Papa Leo XIV:Tuoneshe unyenyekevu,kielelezo cha uhuru,Kanisani ni nyumba ya ukarimu daima
Na Angella Rwezaula - Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV akiwageukia umati wa waamini na mahujaji waliofika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 31 Agosti 2025, alidadavua Injili ya Siku ya Dominika ya XXII ya Mwa C. Papa alianza kwa salamu: “Kaka na dada, Dominika Njema! Kuketi pamoja mezani, hasa siku za mapumziko na sherehe, ni ishara ya amani na ushirika katika kila utamaduni. Katika Injili ya Dominika hii (Luka 14:1, 7-14 ) Yesu anaalikwa kwenye chakula cha mchana na mmoja wa viongozi wa Mafarisayo. Kuwa na wageni kunapanua nafasi ya moyo, na kuwa mgeni kunahitaji unyenyekevu ili kuingia katika ulimwengu wa wengine. Utamaduni wa kukutana unalishwa na ishara hizi zinazoleta watu pamoja.”
Baba Mtakatifu aliendelea kusema kuwa “Mkutano sio rahisi kila wakati. Mwinjili anabainisha kwamba wale waliokaa mezani “walikuwa wakimtazama” Yesu, na kwa ujumla Yeye alichukuliwa kwa mashaka fulani na watafsiri wakali zaidi wa mapokeo ya kiutamaduni.” Hata hivyo, Papa Leo alizia kusema “kukutana kunatokea kwa sababu Yesu anakaribia kweli, si nje ya hali hiyo. Kiukweli anakuwa mgeni, kwa heshima na uhalisi. Anaachana na zile tabia njema ambazo ni taratibu tu ili kuepuka kushirikishana. Kwa hivyo, kwa mtindo wake mwenyewe, kwa mfano, anaelezea kile anachokiona na kuwaalika wale wanaomtazama kutafakari. Hakika ameona kuna mbio za kushika nafasi za kwanza. Hii hutokea hata leo, si katika familia, lakini katika matukio wakati kuna fursa muhimu kwa kutaka "kutambuliwa;” kwa hiyo badala ya kuwa pamoja hugeuka kuwa mashindano.”
Kwa upande huo Papa amefafanua kuwa: “Kuketi pamoja kwenye meza ya Ekaristi katika Siku ya Bwana kunamaanisha pia sisi kumwachia Yesu Neno. Kwa hiari anakuwa mgeni wetu na anaweza kutuelezea jinsi anavyotuona. Ni muhimu sana kujiona kupitia macho Yake: kufikiria upya jinsi mara nyingi tunapunguza maisha kuwa mashindano, jinsi tunavyokosa mpangilio ili kupata kutambuliwa, jinsi tunavyojilinganisha sisi kwa sisi bila lazima. Kutulia kutafakari, tukijiruhusu sisi wenyewe kutikiswa na Neno ambalo linatilia shaka vipaumbele vinavyochukua mioyo yetu: ni uzoefu wa uhuru. Yesu anatuita kwa uhuru.”
Baba Mtakatifu alisema kuwa: “Katika Injili, anatumia neno "unyenyekevu" kuelezea aina kamili ya uhuru (ona Luka 14:11). Unyenyekevu, kwa kweli, ni uhuru kutoka kwa mtu mwenyewe. Inatokea wakati Ufalme wa Mungu na haki yake vimeteka shauku yetu kikweli na tunaweza kujiruhusu kutazama mbele sana: si kwenye ncha ya vidole vya miguu yetu, bali mbele sana! Wale wanaojikweza kwa ujumla hawajapata chochote cha kuvutia zaidi wao wenyewe,na hatimaye wanakuwa wa kutojiamini kidogo. Walakini wale ambao wameelewa jinsi walivyo wa thamani machoni pa Mungu, wale wanaojihisi kwa kina kuwa wao ni wana au binti za Mungu, wana mambo makubwa zaidi ya kujivunia na kuwa na hadhi inayong'aa kutoka ndani. Inakuja mbele, inashikilia nafasi ya kwanza, bila kujitahidi na bila mikakati, wakati, badala ya kutumia hali, tunajifunza kutumikia.
Kwa kuhitimisha Papa alisema kuwa: “Leo tuombe kwamba Kanisa liwe uwanja wa mafunzo kwa ajili ya unyenyekevu kwa wote, yaani, nyumba ambayo tunakaribishwa daima, mahali ambapo nafasi hazipatikani kwa kushindaniwa na ambapo Yesu bado anaweza kusema na kutufundisha unyenyekevu wake na uhuru wake. Maria, ambaye tunamwomba sasa, ndiye Mama wa nyumba hii kweli.”