Papa Leo XIV awatangaza Watakatifu wapya,Pier Giorgio na Carlo:Kuishi kwa sala,urafiki na mapendo!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu akiwageukia mamia elfu ya waamini waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro kwa ajili ya tukio la Kanisa la kuwatangaza watakatifu wapya, Dominika tarehe 7 Septemba 2025, alianza kusema kuwa: Wapendwa kaka na dada Katika somo la kwanza, tulisikia swali: "[Bwana,] ni nani angalijua mapenzi yako kama usingetoa hekima na kumtuma Roho wako Mtakatifu kutoka juu?" (Hekima 9:17). Tuliisikia baada ya Wenyeheri vijana wawili, Pier Giorgio Frassati na Carlo Acutis, kutangazwa kuwa watakatifu, na hii ni majaliwa. Kiukweli, swali hili, katika Kitabu cha Hekima, linahusishwa na kijana kama wao: Mfalme Sulemani.
Baada ya kifo cha baba yake Daudi, alitambua kwamba alikuwa na vitu vingi sana: uwezo, mali, afya, ujana, uzuri, na ufalme. Lakini kwa hakika wingi huu mkubwa wa njia ulikuwa umezua swali moyoni mwake: "Nifanye nini ili pasiwepo kitu kinachopotea?" Na alielewa kwamba njia pekee ya kupata jibu ni kumwomba Mungu zawadi kubwa zaidi: Hekima yake, kujua mipango yake na kushikamana nayo kwa uaminifu. Alikuwa ametambua, kwa hakika, kwamba ni kwa njia hii tu kila kitu kingepata nafasi yake katika mpango mkuu wa Bwana. Ndiyo, kwa sababu hatari kubwa maishani ni kuipoteza nje ya mpango wa Mungu. Yesu, pia, katika Injili, anazungumza nasi juu ya mpango ambao lazima tuushike kikamilifu. Anasema: “Yeyote asiyeuchukua Msalaba wake na kunifuata hawezi kuwa mfuasi wangu” ( Lk 14:27 ); na tena: “Yeyote miongoni mwenu asiyeacha vyote alivyo navyo hawezi kuwa mfuasi wangu” (Lk 14, 33).
Baba Mtakatifu aliendelea, yaani, anatuita tujitupe sisi wenyewe bila kusita katika tukio analopendekeza, kwa akili na nguvu zinazotoka kwa Roho Wake na ambazo tunaweza kukumbatia kwa kiwango ambacho tunajivua sisi wenyewe, wa mambo na mawazo ambayo tunashikamana nayo, na kusikiliza neno Lake. Vijana wengi, kwa karne nyingi, wamelazimika kukabiliana na njia panda hii maishani. Fikiria Mtakatifu Fransisko wa Assisi: kama Sulemani, yeye pia alikuwa kijana na tajiri, mwenye kiu ya utukufu na umaarufu. Kwa sababu hii, aliondoka kwenda vitani, akitarajia kuwekezwa kama "amiri jeshi mkuu" na kufunikwa na heshima. Lakini Yesu alimtokea njiani na kumfanya atafakari yale aliyokuwa akifanya.
Akiwa amepona, alimuuliza Mungu swali rahisi: "Bwana, wataka nifanye nini?" Na kutoka hapo, akirudia hatua zake, alianza kuandika historia tofauti: Historia ya ajabu ya utakatifu sisi sote tunaijua, akijivua kila kitu ili kumfuata Bwana (Lk, 14:33), akiishi katika umaskini na kupendelea upendo kwa ndugu zake, hasa walio dhaifu na wadogo zaidi, kuliko dhahabu, fedha, na vitambaa vya thamani vya baba yake. Na ni watakatifu wengine wangapi tungeweza kukumbuka! Wakati mwingine tunawaonyesha kama takwimu kubwa, tukisahau kwamba kwao yote ilianza wakati, bado wachanga, walijibu "ndiyo" kwa Mungu na kujitoa kwake kikamilifu, bila kushikilia chochote.
