Papa Leo XIV,Waagostinian:kigezo cha kutathimini matendo yenu,ndicho kiunganishe
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kusikiliza, unyenyekevu na umoja vilikuwa vipengele muhimu alivyojikita navyo, Baba Mtakatifu Leo XIV kwa Watawa wa Shirika la Mtakatifu Agostino, wakati wa mahubiri kwenye Misa ya ufunguzi wa Mkutano wao wa 188 , jioni ya tarehe 1 Septemba 2025, katika Basilika ya Mtakatifu Agostino huko Campo Marzio, katikati mwa jiji la Roma. Zaidi ya mamia ya watawa walikuwapo katika maadhimisho hayo ambayo yamefungua siku hizi za Mkutano hadi tarehe 18 Septemba 2025, utakaofanyika katika Taasisi ya Kipapa ya Baba wa Kanisa, Augustinianum Roma ambapo utawaona wajumbe wa kazi wakiwawakilisha watawa wa kiagostinian 2,341 waliotawanyika katika mabara matano kwenye nyumba 395. Miongoni mwao kuna Askofu wa eneo la Chuquibambilla, Wilder Alberto Vásquez Saldaña, na Askofu Luis Marín wa Mtakatifu Martín, Katibu Msaidizi wa Sinodi ya Maaskofu. Pia walikuwepo watawa kadhaa kutoka katika mashirika mbali mbali ya wanawake wanafuata Kanuni ya Mtakatifu Agostino na watawa wa ndani wa Kiagostinian wakisali pamoja na mapadre, pamoja na kundi la walei walio karibu na shirika hilo.
Baba Mtakatifu aliwasili kwenye Kanisa hilo saa 11:40 jioni, masaa ya Ulaya akifuatana na Mkuu wa Shirika la Mtakatifu Agostino duniani, Padre Alejandro Moral, ambaye alimkaribisha nje. Makofi yalipigwa mara baada ya Papa Leo XIV kuingia ndani ya Kanisa hilo. Baada ya kuvuka kizingiti, Papa alisimama kusali katika Kikanisa cha Mtakatifu Monica na Mtakatifu Nicholas wa Tolentino, upande wa kushoto na kulia wa madhabahu kuu, kwa mtiririko huo.
Kwa njia hiyo baada ya kuanza misa, masomo na Injili, Baba Mtakatifu alianza kusema kwa lugha ya kiingereza kuwa: “Wapendwa kaka na dada, Padre Alejandro Moral, Mkuu wa shirika, ndugu katika uaskofu, Luis na Wilder, na ninyi nyote, ndugu zangu waagostini mliopo hapa. Kabla ya kuanza mahubiri rasmi ambayo yametayarishwa, ninataka tu kuwasalimu ninyi nyote. Na kwa wale ambao wanaelewa Kiingereza lakini hawaelewi Kiitaliano: ombeni ili kupokea zawadi ya Roho Mtakatifu! Na pengine, katika wakati huu mfupi wa kutafakari Neno la Mungu na kile ambacho Bwana anawaomba ninyi nyote, ninyi mnaokaribia kuanza Mkutano mkuu wa Kawaida, mtapewa sio lazima karama ya kuelewa au kuzungumza lugha zote, bali karama ya kusikiliza, karama ya unyenyekevu, na karama ya kukuza umoja, ndani ya Shirika na kwa njia ya Shirika, katika Kanisa na ulimwenguni kote.
Baadaye aliendelea na mahubiri rasimi kwa lugha ya kiitaliano. Tunaadhimisha Ekaristi hii mwanzoni mwa Mkutano Mkuu, wakati wa neema kwa Shirika la Agostinian na dakika ya neema kwa Kanisa zima. Katika Misa hii ya nadhiri ya Roho Mtakatifu, tunaomba kwamba Yeye, ambaye kupitia kwake upendo wa Kristo unakaa ndani ya mioyo yetu (rej. Rm 5:5), aongoze kazi yenu siku baada ya siku. Mwandishi wa kale, akizungumzia Pentekoste (rej. Mdo. 2:1-11), anaielezea kama "ushindi mwingi na usiozuilika wa Roho"( Didimus the Blind, De Trinitate, 6, 8: PG 39, 533). Tumuombe Bwana kwamba hili pia liwe jambo kwenu: kwamba Roho Wake aweze kushinda mantiki yote ya kibinadamu, kwa njia “nyingi na isiyozuilika,” ili Nafsi ya Tatu ya Mungu iwe kweli mhusika mkuu wa siku zijazo. Roho Mtakatifu anazungumza leo kama zamani. Anafanya hivyo katika ("penetralia cordis") na kupitia kaka na dada zetu na hali za maisha. Kwa sababu hiyo, ni muhimu kwamba hali yahalisi ya Mkutano Mkuu kwa kupatana na mapokeo ya karne ya zamani ya Kanisa, iwe ya kusikiliza: kumsikiliza Mungu, kusikiliza wengine.
