杏MAP导航

Tafuta

Picha hii  inabeba ujumbe mzito wa utume wa Papa Leo XIV ameketi chini pembeni ya mtoto mdogo msichana aliyekuwa kwenye Kambi ya Kipindi cha Kiangazi ya Watoto wa wafanyakazi wa Vatican, Picha hii inabeba ujumbe mzito wa utume wa Papa Leo XIV ameketi chini pembeni ya mtoto mdogo msichana aliyekuwa kwenye Kambi ya Kipindi cha Kiangazi ya Watoto wa wafanyakazi wa Vatican, 

Papa Leo XIV: Unyenyekevu wa Watoto ni Mfano Bora wa Kuigwa!

Wote wawili wanatabasamu, Papa anamwangalia mpiga picha, lakini mtoto kumwangalia Papa kwa macho ya furaha. Kwa nini picha hii ni muhimu? Kwa sababu kushuka chini ni alama ya unyenyekevu wa Baba Mtakatifu Leo XIV akionesha njia ya kufuata, hasa kwa wale wenye madaraka ya kuongoza dunia: kushuka na kujinyenyekesha na hivyo kuwa sawa na watoto, kuuangalia ulimwengu kwa macho ya watoto.. Unyenyekevu wa watoto wadogo ni mfano bora wa kuigwa!

Na Sarah Pelaji, -Vatican

Imepita miezi kadhaa tangu kuchaguliwa kwa Kardinali Robert Francis Prevost kuwa Papa na tayari picha nyingi zenye ujumbe wa kina zimeanza kuchora sura ya Upapa huu mpya wa Leone XIV. Miongoni mwa picha hizo, ijapokuwa haijajulikana na kusambaa sana, ni ile ya Papa Leo XIV akipiga magoti na kuketi chini karibu na msichana mdogo aliyemtaka ampe mchoro wake. Ni kitendo rahisi, lakini chenye ujumbe mzito unaoikumbusha dunia kuwa, ili kujenga dunia bora, lazima tushuke, tujinyenyekeshe na kuwa kama watoto. Katika kipindi kifupi hiki cha Upapa wa Leo XIV, zimekuwepo picha nyingi zilizojaa maana nzuri ya upapa wake huku baadhi zikiendelea kubaki kwenye kumbukumbu ya muda mrefu, kama vile machozi aliyoyazuia hadharani siku ya tarehe 8 Mei 2025 alipochaguliwa na Baraza la Makardinali kuwa mrithi wa Kiti cha Khalifa wa Mtakatifu Petro kisha akatoka hadharani katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuwabariki waamini na watu wenye mapenzi mema waliokuwepo uwanjani hapo. Alipowaangalia   waamini hao kwa furaha siku hiyo alizuia machozi ya upendo, kujisadaka kwa utume alipotoa Salam na Baraka zake za kwanza kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi.”

Papa Leo XIV: malezi na makuzi ya watoto ni muhimu sana.
Papa Leo XIV: malezi na makuzi ya watoto ni muhimu sana.   (ANSA)

Hata hivyo hivi karibuni kuna picha moja ambayo haijasambaa na kutambulika sana lakini inabeba ujumbe mzito wa utume wa Papa Leo XIV ambapo picha hiyo inamwonesha Papa Leo XIV akiwa ameketi chini pembeni ya mtoto mdogo msichana aliyekuwa kwenye Kambi ya Kipindi cha Kiangazi ya Watoto wa wafanyakazi wa Vatican, akimwonesha Papa Leo XIV mchoro wake. Wote wawili wanatabasamu, Papa anamwangalia mpiga picha, lakini mtoto kumwangalia Papa kwa macho ya furaha. Kwa nini picha hii ni muhimu? Kwa sababu kushuka chini ni alama ya unyenyekevu wa Baba Mtakatifu Leo XIV akionesha njia ya kufuata, hasa kwa wale wenye madaraka ya kuongoza dunia: kushuka na kujinyenyekesha na hivyo kuwa sawa na watoto, kuuangalia ulimwengu kwa macho ya watoto. Ni nini kingetokea kama kila mmoja wetu angekuwa na ujasiri wa kushuka, kama Yesu alivyofanya alipowakemea wanafunzi waliotaka kuwafukuza watoto kwa kuwaona “kero”? Ndipo akasema, ‘Waacheni watoto waje kwangu.’