Mtakatifu Agostino anasimulia, katika suala hili, kwamba katika "fundo la mateso na fundo la maisha yake, sauti, ya ndani kabisa, ilimwambia: "Ninakutaka." Na kwa hivyo Mungu akampa mwelekeo mpya, njia mpya, mantiki mpya, ambayo hakuna chochote cha uwepo wake kilipotea. Katika muktadha huu, leo tunatazamia kwa Mtakatifu Pier Giorgio Frassati na Mtakatifu Carlo Acutis: kijana kutoka mwanzoni mwa karne ya ishirini na kijana wa siku zetu, wote kwa upendo na Yesu na tayari kutoa kila kitu kwa ajili yake.
Pier Giorgio alikutana na Bwana kupitia shule na vikundi vya Kanis, Chama cha Matendo ya Vijana Katoliki, Mkutano wa Mtakatifu Vincent wa Paulo, Shirikisho la Vyuo Vikuu Katoliki Italia (FUCI), na Udugu wa tatu wa Wadominikani na alishuhudia hili kwa furaha yake ya maisha na maisha yake ya Kikristo, kwa njia ya sala, urafiki, na mapendo. Kiasi kwamba, walipomwona akizunguka katika mitaa ya Torino na mikokoteni iliyojaa misaada kwa maskini, marafiki zake walimpatia jina la utani la “Kampuni ya Usafiri wa Frassati.” Hata leo, maisha ya Pier Giorgio yanasimama kama mwanga wa hali ya kiroho ya walei. Kwake yeye, imani haikuwa ibada ya kibinafsi: akiongozwa na nguvu ya Injili na ushirika wake katika mashirika ya Kanisa, alijitolea kwa ukarimu kwa jamii, alichangia maisha ya kisiasa, na alijitolea kwa bidii kuwahudumia maskini.
Papa Leo XIV aliendelea, kwa upande wake Carlo, alikutana na Yesu katika familia yake, shukrani kwa wazazi wake, Andrea na Antonia ambapo hapa leo na ndugu zake wawili, Francesca na Michele—na kisha shuleni, pia, na hasa katika Sakramenti, zinazoadhimishwa katika jumuiya ya parokia. Alikua, kwa hivyo, akijumuisha maombi, michezo, masomo, na upendo katika siku zake kama mtoto na kijana.
Pier Giorgio na Carlo walikuza upendo wao kwa Mungu na kaka na dada zao kwa njia rahisi, zinazoweza kupatikana kwa wote: Misa Takatifu ya kila siku, sala, na hasa Ibada ya Ekaristi. Carlo alisema: "Mbele ya jua, mtu hubadilika rangi. Mbele ya Ekaristi, mtu anakuwa mtakatifu!” na tena: “Huzuni unatazama ndani; furaha inamtazama Mungu. Uongofu si kitu zaidi ya kuhamisha macho ya mtu kutoka chini kwenda juu; mwendo rahisi wa mtazamo unatosha.” Jambo lingine muhimu kwao lilikuwa Kuungama mara kwa mara. Carlo aliandika hivi: “Kitu pekee ambacho tunapaswa kuogopa kiukweli ni dhambi,” na alishangaa kwa nini—kwa maneno yake mwenyewe—“watu wanajali sana uzuri wa miili yao na si uzuri wa nafsi zao.”
Wote wawili, hatimaye, walikuwa na ibada kubwa kwa Watakatifu na kwa Bikira Maria, na kwa ukarimu walifanya mapendo. Pier Giorgio alisema: "Karibu maskini na wagonjwa naona mwanga ambao hatuna." Aliita upendo "msingi wa dini yetu" na, kama Carlo, aliifanya hasa kwa ishara ndogo, thabiti, mara nyingi zilizofichwa, akiishi kile ambacho Papa Francisko aliita "utakatifu wa 'mlango wa karibu'" (Gaudete et Exsultate, 7). Hata ugonjwa ulipowakumba na kukatisha maisha yao ya ujana, hata hili halikuwazuia au kuwazuia kupenda, kujitoa wenyewe kwa Mungu, kumbariki na kujiombea wenyewe na kwa kila mtu.