Kwa kutafakari juu ya Pentekoste, Baba yetu Mtakatifu Agostino, akijibu swali la uchochezi la wale waliouliza kwa nini, leo hii, ishara isiyo ya kawaida ya "glossolalia" hairudiwi, kama ilivyokuwa huko Yerusalemu, inatoa tafakari ambayo nadhani itakuwa ya manufaa sana kwenu katika mamlaka mnayokaribia kutimiza. Agostino anasema: "Mwanzoni, kila mwamini [...] alizungumza kwa lugha zote [...]. Sasa mwili wa waamini huzungumza katika lugha zote. Kwa hiyo, hata sasa, lugha zote ni zetu, kwa kuwa sisi ni viungo vya mwili unaosema "(Mahubiri 269, 1). Wapendwa, hapa, pamoja, ninyi ni viungo vya Mwili wa Kristo, unaonena lugha zote. Ikiwa sio wale wote wa Ulimwengu, hakika wale wote ambao Mungu anawajua ni muhimu kwa utimilifu wa wema ambao, kwa hekima yake ya riziki, anawakabidhi. Kwa hiyo, muishi siku hizi kwa juhudi za dhati za kuwasiliana na kuelewana, na mfanye hivyo kama jibu la ukarimu kwa zawadi kuu na ya pekee ya mwanga na neema ambayo Baba wa Mbinguni anawapatia kwa kuwaita hapa, hasa ninyi, kwa manufaa ya wote.
Na tunakuja kwenye sehemu ya pili: mfanye haya yote kwa unyenyekevu. Mtakatifu Agostino, akitoa maoni yake juu ya namna mbalimbali ambazo Roho Mtakatifu amemimina kwa ulimwengu kwa karne nyingi, anatafsiri wingi huu kama mwaliko wa sisi kujinyenyekeza mbele ya uhuru na kutochunguzwa kwa matendo ya Mungu. Hakuna mtu anayepaswa kufikiria kuwa ana majibu yote. Acheni kila mtu ashiriki kwa uwazi kile alichonacho. Wote wanapaswa kukaribisha kwa imani kile ambacho Bwana anavuvia, wakijua kwamba “kama vile mbingu zilivyo juu ya nchi” (Isa 55:9), njia zake ziko juu sana kuliko njia zetu na mawazo yake juu ya mawazo yetu. Ni kwa njia hiyo tu ndipo Roho ataweza “kufundisha” na “kukumbusha” yale aliyosema Yesu (rej. Yh 14:26), akiyachonga mioyoni mwenu ili mwangwi wake uenee kutoka kwao katika upekee na kutorudiwa kwa kila mpigo wa moyo.
Papa alikazia kusema kuwa, hata hivyo, kuna jambo moja zaidi la kutafakari ambalo ningependa kusisitiza kuhusu kile ambacho Liturujia ya Neno imetupatia leo: thamani ya umoja. Katika somo la kwanza, Mtakatifu Paulo, akizungumzia jumuiya ya Korintho, anatoa maelezo ambayo yanaweza kutumika kwa urahisi kwenye Mkutano Mkuu wenu. Hapa pia, kiukweli, "kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa faida ya wote" ( 1 Kor 12: 7 ), hapa pia "Roho huyo huyo hufanya kazi hizi zote, akiwagawia kila mtu kama apendavyo" (1Kor 12, 11), na kwenu pia inaweza kusemwa kwamba "kama vile mwili ulivyo mmoja, una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili, ingawa ni vingi." Umoja uwe kitu cha lazima kwa juhudi zenu, lakini sio hivyo tu: lazima pia kuwa kigezo cha kutathmini matendo yenu na kufanya kazi pamoja, kwa sababu kile kinachounganisha kinatoka kwake, lakini kinachogawanyika hakiwezi kuwa.
Katika suala hili, Mtakatifu Agostino pia anakuja kutusaidia hapa, akitoa maoni yake juu ya muujiza wa Pentekoste, akibainisha kuwa: "Kama vile lugha tofauti ambazo mtu angeweza kuzungumza zilikuwa ishara ya uwepo wa Roho Mtakatifu, hivyo sasa upendo wa umoja ni ishara ya uwepo wake" (ibid., 3). Na kisha aliendelea: "Kwa maana kama vile watu wa kiroho wanavyofurahi katika umoja, watu wa kimwili daima hutafuta mafarakano.” Kwa hiyo anauliza: "Ni nguvu gani kubwa kuliko uchamungu wa upendo wa umoja?" na kuhitimisha: "Utakuwa na Roho Mtakatifu unapokubali moyo wako kushikamana na umoja kwa njia ya upendo wa kweli"(ibid.).Kwa hiyo Kusikiliza, unyenyekevu, na umoja: haya ni mapendekezo matatu, ambayo ninatumaini ni muhimu, ambapo liturujia inatupatia kwa siku hizi zijazo. Mwaliko ni kufanya kuwa wenu kwa kupyaisha maombi tuliyomweleza Bwana mwanzoni mwa sherehe hii: “Roho, Mwokozi, atokaye kwako, ee Baba, atie nuru nia zetu na, sawa sawa na ahadi ya Mwana wako, atuongoze katika kweli yote” (taz.Misale ya Roma, Votive Mass of the Holy Spirit).