Papa Leo XIV:Mungu anataka amani.Ushindi wa silaha ni kushindwa
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mara baada ya Misa takatifu na kabla ya sala ya Malaika wa Bwana, katika fursa ya Kuwatangaza kuwa Watakatifu Pier Giorgio Frassati na Carlo Acutis, Dominika tarehe 7 Septemba 2025, kwa waamni waliounganisha katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu alikuwa na ya kusema: “Ndugu wapendwa, kabla ya kuhitimisha sherehe hii iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu, napenda kuwasalimu na kuwashukuru wote mliojitokeza kwa wingi kusherehekea watakatifu wawili wapya. Ninawasalimu kwa upendo maaskofu na mapadre, na ninawakaribisha kwa heshima wajumbe rasmi na mamlaka mashuhuri.
Katika hali hii hii, Papa aliongeza kusema, “inapendeza kukumbuka kwamba jana(Septemba 6, 2025) Kanisa pia lilitajirishwa na baraka mbili mpya. Huko Tallinn, mji mkuu wa Estonia, Askofu Mkuu Mjesuit Eduard Profittlich, aliyeuawa mwaka 1942 wakati wa mnyanyaso ya serikali ya Kisovieti dhidi ya Kanisa, alitangazwa mwenyeheri. Na huko Veszprém, Hungaria, Mária Magdolna Bódi, mwanamke kijana aliyeuawa mwaka 1945 kwa kuwapinga wanajeshi waliotaka kumbaka, alitangazwa kuwa mwenyeheri. Kwa njia hiyo tumsifu Bwana kwa ajili ya mashahidi hawa wawili, mashahidi jasiri wa uzuri wa Injili.”
Maombi ya Papa Leo XIV kwa ajili ya Ukraine,Nchi Takatifu na duniani kwa ujumla
Papa Leo kadhalika alisema “Kwa maombezi ya Watakatifu na Bikira Maria, tunakabidhi sala yetu isiyo na kikomo ya amani, hasa katika Nchi Takatifu na Ukraine, na katika kila nchi nyingine iliyomwagika damu na vita. Kwa wale walio na mamlaka, ninarudia: sikilizeni sauti ya dhamiri!”
“Ushindi unaoonekana kupatikana kwa nguvu ya silaha,” kupanda kifo na uharibifu, Papa alikazia kiukweli ni kushindwa na kamwe hauleti amani na usalama. Mungu hataki vita. Mungu anataka amani! Na Mungu anawaunga mkono wale waliojitolea kujinasua kutoka katika mduara wa chuki na kutembea njia ya mazungumzo.
Katika Audio mtasikiliza pia mahojiano na walioshiriki Misa Takatifu ya Kutangazwa kuwa Watakatifu Pier Giorgio Frassati na Carlo Acutis.