Papa Leo XIV: "Nina kiu," Yesu anadhihirisha ubinadamu wake na wetu pia!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika mzunguko wa Katekesi kuhusu Jubilei 2025, “Yesu Kristo ni Tumaini letu,” kipengele cha III: “Pasaka ya Yesu,” Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 3 Septemba 2025, amejikita na mada ya “Kusulibiwa: Ninaona Kiu”(Yh 19,28). Kwa kuwageukia waamini na mahujaji waliunganika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, mjini vatican, alianza kusema: Katika kiini cha simulizi la Mateso, katika wakati mzito na wa giza nene la maisha ya Yesu, Injili ya Yohane inatupatia maneno mawili ambayo yanajumuisha fumbo kuu: "Naona kiu" (19:28), na mara baadaye: "Imekwisha" (19:30). Ni maneno ya mwisho, ambayo bado yamejaa uzoefu wa maisha, ambayo yanafichua maana ya uwepo mzima wa Mwana wa Mungu. Msalabani, Yesu anaonekana si kama shujaa mshindi, lakini kama mwombaji wa upendo. Hatangazi, halaani, hajitetei. Anaomba kwa unyenyekevu kile asichoweza kujitolea kwa vyovyote.
Kiu ya Aliyesulubiwa sio tu hitaji la kisaikolojia la mwili unaoteswa. Zaidi ya yote, ni maonesho ya shauku kubwa: ya upendo, ya uhusiano, ya ushirika. Ni kilio cha kimya cha Mungu ambaye, baada ya kutaka kushiriki kila kitu cha hali yetu ya kibinadamu, pia anajiruhusu kushibishwa na kiu hii. Mungu ambaye haoni aibu kuomba chakula, kwa sababu katika ishara hiyo anatuambia kwamba upendo, kuwa wa kweli, lazima pia ujifunze kuomba na sio kutoa tu.
Nina kiu, Yesu anasema, na kwa njia hii anadhihirisha ubinadamu wake na wetu pia. Hakuna hata mmoja wetu anayejitegemea. Hakuna anayeweza kujiokoa peke yake. Maisha "hutimizwa" sio tunapokuwa na nguvu, lakini tunapojifunza kupokea. Na kwa hakika wakati huo, baada ya kupokea sifongo iliyolowekwa katika siki kutoka kwa wageni, Yesu anatangaza: Imekwisha. Upendo ukawa mhitaji, na kwa sababu hiyo ulikamilisha kazi yake. Hiki ndicho kitendawili cha Kikristo: Mungu haokoi si kwa kufanya, bali kwa kujiruhusu atendeke. Si kwa kuushinda uovu kwa nguvu, bali kwa kukubali kikamilifu udhaifu wa upendo. Msalabani, Yesu anatufundisha kwamba utimilifu wa kibinadamu haupatikani kwa nguvu, bali katika kuamini uwazi kwa wengine, hata wanapokuwa maadui na uadui kwetu.
Wokovu hauji katika kujitegemea, bali katika kutambua kwa unyenyekevu hitaji la mtu mwenyewe na kujua jinsi ya kulieleza kwa uhuru. Utimilifu wa ubinadamu wetu katika mpango wa Mungu si tendo la nguvu, bali ni ishara ya uaminifu. Yesu haokoi kwa mabadiliko makubwa ya matukio, lakini kwa kuomba kitu ambacho hawezi kutoa peke yake. Na hapa mlango unafungua kwa tumaini la kweli: ikiwa hata Mwana wa Mungu alichagua kutojitosheleza, basi kiu yetu - upendo, maana, haki - si ishara ya kushindwa, lakini ya ukweli. Ukweli huu, unaoonekana kuwa rahisi sana, ni vigumu kukubalika. Tunaishi katika enzi inayothamini utoshelevu, ufanisi na utendakazi.
Hata hivyo, Injili inatuonesha kwamba kipimo cha ubinadamu wetu si kile tunachoweza kufikia, lakini uwezo wetu wa kujiruhusu wenyewe kupendwa na, inapobidi, hata kusaidiwa. Yesu anatuokoa kwa kutuonesha kwamba kuomba si jambo lisilofaa, bali ni ukombozi. Ni njia ya kutoka katika uficho wa dhambi, kuingia tena katika nafasi ya ushirika. Tangu mwanzo, dhambi imetokeza aibu. Lakini msamaha wa kweli huja wakati tunaweza kukabiliana na hitaji letu na kutoogopa tena kukataliwa.
Kwa hiyo kiu ya Yesu msalabani, ni yetu pia. Ni kilio cha wanadamu waliojeruhiwa ambao bado wanatafuta maji ya uzima. Na kiu hii haitutenganishi na Mungu, bali inatuunganisha Kwake. Ikiwa tuna ujasiri wa kukiri, tunaweza kugundua kwamba hata udhaifu wetu ni daraja la mbinguni. Kwa hakika katika kuomba, si kwa kumiliki njia ya uhuru inafunguka kwa sababu tunaacha kujifanya kuwa tunajitosheleza.
Katika udugu, katika maisha rahisi, katika sanaa ya kuomba bila aibu na kutoa bila hesabu, kuna furaha isiyojulikana kwa ulimwengu. Furaha ambayo huturudisha kwenye ukweli wa asili wa utu wetu: sisi ni viumbe vilivyoumbwa kutoa na kupokea upendo. Baba Mtakatifu leo XIV aliendelea kusema kuwa, katika kiu ya Kristo tunaweza kutambua kiu yetu wenyewe. Na jifunze kwamba hakuna kitu zaidi ya kibinadamu, hakuna kitu zaidi ya Mungu, kuliko kuwa na uwezo wa kusema: Nahitaji msaada. Tusiogope kuomba hasa pale tunapoona hatustahili. Tusione aibu kunyosha mkono. Ni hapo hasa, katika ishara hiyo ya unyenyekevu, ambapo wokovu umefichwa. Papa alihitimisha tafakari yake.