Papa Leo XIV,kukomesha silaha duniani:Watafua panga zao ziwe majembe na mikuki yao iwe miundu!
Na Agella Rwezaula – Vatican.
Mara baada ya tafakari na Sala ya Malaika wa Bwana, akiwageukia waamini na mahujaji waliounganika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 31 Agosti 2025 Baba Mtakatifu Leo XIV alisema kuwa Wapendwa kaka na dada “Kwa bahati mbaya, vita vya Ukraine vinaendelea kupanda kifo na uharibifu. Hata katika siku za hivi karibuni, milipuko ya mabomu imepiga miji kadhaa, ukiwemo mji mkuu wa Kyiv, na kusababisha wahanga wengi. Ninapyaisha ukaribu wangu kwa watu wa Kiukraine na familia zote zilizojeruhiwa. Ninawasihi kila mtu asikubali kutojali, bali awafikie kwa njia ya maombi na ishara thabiti za upendo.”
Papa Leo XIV aliendelea: “Ninasisitiza kwa nguvu ombi langu la dharura la usitishaji mapigano mara moja na kujitolea kwa dhati kwa mazungumzo. Umefika wakati kwa wale wanaohusika kuachana na mantiki ya silaha na kuanza njia ya mazungumzo na amani, kwa kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa. Sauti ya silaha lazima inyamazishwe, wakati sauti ya udugu na haki lazima ipazwe.”
Papa alikumbusha tukio jingine baya: “Maombi yetu kwa ajili ya waaathiriwa wa tukio la kupigwa risasi wakati wa Misa ya shule katika jimbo la Minnesota nchini Marekani ni pamoja na watoto wengi wanaouawa na kujeruhiwa kila siku duniani kote. Tumuombe Mungu azuie janga la silaha, kubwa kwa ndogo, linaloathiri ulimwengu wetu. Mama yetu Maria, Malkia wa Amani, atusaidie kutimiza unabii wa Isaya: “Watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu” (Isa 2:4).”
Papa Leo XIV alikazia kusema kuwa “Mioyo yetu pia imejeruhiwa na zaidi ya watu hamsini waliofariki na takriban mia moja bado hawajulikani waliko katika ajali ya meli iliyojaa wahamiaji waliokuwa wakijaribu safari ya kilomita 1,100 kwenda Visiwa vya Canary, ambayo ilipinduka kwenye pwani ya Atlantiki ya Mauritania. Msiba huu mbaya unarudiwa kila siku ulimwenguni kote. Tunaomba kwamba Bwana atufundishe, kama watu binafsi na kama jamii, kutii neno lake kikamilifu: “Nilikuwa mgeni nanyi mkanikaribisha” (Mt 25:35). Tunawakabidhi majeruhi wetu wote, waliopotea, na wafu, kila mahali, kwa kumbatio la upendo la Mwokozi wetu.”
Papa akikumbusha tukio la mwezi Septemba alisema: “Septemba 1, ni Siku ya Dunia ya Maombi ya Utunzaji wa kazi ya Uumbaji. Miaka kumi iliyopita, Papa Francisko, kwa makubaliano na Patriaki wa Kiekumeni Bartholomew wa Kwanza, alianzisha Siku hii kwa ajili ya Kanisa Katoliki. Ni muhimu zaidi na ya haraka kuliko wakati mwingine wowote, na mwaka huu mada yake ni: "Mbegu za Amani na Matumaini." Kwa pamoja na Wakristo wote, tunaisherehekea na kuirefusha kote katika "Kipindi cha kazi ya Uumbaji" hadi tarehe 4 Oktoba, katika siku kuu ya Mtakatifu Francis wa Assisi.” Papa aliongeza: “Katika roho ya ‘Wimbo wa Sifa Ndugu Jua’ uliotungwa naye miaka 800 iliyopita, tunamsifu Mungu na kufanya upya ahadi yetu ya kutoharibu zawadi yake bali kutunza nyumba yetu ya kawaida.
Papa aliwageukia waamini na mahujaji waliofika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro kwamba:“ Nawasalimu ninyi nyote, waamini wa Roma na mahujaji kutoka Italia na nchi mbalimbali. Hasa, ninasalimia vikundi vya Parokia ya Quartu Mtakatifu Elena, Morigerati, Venegono, Rezzato, Brescello, Boretto na Gualtieri, Val di Gresta, Valmadrera, Stiatico, Sortino, na Casadio; na kundi la familia kutoka Lucca ambao wamekuja kwenye njia ya Francigena. Pia ninawasalimu Walei, Udugu wa Masista wa Dimesse wa Padua, vijana wa Matendo ya Kikatoliki na AGESCI ya Reggio Calabria, vijana wa Gorla Maggiore, na wanakipamimara wa Castel mtakatifu Pietro Terme; Vile vile Shalom Harakati ya Mtakatifu Miniato na Angiolo ya Bravo Philharmonic, kundi cha chama cha "Note Libere" cha Taviano, na kikundi cha "Wazazi wa Orsenigo." Hatimaye aliwatakia “Dominika njema kwa wote!