Papa azindua Borgo Laudato si':ni mbegu ya matumaini,inayoweza kuzaa matunda ya haki na amani
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV jioni ya tarehe 5 Septemba 2025 amezindua Mpango wa Borgo Laudato si', wenye hekta 55 za ardhi katika semye ya Bustani kubwa ya Kipapa huko Castel Gandolfo. Borgo inaunganisha roho mbili: Kituo cha Elimu ya Juu cha Laudato si', kilichoanzishwa na Barua mbili za mkono(chirographs) za Papa Francisko na moyo wa elimu wa mpango huo, na mfumo wa kilimo ulioanzishwa juu ya kanuni za ikolojia fungamani. Baada ya kutembelea eneo hilo kubwa sana ndani ya kijani kibichi, kulikuwa na sehemu ya ibada fupi ya neno ambapo katika mahubiri, Baba Mtakatifu Leo alianza kusema kuwa katika Injili ya Mathayo ambayo tumesikia hivi punde, Yesu anatoa mafundisho kadhaa kwa wanafunzi wake. Ningependa kuzingatia mojawapo, ambalo linaonekana linafaa hasa kwa sherehe hii. Anasema: “Waangalieni ndege wa angani... Fikirieni maua ya shambani jinsi yanavyokua” (Mt 6:26, 28). Ni kawaida kwa Bwana wa Nazareti kurejea asili katika mafundisho yake.
Mimea na wanyama mara nyingi hujulikana katika mifano yake. Lakini katika muktadha huu, kuna mwaliko wa wazi wa kutazama na kutafakari uumbaji, vitendo vinavyolenga kuelewa mpango wa asili wa Muumba. Kila kitu kimeagizwa kwa hekima, tangu mwanzo, ili viumbe vyote vichangie katika utimizo wa Ufalme wa Mungu. Kila kiumbe kina jukumu muhimu na maalum katika mpango wake, na kila kimoja ni "jambo jema," kama Kitabu cha Mwanzo kinavyosisitiza( Mwa 1:1-29).Baba Mtakatifu aliendelea kusema kuwa katika andiko hilo hilo la Injili, akirejea ndege na maua, Yesu anawauliza wanafunzi wake maswali mawili: “Je, ninyi si wa thamani kuliko wao? na kisha: "Ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani, ... je! hatawavika ninyi zaidi?"(Mt 6:30). Akiwa anarudia simulizi ya Mwanzo karibu kabisa, Yesu anakazia mahali pa pekee palipohifadhiwa, katika tendo la uumbaji, kwa ajili ya mwanadamu: kiumbe kizuri zaidi, kilichofanywa kwa sura na mfano wa Mungu. Lakini upendeleo huu unakuja na jukumu kubwa: lile la kutunza viumbe vingine vyote, kuheshimu mpango wa Muumba (rej. Mw 2:15).
Utunzaji wa uumbaji, kwa hivyo, unawakilisha wito wa kweli kwa kila mwanadamu, dhamira inayopaswa kutekelezwa ndani ya uumbaji wenyewe, bila kamwe kusahau kwamba sisi ni viumbe kati ya viumbe, na sio waumbaji. Kwa sababu hiyo, Papa ameongeza “ni muhimu, kama mtangulizi wangu alivyoandika, "kurejesha maelewano ya utulivu na uumbaji, kutafakari juu ya mtindo wetu wa maisha na maadili yetu, na kumtafakari Muumba anayeishi kati yetu na katika yote yanayotuzunguka" (Laudato Si', 225).
Mpango wa Borgo Laudato si’ tunaozindua leo hii, ni moja ya mipango ya Kanisa inayolenga kutambua “wito wa kuwa walinzi wa kazi ya mikono ya Mungu” (Laudate Deum, 217): ni kazi yenye changamoto lakini nzuri na ya kuvutia, ambayo ni kipengele cha msingi cha uzoefu wa Kikristo. Borgo Laudato si' ni mbegu ya matumaini, ambayo Papa Francisko ametuachia kama urithi, "mbegu inayoweza kuzaa matunda ya haki na amani."
Papa amesisitiza kuwa “Na itafanya hivyo kwa kubaki mwaminifu kwa mamlaka yake: kuwa kielelezo kinachoonekana cha mawazo, muundo, na matendo, chenye uwezo wa kukuza uwongofu wa ikolojia kupitia elimu na katekesi. Tunachoona leo hii ni mchanganyiko wa uzuri usio wa kawaida, ambapo hali ya kiroho, asili, historia, sanaa, kazi, na teknolojia hutafuta kuishi kwa upatanisho.” Hili hatimaye Papa aliongeza “ ni wazo la "borgo," mahali pa ukaribu na ukaribu wa kuvutia. Na haya yote hayawezi kushindwa kuzungumza nasi juu ya Mungu.”