Siku moja, Pier Giorgio alisema: "Siku nitakayokufa itakuwa siku nzuri zaidi ya maisha yangu." Na kwenye picha ya mwisho, ambayo inamuonesha akipanda mlima katika Bonde la Lanzo, uso wake ulielekea lengo, aliandika: "Kuelekea kwenye urefu." Zaidi ya hayo, hata alipokuwa kijana, Carlo alipenda kusema kwamba Mbingu imetungoja sikuzote, na kwamba kesho yenye upendo inatoa matunda yaliyo bora zaidi leo.
Papa alikazia kufafanua wasifu wao kwamba, Watakatifu Pier Giorgio Frassati na Carlo Acutis ni mwaliko kwetu sote, hasa vijana, tusipoteze maisha yetu, bali tuyaelekeze juu na kuyafanya kuwa kazi bora zaidi. Wanatutia moyo kwa maneno yao: “Si mimi, bali Mungu,” alisema Carlo. Na Pier Giorgio: "Ikiwa una Mungu katikati ya matendo yako yote, basi utafikia mwisho." Hii ndiyo kanuni rahisi lakini yenye kushinda ya utakatifu wao. Na pia ni ushuhuda tunaoitwa kufuata, kufurahia maisha kikamilifu na kukutana na Bwana katika adhimisho la Mbinguni.
Maneno ya Papa Leo XIV kabla Misa Takatitu ya kutangaza Watakatifu
Kabla ya Misa, Papa Leo XIV alisimama mbele ya Jukwaa Kuu la Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro na kuwakaribisha waamini akisema kuwa: “Kaka na dada, leo ni sherehe nzuri kwa Italia yote, kwa Kanisa zima, kwa Ulimwengu mzima! Na kabla ya kuanza kusherehekea adhimisho la kuwatangaza Watakatifu, nilitaka kutoa salamu na neno kwenu nyote, kwa sababu, wakati sherehe hiyo ni nzito sana, pia ni siku ya furaha kubwa! Na hasa nilitaka kuwasalimu vijana wengi waliokuja kwa ajili ya Misa hii Takatifu! Hakika ni baraka kutoka kwa Bwana: ya kuwa pamoja nanyi nyote mliotoka nchi nyingi sana. Kiukweli ni zawadi ya imani ambayo tunataka kushiriki.”
Papa alisisitiza kuwa “Baada ya Misa Takatifu, mkiweza kuwa na subira, ninatumaini kuja na kuwasalimu pale Uwanjani. Na kwa hivyo, mkiwa huko mbali sasa, tutegemee angalau kuweza kusalimiana ...” Aidha Papa Leo XIV aliendelea “Ninawa salimia familia za Wenyeheri wawili ambao karibu watakuwa Watakatifu, wajumbe rasmi, na maaskofu na mapadre wengi ambao wamekuja. Tuwe na shangwe kwa wote, na asante pia kwa kuwa hapa! Wanaume na wanawake watawa, Chama cha Matendo ya vijana wakatoliki.”
Papa Leo aliendelea kwamba “Tunajiandae kwa adhimisho hili la kiliturujia kwa sala, kwa mioyo iliyofunguka, tukitamani kweli kupokea neema hii kutoka kwa Bwana. Na sisi sote tunahisi mioyoni mwetu jambo lile lile ambalo Pier Giorgio na Carlo walipata: upendo huu kwa Yesu Kristo, hasa katika Ekaristi, lakini pia kwa maskini, kwa kaka na dada zetu. Ninyi nyote, sisi sote, tumeitwa kuwa watakatifu. Mungu awabariki! Nawatakia Sherehe ya furaha! Asante kwa kuwa hapa!”