawazi, maendeleo ya sayansi na teknolojia. Uhuru wa dini ni nguzo ya haki msingi za binadamu; ni kiiini cha Habari Njema ya Wokovu na ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu.

Uhuru wa kuabudi ni sehemu ya haki msingi za binadamu
Uhuru wa kuabudi ni sehemu ya haki msingi za binadamu

Uhuru wa kuabudu na kidini unaweza kusaidia kukuza na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Hii ni chachu ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa na kwamba, ukweli na uwazi ni kanuni msingi katika majadiliano ya kidini na kiekumene. Kumbe, hapa kuna haja ya kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini. Kuna baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanaotaka kuzima uhuru wa kuabudu au kung’oa kabisa uhuru wa kidini kutoka katika masuala ya kisiasa na matokeo yake ni kuibuka kwa kasi kubwa chuki dhidi ya imani, dhuluma na nyanyaso za kidini. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa, Jumanne tarehe 24 Septemba 2024 amehutibia Senate ya nchi ya Poland kwa kujikita katika uhuru wa dhamiri na uhuru wa kidini mintarafu nchi ya kidemokrasia. Amejikita zaidi katika Tamko la Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu uhuru wa kidini, mwendelezo wa tafakari yake katika kipindi cha takribani miaka sitini iliyopita, tangu Mtakatifu Paulo VI hadi Baba Mtakatifu Francisko kwa kukazia haki na amani; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ni mwaliko wa kusimama kidete kupinga kwa nguvu zote misimamo mikali ya kidini na kiimani na badala yake watu wapende kujikita katika misingi ya haki, amani na maridhiano pamoja na kutambua tofauti msingi kati ya dini na siasa. Demokrasia ya kweli inasimikwa katika uhuru wa kweli na wenye ukomo kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema; ukweli na dhamiri nyofu.

Uhuru wa Kidini Poland
24 Septemba 2024, 14:35