Papa Leo XIV:Kama Waagostinian tuwe wapatanishi katika familia,maeneo yetu&kutambua uwepo wa Mungu kati yetu
Na Angella Rwezaula - Vatican.
Katika fursa ya kutumtunikia Nishani ya Mtakatifu Agostino, kutoka Provinsi ya Mtakatifu Thomas wa Villanova nchini Marekani, kwa baba Mtakatifu Leo XIV, ambayo hapo awali ilikusudiwa kwa ajili ya aliye kuwa Kardinali Prevost, ndugu yao, hatimaye iliwasilishwa kama Papa na ambaye alituma ujumbe wa video uliorekodiwa huko Castel Gandolfo. Video hiyo ilioneshwa wakati wa hafla ya jioni huko Philadelphia, iliyohudhuriwa na takriban wageni 700. Kwa njia hiyo makofi ya kishindo, pamoja na kelele za mshangao, zilisikika katika jumba la kifahari katikati mwa jiji la Philadelphia, Pennsylvania, Marekani, wakati wa kuonesha ujumbe wa video kwenye skrini ambayo Papa Leo XIV alianza na salamu za jioni na kwamba na baraka za Mungu ziwe kwenu nyote mnaoshiriki katika tukio hili la ajabu.
Katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Baba yetu Mtakatifu, Mtakatifu Agostino, nimenyenyekea na kuheshimiwa kupokea Nishani ya Mtakatifu Augustino kutoka Provinsi ya Mtakatifu Thomas wa Villanova. Ninaporekodi ujumbe huu, niko mbali na joto la Kirumi, nikitumia muda huko Castel Gandolfo kwa maombi, kutafakari na kupumzika. Mtafurahi kujua kwamba Kanisa la Parokia katika mji huu nje ya Roma, limepewa jina la Mtakatifu Thomas wa Villanova, anayejulikana kama Baba wa maskini, Padre wa Waagostinian mwenye kipawa cha ajabu na Askofu ambaye alijitolea maisha yake katika huduma kwa maskini.
Papa Leo alisema kuwa “Kama Waagostinian, tunajitahidi kila siku kuishi kulingana na mfano wa Baba yetu wa kiroho, Mtakatifu Agostino. Kutambuliwa kama Waagostinian, ni heshima inayozingatiwa sana. Ni jinsi gani nilivyo, na deni kwa roho na mafundisho ya Mtakatifu Agostino na ninawashukuru ninyi nyote kwa njia nyingi maisha yenu yanaonyesha kujitolea kwa kina kwa maadili ya veritas, unitas, caritas(ukweli,umoja,upendo). Papa Leo XIV aliendelea: “Mtakatifu Agostino, kama mnavyojua, alikuwa mmoja wa waanzilishi wakuu wa utawa; askofu, Mtaalimungu, Mhubiri, Mwandishi, na Mwalimu wa Kanisa.
Lakini hii haikutokea mara moja. Maisha yake yalikuwa yamejaa majaribio mengi na makosa, kama maisha yetu wenyewe. Lakini kwa neema ya Mungu, kwa maombi ya mama yake Monica, na Jumuiya ya watu wema waliomzunguka, Agostino aliweza kupata njia ya amani kwa moyo wake usiotulia. Maisha ya Mtakatifu Augustino na wito wake kwa uongozi wa watumishi, yanatukumbusha kwamba sisi sote tumepewa na Mungu karama na kusudi, utimilifu na furaha yetu huja kwa kuzirudisha katika huduma ya upendo kwa Mungu na kwa jirani.
Askofu wa Roma alisisitiza: “Lazima kuwa nanyi nyote usiku wa leo, mnapokusanyika huko Philadelphia ya kihistoria na nyumbani kwa Kanisa la Mtakatifu Agostine, mojawapo ya jumuiya kongwe za kidini nchini Marekani. Tunasimama juu ya mabega ya mapadre wa kiagostinian, kama vile Padre Matthew Carr na Padre John Rossiter, ambao roho yao ya kimisionari iliwaongoza mwishoni mwa miaka ya 1700 kwenda kupeleka habari njema ya Injili katika huduma kwa wahamiaji wa Ireland na Ujerumani, wakitafuta maisha bora na uvumilivu wa kidini. Hadi leo hii, tumeitwa kuendeleza urithi huu wa huduma ya upendo kwa watu wote wa Mungu. Yesu anatukumbusha katika Injili kuwapenda jirani zetu, na hii inatupatia changamoto sasa kuliko wakati mwingine wowote kukumbuka kuwaona jirani zetu leo ??kwa mtazamo wa Kristo: kwamba sisi sote tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu kwa njia ya urafiki, uhusiano, mazungumzo na kuheshimiana. Tunaweza kuona zaidi ya tofauti zetu na kugundua utambulisho wetu wa kweli kama dada na kaka katika Kristo.”
