杏MAP导航

Tafuta

Takwimu zinaonesha kwamba, Mataifa yanaendelea kuwekeza zaidi katika biashara na matumizi ya silaha za kivita, hatari kwa usalama na amani ya Jumuiya ya Kimataifa. Takwimu zinaonesha kwamba, Mataifa yanaendelea kuwekeza zaidi katika biashara na matumizi ya silaha za kivita, hatari kwa usalama na amani ya Jumuiya ya Kimataifa.  Tahariri

Mataifa Yanaendelea Kuwekeza Katika Biashara Na Matumizi ya Silaha: Hatari Kwa Amani

Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika Tahariri yake kuhusu maneno ya Baba Mtakatifu Francisko kuhusu madhara ya vita anasema, kuna mamilioni ya watu hawana bima ya afya na hivyo wanaogelea katika dimbwi la magonjwa na vifo. Vijana hawana fursa za ajira na kwamba, familia nyingi zinapambana na hali ngumu ya maisha na umaskini! Hatari!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Amani inasimikwa katika misingi ya: Ukweli, haki, upendo na uhuru kama anavyofafanua Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa Kitume “Pacem in terris” yaani: “Amani Duniani.” Kimsingi, watu wanatofautiana kwa mambo mengi sana, lakini kanuni hizi zinaweza kutumika ili kuheshimu na kuwawajibisha wanasiasa, ili kujizatiti katika kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hii ni changamoto kwa watu wa Mungu kudumisha upendo, kwa kukuza majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi; mshikamano na matumizi bora zaidi ya nguvu kazi. Amani duniani inahatarishwa sana kutokana na vitisho vya silaha za nyuklia na mchakato wa kuendelea kuwekeza katika biashara na matumizi ya silaha duniani. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, amani siyo tu kutokuwepo kwa vita, kinzani wala mipasuko ya kijamii bali ni matunda ya haki, maendeleo, mshikamano wa udugu wa kibinadamu, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na kusimamia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanaendelea kuwekeza sana katika biashara na matumizi ya silaha kama inavyojionesha katika vita inayoendelea sasa kati ya Urussi na Ukraine.

Mataifa yanaendelea kuwekeza zaidi katika biashara na matumizi ya silaha za kivita.
Mataifa yanaendelea kuwekeza zaidi katika biashara na matumizi ya silaha za kivita.

Kuna kiasi kikubwa cha rasilimali fedha kimechepushwa na kupelekwa ili kuongeza nguvu za kijeshi katika vita kati ya Urussi na Ukraine. Hii ni rasilimali fedha ambayo ilipaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa familia nyingi ambazo zinateseka na umaskini kutokana na athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa. Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika Tahariri yake kuhusu maneno ya Baba Mtakatifu Francisko kuhusu madhara ya vita anasema, kuna mamilioni ya watu hawana bima ya afya na hivyo wanaogelea katika dimbwi la magonjwa na vifo. Kuna watu na hasa vijana wamekatishwa na kujikatia tamaa ya maisha kwa kukosa fursa za ajira na kwamba, hali ngumu ya uchumi imepelekea Serikali nyingi kushindwa kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji wamaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Kuna mamilioni ya watu wanaopekenyuliwa kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha, mambo yanayokwenda kinyume kabisa cha utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufuata nyayo za watangulizi wake kukemea na kulaani vita kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Yohane Paulo II dhidi ya Vita ya Ghuba ya Uajemi na hatimaye kupinduliwa kwa Rais Saddam Hussein na matokeo yake nchini Iraq. Kuibuka kwa vikundi vya kigaidi na madhara yake katika Jumuiya ya Kimataifa. Inasikitisha kuona Mataifa yakitumia asilimia 2% ya Pato Ghafi la Taifa, GNP kwa ajili ya biashara na matumizi ya silaha. Vita inaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Bado kuna mashindano makubwa mintarafu madaraka, nguvu ya kiuchumi na kivita. Falsafa ya vita haina tena nafasi kwa sababu ni chanzo kikuu cha maafa ya watu na mali zao bila kusahau uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote. Tangu mwaka 2016 nchi za Ulaya zimeongeza bajeti yake kwa matumizi ya kijeshi kwa asilimia 24.5%. Kanisa linatambua umuhimu wa nchi kulinda usalama wa raia na mali zao, lakini katika miaka ya hivi karibuni kuna ongezeko kubwa la biashara na matumizi ya silaha za maangamizi, hatari katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano anakaza kusema, kuna haja ya kusikiliza na kujibu kwa vitendo mwaliko wa Baba Mtakatifu Francisko wa kuwekeza katika ujenzi wa utamaduni wa haki, amani, maridhiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ni wakati muafaka wa kuwajibika kimaadili ili kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa vijana wa kizazi kipya, kwa kulinda na kutunza ikolojia sanjari na kuondokana na biashara pamoja na matumizi ya silaha. Vita baridi inapaswa kuzikwa na kusahaulika kama ilivyo kwa Ukuta wa Berlin.  

Tahariri Vita
28 Machi 2022, 16:03