Hija ya Kitume ya Papa Francisko Cyprus na Ugiriki: Huduma ya Upendo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis linatoa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema, wanahamasishwa kuwa ni vyombo, mashuhuda na wajenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu katika huduma ya upendo. Caritas Internationalis imejiwekea Malengo Makuu 17, ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi kwa ajili ya kudumisha utu, heshima, haki, ustawi na kuendelea kujikita katika maendeleo fungamani ya binadamu! Caritas Cyprus ilianzishwa kunako mwaka 1979 na kusajiliwa rasmi kunako mwaka 1986. Kutokana na athari za myumbo wa uchumi kitaifa na Kimataifa, idadi ya watu wanaohudumiwa na Caritas Cyprus imeongezeka maradufu kutoka watu 2, 300 katika kipindi cha kati ya mwaka 2019- 2020. Kati ya mwaka 2021 idadi imeongezeka na kufikia kiwango cha watu 3, 822 kutoka katika nchi 66 tofauti tofauti. Hii ni huduma inayotolewa huko Larnaca, Limassol na Pathos. Huduma zinazotolewa ni pamoja na: chakula, malazi, dawa, ajira, ushauri nasaha na elimu kwa watoto wadogo pamoja na huduma za kisheria na msaada elimu kwa watoto.
Kwa upande wake, Caritas Greece “Caritas Hellas” ni mwanachama wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, tangu mwaka 1952. Kati ya Mwaka 2019-2020 Caritas Greece ilitoa huduma kwa watu 18, 260 huko Lesvos, watu 5, 400, Kisiwa cha Chios na Samos watu wanaohudumiwa ni 3, 700. Tangu mwaka 2015 Caritas Greece imeendelea kutoa huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na wale wote wanaotafuta hifadhi ya kisiasa Kisiwani hapo. Tangu kufumuka kwa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 Caritas Greece inaendelea kujielekeza katika mapambano dhidi ya UVIKO-19, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kitaifa na Kimataifa. Caritas inaendelea pia kutoa msaada kwa kuwajengea wanawake na wasichana uwezo wa kujitegemea kiuchumi. Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na huduma zinazotolewa kwa wakimbizi na wahamiaji Kisiwani Lesvos kunako mwaka 2019 alichangia kiasi cha Euro 100, 000. Kwa msaada wa Caritas Italia, Caritas Ujerumani pamoja na Ubalozi wa Vatican nchini Ugiriki, Caritas Greece imeendelea kutoa msaada wa makazi bora kwa watu 80.