杏MAP导航

Tafuta

Papa Leo kwa washiriki wa Kongamano la Mtandao Katoliki Afrika:kutembea pamoja kama familia

Papa Leo XIV akihutubia Kongamano la Tatu la Mtandao Katoliki wa Taalimungu na Kichungaji,Barani Afrika,alisisitiza umuhimu wa matumaini katika safari hapa duniani na kuwataka washiriki wote kutazama mustakabali wa bara hilo kwa matumaini.Aliwatia moyo waendelee kuijenga familia ya Makanisa mahalia katika nchi na maeneo yao mbalimbali,ili kuwe na mitandao ya msaada inayopatikana kwa kaka na dada zetu wote katika Kristo,pia kwa jamii iliyo pana zaidi.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika hafla ya Kongamano la Tatu la Mtandao wa Kikatoliki wa Taalimungu na Kichungaji wa Pan-African(PACTPAN), yaani Baraani Afrika Baba Mtakatifu Leo XIV alituma ujumbe kwa njia ya video, akielezea shukrani zake kwa kazi kubwa ya mtandao huo na kuendeleza maombi yake kwa kila mtu aliyekusanyika kutafakari mustakabali wa Kanisa Barani Afrika. Ujumbe huo wa tarehe 5 Agosti 2025, Papa alianza kusem,  “Ninatuma salamu  kwenu ninyi nyote mnaoshiriki katika Kongamano la tatu la Kikatoliki Barani Afrika  kuhusu Taalimungu, Jamii na Maisha ya Kichungaji. Ninawashukuruwaandaaji kwa kazi  kubwa ya kuandaa mkutano huu muhimu. Pia ninatoa maombi yangu kwa maaskofu, wataalimungu, viongozi wa kichungaji, vijana na waamini walei wote waliokusanyika kutafakari mustakabali wa Kanisa Barani Afrika."

Kama sehemu ya Jubilei 2025, tunasherehekea fadhila ya kitaalimungu

Papa Leo alisema kuwa "Miaka mitatu iliyopita, katika hafla ya Kongamano la pili, Papa Francisko alizungumzia umuhimu wa imani. Sasa, kama sehemu ya Jubilei ya mwaka huu, tunasherehekea fadhila nyingine ya kitaalimungu: matumaini. Labda wakati fulani umuhimu zaidi unatolewa kwa fadhila za imani na mapendo; hata hivyo, tumaini lina fungu muhimu katika safari yetu ya kidunia. Hakika, inaweza kuonekana kama fadhila inayounganisha hizo mbili.  Kwa maana moja, imani na taalimungu hutoa msingi wa kumjua Mungu, wakati upendo ni maisha ya upendo tunayofurahia pamoja naye. Hata hivyo, ni kwa nguvu ya matumaini kwamba tunatamani kupata utimilifu wa furaha hii Mbinguni. Hivyo, inatutia moyo na kututegemeza ili tumkaribie Mungu hata tunapokabili ugumu wa maisha."

Afrika inakabiliwa na shida zake maalum

Papa Leo XIV alisisitiza kuwa kama wanavyojua, Afrika, kama kila sehemu nyingine ya ulimwengu, inakabiliwa na shida zake maalum. Wanapokabiliwa na changamoto hizo na mtazamo kwamba mambo hayabadiliki, ni rahisi kukata tamaa. Hata hivyo, ni jukumu hasa la Kanisa kuwa nuru ya ulimwengu na mji uliowekwa juu ya mlima, ili kuwa mwanga wa matumaini kwa mataifa. Kuhusiana na hili, mada ya Kongamano lako ni muhimu hasa: “Kusafiri pamoja kwa matumaini kama Familia ya Kanisa la Mungu Barani Afrika.” Ingawa kila mmoja wetu ameitwa kusitawisha uhusiano wetu binafsi na Mungu, wakati huo huo, kupitia ubatizo wetu tunaunganishwa kama wana na mabinti wa Baba yetu wa Mbinguni.  Kwa hiyo, tuna wajibu fulani wa kuangaliana. Kiukweli, kwa kawaida familia ndiyo mahali pa kwanza ambapo tunapokea upendo na utegemezo tunaohitaji ili kusonga mbele na kushinda majaribu tunayokabili maishani.

Papa anawatia moyo kujenga familia ya makanisa mahalia na mitandao ya msaada

Kwa sababu hiyo, Papa Leo XIV anawatia moyo waendelee kuijenga familia ya Makanisa mahalia katika nchi na maeneo yao mbalimbali, ili kuwe na mitandao ya msaada inayopatikana kwa kaka na dada zetu wote katika Kristo, na pia kwa jamii pana zaidi, hasa wale walio pembezoni. Hatimaye, Papa Leo alipenda  kusisitiza umuhimu wa kuona umoja kati ya taalimungu na kazi ya kichungaji. Tunapaswa kuishi kile tunachoamini. Kristo alituambia kwamba hakuja tu kutupa uhai bali kuutoa kwa ukamilifu. Kwa hivyo, ni kazi yako kufanya kazi pamoja kutekeleza programu za kichungaji zinazoonyesha jinsi mafundisho ya Kanisa yanavyosaidia kufungua mioyo na akili za watu kwa ukweli na upendo wa Mungu. Papa aliwapongeza kwa kazi yao na kwa maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa, ili aweze kuwaongoza na kuhamasisha juhudi zao. “Na baraka za Mwenyezi Mungu, Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu ziwashukie na kukaa nanyi milele. Amina.”

Papa leo XIV atuma ujumbe kwa Mtanado katoliki Barani Afrika
06 Agosti 2025, 10:20