杏MAP导航

Tafuta

Papa Leo XIV:tumaini la Kikristo si kukwepa ni uamuzi.Uhai utolewao kwa upendo hauwezi kuondolewa na mtu

Yesu anapojibu,“Ndiye Mimi”askari hao walianguka chini.Hiki ni kifungu cha ajabu,kwani usemi huu, katika ufunuo wa kibiblia,unakumbusha jina lenyewe la Mungu:"Mimi ndiye."Yesu anafunua kwamba uwepo wa Mungu unadhihirika hasa ambapo wanadamu hupitia ukosefu wa haki,woga, na upweke.Hapo ndipo nuru ya kweli iko tayari kuangaza bila woga wa kugubikwa na giza linalosonga mbele.Ni tafakari ya Katekesi ya Papa kwa waamini wapatao 1500,Agosti 27.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika mzunguko wa Katekesi wa Jubilei  2025: Yesu Kristo Tumaini letu. Mwendelezo wa Pasaka ya Yesu, Baba Mtakatifu Leo XIV amejikita na mada ya kujisalimisha kwa swali: “ Je mnamtafuta nani Yh 18,4). Awali ya yote ilisomwa Injili “Ndipo Yesu, akijua yote yatakayompata, akatokea, akawaambia, Mnamtafuta nani? Wakamjibu, "Yesu wa Nazareti." Yesu akawaambia, "Ndiye Mimi!" Yuda, msaliti wake, alikuwa pamoja nao. Alipowaambia, “Ndiye Mimi,” wakarudi nyuma na kuanguka chini. Akawauliza tena, Mnamtafuta nani? Wakajibu, “Yesu wa Nazareti.” Yesu akajibu, "Nimewaambia ya kwamba Ni mimi ; basi ikiwa mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao." Hii ilikuwa ili litimie neno alilosema: “Katika wale ulionipa sikumpoteza hata mmoja.”(Rej Yhn 18,4-7).

Katekesi ya Papa Agosti 27
Katekesi ya Papa Agosti 27   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu akiwageukia waamini na mahujaji wapatao 15,000 katika Ukumbi wa Paulo VI, Basilika ya Mtakatifu Petro, na Ua la Petrine, alisema “Wapendwa Kaka na dada , leo hii tunaakisi tukio linaloashiria mwanzo wa Mateso ya Yesu: wakati wa kukamatwa kwake katika bustani ya Mizeituni. Mwinjili Yohane, pamoja na kina chake cha kiutamaduni, haoneshi Yesu mwenye hofu, anayekimbia au kujificha. Badala yake, anatuonesha mtu aliye huru, ambaye anasonga mbele na kunena, akikabiliana ana kwa ana na saa ambapo nuru ya upendo mkuu zaidi inaweza kufunuliwa. “Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akaja, akawaambia, Mnamtafuta nani?’” (Yh 18:4). Yesu anajua. Walakini, anaamua kutorudi nyuma. Anajisalimisha. Sio kwa udhaifu, lakini kwa upendo. Upendo uliojaa sana, uliokomaa sana kiasi  kwamba haogopi kukataliwa. Yesu hatekwi: anajiacha atekwe. Yeye sio mwathirika wa kukamatwa, lakini muhusika  wa zawadi.

Baba Mtakatifu aliendelea kusema kuwa “Ishara hii inajumuisha tumaini la wokovu kwa wanadamu wetu: tukijua kwamba, hata katika saa ya giza zaidi, tunaweza kubaki huru kupenda kwa ukamilifu. Yesu anapojibu, “Ndiye Mimi” askari hao walianguka chini. Hiki ni kifungu cha ajabu, kwani usemi huu, katika ufunuo wa kibiblia, unakumbusha jina lenyewe la Mungu: "Mimi ndiye." Yesu anafunua kwamba uwepo wa Mungu unadhihirika hasa ambapo wanadamu hupitia ukosefu wa haki, woga, na upweke. Hapo ndipo nuru ya kweli iko tayari kuangaza bila woga wa kugubikwa na giza linalosonga mbele. Katika moyo wa usiku, wakati kila kitu kinaonekana kuporomoka, Yesu anaonesha kwamba tumaini la Kikristo si kukwepa, bali ni uamuzi. Mtazamo huu ni tunda la sala ya kina ambayo hatuombi Mungu atuepushe na mateso, bali tuwe na nguvu ya kudumu katika upendo, tukijua kwamba uhai unaotolewa kwa ajili ya upendo kwa uhuru hauwezi kuondolewa kutoka kwetu na mtu yeyote. “Kama mwanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao” (Yh 18:8). Wakati wa kukamatwa kwake, Yesu hakujali kujiokoa mwenyewe: alitamani tu kwamba marafiki zake waende huru. Hii inaonesha kwamba sadaka yake ni tendo la kweli la upendo.

