Mons.Balestrero:wanafamilia wanasaidiana kukua na hekima na kuoanisha haki na mahitaji mengine
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika Makao ya Umoja wa Mataifa, Askofu Mkuu Ettore Balestrero alitoa tamko katika Kikao cha 57 cha kawaida cha Bara la Haki za Kibinadamu tarehe 25 Septemba 2024, huko Geneva nchini Uswiss. Askofu Mkuu akianza hotuba yake alisema kuwa: “Tamko la Kimataifa la Haki za Kibinadamu linatambua familia kama kitengo cha asili na cha msingi cha jamii na inathibitisha kwamba ina haki ya kulindwa na jamii na Serikali." Haya pia yamesisitizwa na Vatican mara kwa mara kwamba: “Mustakabali wa ubinadamu unapita kwa njia ya familia", ambayo kushamiri kwake kunachangia ustawi wa taifa. Ndani ya familia, wanadamu huzaliwa na kujifunza kuheshimu na kukuza utu wa kibinafsi katika vizazi. Wakiongozwa na kanuni ya “kutoa bure”, wanafamilia wanasaidiana kukua na hekima zaidi na kuoanisha haki za kibinafsi na mahitaji mengine ya maisha ya kijamii.”
Familia ni shule ya ubinadamu wa ndani zaidi
Kwa hivyo familia hutumika kama shule ya ubinadamu wa ndani zaidi, iikiwa na jukumu muhimu katika kutetea haki za binadamu za washiriki wake. Kwa hivyo, ni muhimu kuendeleza sera za kijamii, kiuchumi na kitamaduni zenye mwelekeo wa familia katika ngazi za ndani na kimataifa. Sera hizo zinapaswa kujumuisha, pamoja na mambo mengine, hatua za kukuza ndoa na kutegemeza familia, kulinda uhai, kupatanisha kazi na maisha ya familia, na kuwasaidia wazazi katika jukumu lao la kuwa waelimishaji wa msingi wa watoto wao. Katika enzi ya sasa, idadi kubwa ya wanandoa huchagua kukataa kupata watoto. Hii ina madhara makubwa kwa uhai na mshikamano wa jamii, yenye uwezo wa kuathiri hata uthabiti wa mifumo ya ustawi na uchumi wenyewe.
Familia inazidi kudharauliwa na kudhalilishwa
Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican aidha alisema kuwa Ujumba wake “pia una wasiwasi kwamba familia inazidi kudharauliwa na kudhalilishwa katika mikutano ya kimataifa. Majibu ya kwamba ‘watu binafsi na wala si familia ni wamiliki wa haki’ mara nyingi hutumiwa kwa njia ya aibu kama kisingizio cha kupunguza au kukataa lugha au mipango inayolenga kulinda na kukuza familia kama manufaa ya kimsingi ya pamoja. Familia ni jamii ya kwanza na pia mahali pa pekee pa kupata elimu na malezi ili kuchangia vyema maisha ya jamii. Kwa hiyo, ni jambo la msingi kabisa, si la nyongeza wala si la kushtukiza, wala halina madhara hata kidogo, kwa utambuzi kamili na kufurahia haki za binadamu za wote. Katika suala hili, inapaswa pia kusisitizwa kuwa familia mara nyingi ni mtetezi mkuu na msaidizi wa walio hatarini zaidi katika jamii: wasiozaliwa, watoto, wazee na watu wenye ulemavu. Ni matumaini ujumbe wake kwamba mjadala huu muhimu wa jopo utafanya kuhimiza ufahamu wa kina na kujitolea upya kwa familia katika kazi ya Baraza la Haki za Binadamu. “Kama familia inavyoenda, ndivyo taifa linavyokwenda na ndivyo inavyoenda ulimwengu wote tunamoishi.”