Papa Francisko: Hija ya Kitume Romania: Majadiliano ya kiekumene
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 31 Mei hadi 2 Juni 2019 anafanya hija ya 30 ya kitume kimataifa inayoongozwa na kauli mbiu “Twende pamoja” ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa; kwa kufuata nyayo za mashuhuda wa imani, waliomimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake! Baba Mtakatifu anakwenda nchini Romania kama hujaji na ndugu yao katika Kristo ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano unaokita mizizi yake katika amana na utajiri wa imani nchini Romania!
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Vatican News anasema kwamba, hija ya Baba Mtakatifu inakita ujumbe wake katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, changamoto na mwaliko wa kuvumbua tena tunu msingi za maisha ya kiroho, katika ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili familia ya Mungu nchini Romania iweze kwenda kwa pamoja! Baba Mtakatifu anaanza hija hii, wakati ambapo Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria kumtembelea Elizabeth na hapo waamini wanaomba mapendo ya jirani!
Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Romania kutembea kwa pamoja katika fadhila ya unyenyekevu, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya huduma hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anataka kushirikiana na kushikamana na waamini katika hija hii, ili kuwahamasisha kuwa ni mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo, kwa kutambua na kuthamini amana na utajiri unaofumbatwa nchini Romania kutokana na uwepo wa Kanisa la Kiorthodox.
Baba Mtakatifu anataka kuwahamasisha vijana kujenga na kudumisha utamaduni wa wa watu kukutana na kusaidiana katika maisha; kwa kutambua kwamba, tofauti zao msingi ni amana na utajiri na kamwe si sababu ya chuki, uhasama na utengano. Haya ndiyo mambo msingi ambayo Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwashirikisha watu wa Mungu nchini Romania wakati wa hija yake kitume. Hii ni hija ya kitume, inayobeba uzito mkubwa katika majadiliano ya kiekumene na waamini wa Kanisa la Kiorthodox nchini Romania. Hii ni sehemu ya kumbu kumbu endelevu ya hija iliyofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II, miaka ishirini iliyopita, yaani kunako mwaka 1999.
Tangu wakati huo, malango ya nchi zenye waamini wengi wa Kanisa la Kiorthodox yakaanza kufunguka. Changamoto iliyotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II ilikuwa ni umoja, hatua kubwa katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuimarisha mchakato huu kwa kukazia: Uekumene wa damu unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani kiasi hata cha waamini kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Hawa ni waamini “wanaofyekelewa mbali” kutokana na ukosefu wa uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini, sehemu muhimu sana ya haki msingi za binadamu. Wao wamejenga umoja katika mateso na kifo na sasa wanafurahia maisha na uzima wa milele, changamoto na mwaliko wa kuendelea kufuata nyayo zao!
Ni Uekumene wa maisha ya kiroho kwa kuthamini utajiri na amana ya tunu msingi za maisha ya kiroho miongoni mwa waamini wa Makanisa haya mawili. Huu ni Uekumene wa sala na huduma ya Injili ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea nchini Romania alisema kwamba, nchi hii ni Bustani ya Bikira Maria kwa sababu inapambwa na waamini kutoka katika madhehebu mbali mbali ya Kikristo! Hawa ni waamini wanaotoka Romania, Hungaria, Croatia na Poland. Kuna Waarmenia ambao wengi wao ni waamini wa Kanisa la Kiorthodox.
Kardinali Parolin anakaza kusema, Madhabahu ya Bikira Maria wa ?umuleu-Ciuc ni kielelezo makini cha Bustani ya Bikira Maria. Baba Mtakatifu katika mafundisho yake, daima anawahimiza watu kuheshimu na kuthamani historia, kumbu kumbu, mapokeo, mila, desturi na tamaduni njema za nchi zao! Ndiyo maana Baba Mtakatifu anawaalika waamini wote hawa kutembea kwa pamoja, ili kuvuka vizingiti vya utengano wa kihistoria, ili kwa pamoja, waweze tena kuunganishwa na imani moja kwa Kristo Yesu! Miaka ishirini imegota tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea Romania na itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, Nchi za Umoja wa Ulaya zimepiga kura kuwachagua wawakilishi katika Bunge la Umoja wa Ulaya!
Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwaimarisha wananchi wa Romania waliojiunga na Umoja wa Ulaya kunako mwaka 2007 na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa utajiri na amana inayobubujika kutoka katika utamaduni wa Romania. Haki, amani, umoja, uhuru, upendo na mshikamano wa dhati ni kati ya mambo msingi yaliyopewa kipaumbele cha pekee na waasisi wa Umoja wa Ulaya. Lengo ni kuimarisha utu, heshima na haki msingi za binadamu na mshikamano unaoratibiwa na kanuni auni. Hizi ni tunu ambazo zinaweza kusaidia mchakato wa upyaishaji wa Umoja wa Ulaya; tunu ambazo anasema Kardinali Pietro Parolin, katibu mkuu wa Vatican zinapata chimbuko lake kutoka katika Ukristo!