Ukaribu wa Papa Leo XIV kwa watu wa Cabo Delgado,Msumbiji
Na Angella Rwezaula -Vatican.
Mara baada ya Tafakari na sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu Leo XIV akiwageukia waamini na mahujaji waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 24 Agosti 2025 alisema: “Ninaelezea ukaribu wangu kwa watu wa Cabo Delgado, Msumbiji, waathiriwa wa hali ya ukosefu wa usalama na ghasia ambayo inaendelea kusababisha vifo na kufukuzwa.” Papa aliongeza kusema “Pamoja na kuwaomba tusiwasahau ndugu zetu hawa, ninawaalika kuwaombea na kuwaeleza matumaini yangu kuwa juhudi za viongozi wa nchi zifanikiwe kurejesha usalama na amani katika eneo hilo.”
Papa alikumbusha wito wake wa hivi karibuni wa kusali kwa ajili ya amani duniani kwamba “ Ijumaa iliyopita, tarehe 22 Agosti, tuliandamana na sala zetu na kufunga kwa ajili ya kaka na dada zetu wanaoteseka kwa sababu ya vita. Leo hii tunaungana na kaka na dada zetu wa Ukraine ambao, kwa mpango wa kiroho “Sala ya Ulimwengu kwa ajili ya Ukraine,” wanamwomba Bwana aipe amani nchi yao inayoteswa.”
Kwa kuhitimisha, na salamu, Papa Leo XIV alisema “Nawasalimu ninyi nyote, waamini wa Roma na mahujaji kutoka nchi mbalimbali, hasa zile za Karaganda, Kazakhstan, Budapest, na jumuiya ya Chuo cha Kipapa cha Amerika Kaskazini.” Papa aliendelea “Nina furaha kuwakaribisha Bendi ya Muziki ya Gozzano na vikundi vya parokia kutoka Bellagio, Vidigulfo, Carbonia, Corlo, na Val Cavallina. Pia ninawasalimu waamini ambao wamefika kwa baiskeli kutoka Rovato na Manerbio, na kikundi cha wasafiri cha Via Lucis. Kwa wote ninawatakia Dominika Njema.”