Papa Leo XIV: Unyenyekevu wa watoto ni muhimu
Papa Leo XIV: Unyenyekevu wa watoto ni muhimu   (ANSA)

Jambo hilo pia linatafakarisha ulimwengu katika kina cha maswali mbalimbali ikiwemo; Je, leo hii tunawaachia watoto waje kwetu? Na zaidi, Je, sisi tunaenda kwao? Tunaenda kwa wale watoto wanaokumbwa na vita, wale wanaoteseka kwa sababu ya ubinafsi na uchoyo wa watu wazima; wale wanaodhulumiwa na kuteswa kwa mifumo mbalimbali ya ukatili na nyanyaso. Mantiki na moyo vinadai kwamba, wakubwa wawalinde wadogo lakini kinyume chake ndicho hutokea katika vita vinavyoamuliwa na watu wazima ambapo waathirika wa kwanza wanakuwa ni watoto. Je, tungekosa nini sisi kama wanajamii wakiwemo viongozi wa kimataifa tukishuka hadi kiwango cha watoto wa Gaza, Kharkiv, Goma na maeneo mengine mengi yanayoteseka kutokana na migogoro ya silaha? Labda, tukifanya hivyo, kitu kingebadilika.

Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wangekuwa na unyenyekevu kama watoto...
Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wangekuwa na unyenyekevu kama watoto...   (AFP or licensors)

Mohandas Karamchand Gandhi alisema: “Ikiwa tunataka kufundisha amani ya kweli katika dunia hii na iwapo tunataka kupigana vita dhidi ya vita lazima tuanze na watoto.” Hebu tuseme kwa mfano, kama katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wangeketi watoto kutoka Mataifa yenye nguvu duniani. Je, hali ya siasa za Kimataifa isingebadilika? Kwa masikitiko, tunapaswa kukubali kuwa sumu ya vita tunaipokea tangu utotoni. Bertolt Brecht alielezea kwa uchungu hali hiyo kwenye shairi lake alipokuwa akishuhudia kuibuka kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia: ‘Watoto hucheza michezo ya kivita. Hawawezi kuigiza michezo ya amani kwa kuwa watu wazima daima hufanya vita. Ndiyo maana, labda njia pekee ya kubadili historia ni hii ambayo kwa wengi huonekana kama haiwezekani: kushuka, kuacha kiburi chetu cha watu wazima na kuweka macho (na zaidi mioyo yetu) katika kiwango cha chini cha watoto. Papa Leo XIV akiwa kama mmisionari na Askofu huko Peru, mara nyingi amekuwa akiketi chini kwa ajili ya watoto. Picha nyingi zinathibitisha hilo. Na sasa akiwa kama Khalifa wa Mtakatifu Petro mtindo wake wa maisha ya unyenyekevu haujabadilika, kama picha ya hivi karibuni kabisa katika Kituo cha Kiangazi cha Vatican ndani ya Ukumbi wa Paulo VI inavyoonesha. Picha ya Papa Leo XIV na mtoto inatufundisha kuwa, kujinyenyekesha ni lazima ili kukuza utu, heshima, haki na ubinadamu wetu. Somo ambalo kwa sasa tunalihitaji kwa dhati kwenye ulimwengu huu uliojawa na mahangaiko, mipasuko ya kivita kutokana na uchu wa mali na madaraka.

Papa LEO XIV: Fadhila ya Unyenyekevu
12 Agosti 2025, 10:00