Katekesi ya Papa Agosti 27
Katekesi ya Papa Agosti 27   (@Vatican Media)

Yesu anajiruhusu kukamatwa na kufungwa na walinzi ili  waweze tu  kuwaweka huru wanafunzi wake. Yesu aliishi kila siku ya maisha yake akijitayarisha kwa ajili ya saa hii ya ajabu na ya kushangaza. Kwa hiyo, inapofika, ana nguvu ya kutotafuta kutoroka. Moyo wake unajua vizuri kwamba kupoteza maisha kwa ajili ya upendo sio kushindwa, lakini kuna kuzaa kwa ajabu. Kama punje ya ngano, ikianguka chini, haiachwi peke yake, bali inakufa na kuzaa. Yesu, pia, anatatizwa tu na njia inayoelekea kwenye kifo na mwisho. Lakini anasadiki vile vile kwamba ni maisha tu yaliyopotea kwa ajili ya mapendo  hatimaye yanapatikana. Hapa ndipo panapo tumaini la kweli: si katika kujaribu kuepuka maumivu, bali katika kuamini kwamba, hata ndani ya moyo wa mateso yasiyo ya haki, mbegu ya maisha mapya imefichwa. Na sisi je? Ni mara ngapi tunatetea maisha yetu, mipango yetu, uhakika wetu, bila kujua kwamba, kwa kufanya hivyo, tunabaki peke yetu? Mantiki ya Injili ni tofauti: ni kile tu kinachotolewa hustawi; upendo tu ambao unakuwa wa bure unaweza kurejesha uaminifu hata pale ambapo yote yanaonekana kupotea.

Katekesi ya Papa Agosti 27
Katekesi ya Papa Agosti 27   (@Vatican Media)

Injili ya Marko pia inatuambia kuhusu kijana ambaye, Yesu anapokamatwa, anakimbia uchi (Mk 14:51). Ni taswira ya fumbo lakini yenye kusisimua sana. Sisi pia, katika majaribio yetu ya kumfuata Yesu, tunapitia nyakati ambazo tunashikwa na tahadhari na kuvuliwa uhakika wetu. Hizi ndizo nyakati ngumu zaidi, tunapojaribiwa kuacha njia ya Injili kwa sababu upendo unaonekana kuwa safari isiyowezekana. Na bado, ni kijana hasa, mwishoni mwa Injili, ambaye anatangaza ufufuko kwa wanawake, si uchi tena, lakini amevaa vazi jeupe. Hili ndilo tumaini la imani yetu: dhambi zetu na kusitasita kwetu hakumzuii Mungu kutusamehe na kurejesha hamu yetu ya kuanza tena kufuata, kutuwezesha kutoa maisha yetu kwa ajili ya wengine. Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu amesema kuwa sisi pia tujifunze kujisalimisha wenyewe kwa mapenzi mema ya Baba, tukiruhusu maisha yetu kuwa mwitikio wa mema tuliyopokea. Katika maisha, hatuhitaji kuwa na kila kitu chini ya udhibiti. Tunachohitaji kufanya ni kuchagua kupenda kwa uhuru kila siku. Hili ndilo tumaini la kweli: tukijua kwamba, hata katika giza la majaribu, upendo wa Mungu hututegemeza na kuzaa matunda ya uzima wa milele ndani yetu,”alihitimisha.

Katekesi ya Papa, Agosti 27
Katekesi ya Papa, Agosti 27   (@Vatican Media)
Katekesi ya Papa 27 Agosti 2025
27 Agosti 2025, 17:03