Ujumbe wa Papa Leo XIV kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 20 wa SECAM, Kigali
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katokiki Afrika na Madagascar, SECAM ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, uliowahamasisha Maaskofu kutoka Barani Afrika kushikamana kwa hali na mali, ili kuweza kukoleza ari na moyo wa kimisionari, tayari kujikita katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. SECAM ikazinduliwa rasmi tarehe 31 Julai 1969 huko Uganda. Mtakatifu Paulo VI alipotembelea kwa mara ya kwanza Bara la Afrika kwa kufanya hija ya kitume nchini Uganda kuanzia tarehe 31 Julai hadi tarehe 2 Agosti 1969 kwanza kabisa: aliitaka familia ya Mungu Barani Afrika kuwa mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo kwa Kristo na Kanisa lake; kujenga na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu Barani Afrika. Alisema, viongozi wa kisiasa Barani Afrika wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa misingi ya haki, amani na maridhiano.
Kanisa kwa kushirikiana na Serikali mbalimbali Barani Afrika zisaidie kukoleza mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kwa: kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu, wanawake Barani Afrika wakipewa kipaumbele cha kwanza! Alilitaka Kanisa kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu, afya, kilimo na huduma bora za maji safi na salama. Katika muktadha huu, Mtakatifu Paulo VI alikazia umuhimu wa majadiliano ya kidini na kiekumene Barani Afrika kama njia ya kukuza na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kidugu. Alikazia pia umuhimu wa kukuza na kuendeleza mashirika na vyama vya kitume ili kusaidia majiundo, malezi na makuzi ya imani, tayari kuchangia katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu! Mtakatifu Paulo VI, katika hija yake ya kitume, aliwataka waamini kuiga mfano bora wa Mashahidi wa Uganda walioyamimina maisha yao kama kielelezo cha ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Akawataka wawe jasiri na thabiti katika imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani. Ujasiri wa imani unawawezesha waamini kumwilisha Neno la Mungu katika maisha na vipaumbele vyao.
Waamini waendelee kuboresha na kupyaisha: matumaini, mapendo na imani yao kwa njia ya Sakramenti za Kanisa na Ibada mbalimbali, ambazo zitawasaidia kuwa kweli ni wafuasi wamisionari wa Kristo Yesu, kwa kuhakikisha kwamba, imani inamwilishwa katika matendo adili na matakatifu. Imani iwasaidie kuonesha upendo kwa Mungu na jirani. Mtakatifu Paulo VI, wakati alipokuwa anazungumza na Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbalimbali za Bara la Afrika, alikazia umoja na mshikamano katika urika wa Maaskofu katika kutekeleza dhamana na wajibu wao wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Ili kukuza na kudumisha maisha ya Kikristo Barani Afrika kwa kutambua kwamba, tangu wakati huu, waafrika wenyewe wanapaswa kuwa ni wamisionari Barani Afrika tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mungu Barani Afrika. Dhamana hii inajikita katika ujenzi wa miundo mbinu ya Kanisa, inayoliwezesha Kanisa kuonenana, chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu. Kanisa kwa asili ni la kimisionari, dhamana inayopaswa kuendelezwa na kudumishwa Barani Afrika.
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katokiki Afrika na Madagascar, SECAM, kuanzia tarehe 28 Julai hadi tarehe 4 Agosti 2025 linaadhimisha Mkutano wake mkuu wa 20 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Kristo Yesu, Chemchemi ya Matumaini, Upatanisho na Amani.” Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na kusoma na Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora, Tanzania, Jumamosi tarehe 2 Agosti 2025, Baba Mtakatifu Leo XIV ameonesha uwepo wake wa karibu kwa wajumbe wa mkutano huu wa SECAM na kwamba, anaunga mkono maamuzi yatakayotolewa na wajumbe wa mkutano huuu unaofanyika Kigali, nchini Rwanda. Baba Mtakatifu Leo XIV anawahamasisha Maaskofu Barani Afrika kujikita kikamilifu katika ujenzi wa Makanisa mahalia na kwamba, Kanisa liwe ni alama wazi inayoshuhudia matumaini ya Kikristo, Umoja na Upatanisho Barani Afrika.
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, majadiliano ya kina, wakati wa maadhimisho ya Mkutano mkuu wa SECAM yatajenga na kuimarisha uzoefu na mang’amuzi ya upendo wa Mungu unaopyaisha matumaini kutoka kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu. Maaskofu Barani Afrika wawe ni vyombo na mashuhuda wa umoja na ushirika na kwamba, wataendelea kukoleza na kuimarisha umoja huu miongoni mwa jamii zilizomeguka na kusambaratika na kwamba, Makanisa mahalia yataendelea kuwa ni alama wazi ya matumaini kwa watu wote wa Mungu Barani Afrika. Baba Mtakatifu Leo XIV amewaweka watu wote wa Mungu chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa matumaini na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume! Wakati huo huo, Rais Paul Kagame wa Rwanda, amekutana na kuzungumza na Kamati kuu ya SECAM na kuwakumbusha kwamba, wale wote wenye dhamana na wajibu wa uongozi ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake kutenda vyema kwa ajili ya ubinadamu. Kushindwa na kufaulu ni sehemu ya ubinadamu, lakini, kamwe watu wasikwamishwe na historia iliyopita, lakini iwasaidie kujifunza, kufanya kazi kwa ushirikiano na hivyo kuandaa mazingira bora zaidi yatakayo saidia kupandikiza: matumaini, upatanisho na amani, si tu nchini Rwanda bali kuzunguka Bara lote la Afrika. Viongozi waliochaguliwa ni Kardinali Fridolin Ambongo, Rais wa SECAM, Askofu Stephen Dami Mamza wa Jimbo Katoliki la Yola, Nigeria; Askofu mkuu José Manuel Imbamba wa Jimbo kuu la Saurimo, Angola pamoja na Askofu Gabriel Edoe Kumordji wa Jimbo Katoliki Keta Akatsi, Ghana ambaye anaendelea kubaki kuwa ni Mtunza Hazina wa SECAM. Makatibu wakuu ni Padre Rafael Simbine Junior; Padre Zéphirin Moube, kutoka Cameroon Katibu mkuu Msaidizi pamoja na Padre Uchechukwu Obodoechina kutoka Nigeria, Katibu mkuu msaidizi.