Papa Leo XIV alisisitiza: “Kama Jumuiya ya waamini na kuhamasishwa na karama ya Waagostinian, tunaalikwa kwenda kuwa wapatanishi katika familia na vitongoji vyetu na kutambua kweli uwepo wa Mungu kati yetu. Amani huanza na kile tunachosema na kutenda na jinsi tunavyosema na kutenda. Papa Leo XIV alisisitiza kuwa “Mtakatifu Augustino anatukumbusha kwamba kabla ya kuzungumza, ni lazima kwanza tusikilize, na kama Kanisa la Sinodi, tunahimizwa kujihusisha tena na sanaa ya kusikiliza kwa njia ya sala, kwa ukimya, utambuzi na tafakari. Tunayo nafasi na wajibu wa kumsikiliza Roho Mtakatifu; kusikiliza kila mmoja; kusikiliza sauti za maskini na wale walio pembezoni ambao sauti zao zinahitaji kusikilizwa. “ Mtakatifu Augustino anatuhimiza kuwa makini na kumsikiliza mwalimu wa ndani, sauti isemayo kutoka ndani yetu sote. Ni ndani ya mioyo yetu ambapo Mungu anazungumza nasi. Katika moja ya mahubiri yake, Mtakatifu Agostino aliwatia moyo wasikilizaji wake: “Msiwe na mioyo yenu masikioni, bali masikio yenu ndani ya mioyo yenu”.
Tunahitaji kufanya nini ili kujizoeza jinsi ya kusikiliza kwa masikio ya mioyo yetu? Ulimwengu umejaa kelele, na vichwa na mioyo yetu inaweza kujazwa na aina nyingi tofauti za jumbe. Jumbe hizi zinaweza kuchochea kutotulia kwetu na kuiba furaha yetu.” Kama jumuiya ya imani, tukijitahidi kujenga uhusiano na Bwana, na tujitahidi kuchuja kelele, sauti za migawanyiko katika vichwa na mioyo yetu, na tujifungue kwa mialiko ya kila siku ya kumjua Mungu na upendo wa Mungu zaidi. Tunaposikia sauti hiyo ya upendo na ya kutia moyo ya Bwana, tunaweza kuishirikisha kwa Ulimwengu tunapojitahidi kuwa wamoja ndani yake.
Baba Mtakatifu Leo XIV alitoa shukrani kwamba: “Ninashukuru kwa heshima hii na hasa kwa msaada wa Misa na maombi yaliyoadhimishwa jioni hii na zaidi ninapojitahidi kuhudumu kwa unyenyekevu. Tafadhali muendelee kuniombea, kwa nia ya watu wote wa Mungu duniani kote. Muwe na uhakika wa maombi yangu kwa ninyi nyote mliokusanyika hapo usiku wa leo: kwa ndugu zangu wa Waagostinian, wamisionari wenzangu wa Villanova, wa zamani, wa sasa na wa siku zijazo, kwa wazee na vijana, matajiri na maskini, kwa marafiki zetu wote wapendwa wa Shirika. Kama Waagostinian tunakuja pamoja na nyakati zetu za wasiwasi, giza na mashaka na kama Agostino, kupitia neema ya Mungu, tunaweza kugundua kwamba upendo wa Mungu ni uponyaji kweli. Tujitahidi kujenga jumuiya ambapo upendo huo unaonekana.”
Na tuendelee kuimarisha utume wetu kama Kanisa na jumuiya ili kukuza amani, kuishi kwa matumaini, na kuakisi nuru na upendo wa Mungu ulimwenguni. Ni katika umoja wetu katika Kristo na ushirika sisi kwa sisi ndipo nuru itakua pamoja na kung'aa zaidi katika ulimwengu wetu. Chini ya maongozi na ulinzi wa Bikira Maria, Mama yetu wa Shauri Jema, tusisahau kamwe karama alizotupatia kwa imani iliyojaa ndiyo, aliyoitoa akikubali kile ambacho Mungu alimpangia. Mungu awabariki ninyi nyote na alete amani mioyoni mwenu isiyotulia, na awasaidie kuendelea kujenga jumuiya ya upendo, mmoja katika nia na moyo, inayomkusudia Mungu. Na Baraka ya Mwenyezi Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu iwafikie ninyi nyote na kukaa nanyi milele. Asanteni sana,” Baba Mtakatifu Leo XIV alihitimisha
Padre Robert P. Hagan, Mkuu wa Provinsi alimkabidhi Medali
Wakati huo, Padre Robert P. Hanga, Mkuu wa Provinsi alimkabidhi Nishani hiyo. Wakati wa kumtunukia alisema kwamba: "Baba Mtakatifu Papa Leo, kwa niaba ya Provinci ya Mtakatifu Thomas wa Villanova, Jumuiya kubwa zaidi ya Waagostinian, ina waamini wengi wa imani. Tunasema asante kwa kukubali heshima hii ya Medali ya Mtakatifu Agostino kwa uongozi wako wa huduma, kujitolea kwako kwa maisha yote maskini, ushuhuda wako kwa maadili ya Agostino, na sasa kama Mchungaji wetu wa Ulimwengu wote kwa mfano ambao umetuwekea sisi sote kukua karibu na Bwana na jirani, na kwamba sote tunaweza kuwa wapatanishi wa amani. Uwe na uhakika wa maombi yetu kwa ajili yako, kwa ajili ya neema yako na nguvu zako unapoendelea kubeba jukumu hili kwa ajili yetu sote. Mungu akubariki." Ikumbukwe Provisni ya Mtakatifu Thomas wa Villanova ni moja kati ya Pronvinsi tatu nchini Marekani inayozunguka nusu ya mashariki, kwa ajili ya kutunukiwa nishani ya Mtakatifu Augustino. Huu ni utambuzi, lakini pia ni ishara, na juu ya yote, heshima kuu ya Pronvinsi inayotolewa kila mwaka kwa watu ambao, kama ilivyoonyeshwa kwenye nukuu wamejipambanua katika hali ya juu ya utumishi wao.