Moyo wa mchungaji na imani ya watu
Na Andrea Tornielli
Nuru rasmi ya kijani kwa ajili ya ibada na uzoefu wa kiroho ambayo ilianza Medjugorje mnamo Juni 1981, wakati watoto sita waliripoti kuona Mamma, iliwezekana kutokana na matunda mengi mazuri yaliyoonekana katika parokia, ambayo zaidi ya watu milioni 1 hutembelea kila mwaka kutoka pande zote ulimwengu. Matunda haya ni pamoja na hija, uwongofu, watu kurudi kwenye Sakramenti, na ndoa zenye matatizo zinazoanza njia ya uponyaji. Haya ndiyo mambo ambayo Baba Mtakatifu Francisko ameyazingatia siku zote, hata alipokuwa Askofu huko Argentina, akithibitisha kwamba uchaji wa Mungu unaowasukuma watu wengi kuelekea kwenye madhabahu ni lazima uambatane, urekebishwe inapobidi, lakini usizuiwe. Wakati wa kuhukumu matukio yanayodaiwa kuwa ya kimbinguni, umakini lazima upewe kwa matunda ya kiroho. Mtazamo huu wa Mrithi wa Petro unalingana na kanuni mpya zilizochapishwa mwezi wa Mei ambazo zimetenganisha hukumu ya Kanisa kutoka katika utambuzi unaodai zaidi wa tukio lisilo la kawaida.
Hija bado inaweza kuendelea, lakini si lazima tena kungojea kuidhinisha ibada na hija, bali kitu muhimu ni kwamba pasiwepo udanganyifu au masilahi yaliyofichika, ujumbe ni wa kweli na zaidi ya yote, uzoefu mwingi mzuri unathibitishwa. Shukrani kwa moyo wa Mchungaji Papa Francisko, tamko juu ya mojawapo ya maonesho maarufu na yenye utata ya Maria wa karne iliyopita umefanyika. Ni uamuzi ambao hauji kwa mshangao. Tayari mnamo Mei, Kardinali Fernandez, akijibu swali kuhusu Medjugorje, alikuwa amesema: “Kwa kanuni hizi, tunafikiri itakuwa rahisi kusonga mbele na kufikia hitimisho.” Huu si mtazamo ambao haujawahi kushuhudiwa, kama inavyothibitishwa na maneno yaliyotumiwa na Kardinali Ratzinger wakati huo katika mahojiano marefu ya kitabu kuhusu “Ripoti ya Ratzinger:” “Mojawapo ya vigezo vyetu ni kutenganisha kipengele cha kweli au kinachodhaniwa kuwa ni ‘umungu wa asili’ wa mwonekano na ule wa matunda yake ya kiroho.
Hija za Ukristo wa kale zilielekezwa kwenye maeneo ambayo roho yetu ya kisasa ya kuchambua inaweza nyakati fulani kutatanishwa kuhusu ‘ukweli wa kisayansi’ wa mapokeo yanayohusishwa nazo. Hii haimaanishi kwamba hija hizi hazikuwa na matunda, zenye manufaa, muhimu kwa maisha ya watu wa Kikristo. Tatizo si zaidi ya mtazamo wa kisasa wenye uchangamfu (ambao huishia, miongoni mwa mambo mengine, katika namna mpya ya kusadikika) bali ni kutathmini uhai wa maisha ya kidini unaositawi katika maeneo haya.” Papa Benedikto XVI mwenyewe, mnamo mwaka 2010, alikuwa ameunda Tume iliyoongozwa na Kardinali Ruini kuchunguza jambo hilo, na matokeo yalikuwa mazuri.
Ujumbe, uliopewa jina: “Malkia wa Amani,” kwa hivyo unatambua wema wa matunda, unatoa uamuzi mzuri wa jumla wa ujumbe mwingi unaohusiana na Medjugorje ambao umesambazwa kwa miaka mingi, kusahihisha maandishi yenye shida na tafsiri zingine ambazo zinaweza kuwa zimeathiriwa kwa ushawishi wa kibinafsi wa wanaodaiwa kuwa na maono. Kuhusu watoto ambao walikuwa wahusika wakuu wa jambo hilo, ambao kwa miaka mingi walikuwa chini ya mabishano na hata shutuma, hati hiyo inafafanua kutoka katika mistari ya kwanza kabisa kwamba idhini haimaanishi hukumu juu ya maisha yao ya maadili na kwamba, kwa hali yoyote, kiroho, zawadi “hazimaanishi hukumu kuhusu maisha ya kimaadili ya wanaodaiwa kuwa na maono.” Wakati huohuo, ukweli wenyewe kwamba idhini iliyotolewa inaashiria kwamba hakuna vipengele muhimu au vya kutiliwa shaka vilivyogunduliwa, wala uwongo, uzushi, au visasili. Ujumbe wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa unamulika sehemu kuu mbili za ujumbe wa Medjugorje: ule wa uongofu na kurudi kwa Mungu, na ule wa amani.
Jambo hilo lilipoanza na Maria alionekana kama “Malkia wa Amani,” hakuna mtu ambaye angeweza kufikiria kwamba nchi hizo zingekuwa ukumbi wa mapigano ya umwagaji damu wakati wa vita vya Balkan. Mwandishi wa habari hii aliguswa sana aliposhiriki katika hija, kutoka katika ushuhuda wa marafiki na raia wenzake wa waonaji maono: watu ambao hawakuhusika kwa njia yoyote katika maonesho au ujumbe, ambao, walikabiliwa na ukatili wa vita vilivyofanyika katika nchi hizo hata kati ya majirani, walikuwa wamepata njia ya kusamehe. Shukrani kwa uzoefu wao wa imani uliohusishwa na matokeo ya Medjugorje, walikuwa wamepatanishwa hata na wale ambao walikuwa wamefanya vitendo vikali vya jeuri dhidi ya jamaa zao. Hii inawakilisha kipengele cha ‘muujiza’ zaidi kuliko matukio mengine mengi yanayojadiliwa karibu na eneo la matokeo yanayodaiwa. Ujumbe halisi wa Medjugorje hatimaye upo katika jumbe hizo ambazo Mama hujinyenyekeza na kuwaalika kila mtu kutofuata manabii wa uwongo, wala kutafuta habari kuhusu "siri" na utabiri wa mwisho wa dunia (apocalyptic.) Ujumbe mmoja wa Novemba 1982 unathibitisha hili: “Usiende kutafuta mambo yasiyo ya kawaida. Badala yake, chukua Injili, isome, na kila kitu kitakuwa wazi kwako.