Papa Leo XIV Ujumbe Kumbukizi Miaka 80 ya Mashambulizi ya Hiroshima na Nagasaki
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ilikuwa ni majira ya saa mbili na robo asubuhi kwa saa za Japan, tarehe 6 Agosti 1945, miaka 80 iliyopita, ndege ya kijeshi ya Marekani chapa “B-29 Enola Gay” ilipodondosha bomu la nyuklia na kuwauwa hapo hapo watu 140,000 kati ya wenyeji wapatao 350,000 wa mji wa Hiroshima, nchini Japan. Takribani saa sita mchana ya tarehe 9 Agosti 1945, bomu la nyuklia liliangushwa tena na Marekani kwenye mji wa Nagasaki na wingu zito lilienea mjini humo na huo ukawa ni mwanzo wa maafa makubwa kwa watu na mali zao. Na huo ukawa ni mwisho wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, kielelezo cha: ukatili wa hali ya juu kabisa, ubinafsi na utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko. Silaha za nyuklia bado ni tishio kubwa kwa: amani, usalama, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi duniani. Watu wengi walipoteza maisha kutokana na kiu iliyosababishwa na mionzi mikali ya silaha za nyuklia. Japan inatambua fika madhara ya vita na matumizi ya silaha za nyuklia; maafa ya tetemeko kubwa la ardhi na tsunami iliofuatia vilisababisha vifo vya watu zaidi ya 20,000 nchini Japan. Uharibifu uliosababishwa kwenye mtambo wa nyuklia wa Fukushima Daichi ukapelekea maafa makubwa kwa watu na mali zao. Haya ni mambo ambayo bado yameacha kumbukumbu hai katika maisha ya wananchi wa Japan. Ni muda muafaka wa kuadhimisha kumbukizi ya Miaka 80 tangu miji ya Hiroshima na Nagasaki iliposhambuliwa kwa mabomu ya nyuklia ili kuendelea kuombea: umoja, amani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Leo hii, bado kuna vita baridi, amani inaendelea kutishiwa kwa sababu ya utengenezaji na ulimbikizaji wa silaha za nyuklia sanjari na athari za mabadiliko ya tabianchi. Mashambulizi ya silaha za nyukilia si jambo la kufikirika hata kidogo, kwa sababu hata wakati huu, kuna mashindano ya utengenezaji na ulimbikizaji wa silaha za nyuklia, hali inayotishia usalama, amani na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa.
Bado kuna vitisho vya mashambulizi ya silaha za nyuklia, kuna vitendo vya kigaidi ambavyo ni kinyume kabisa cha uhuru wa kuabudu, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Zaidi ya hayo, kuna mashindano ya biashara ya silaha duniani, ambayo ni chanzo cha vita, kinzani na migogoro sehemu mbalimbali za dunia. Kuna baadhi ya nchi zinapenda sera za kutengeneza, kumiliki na kulimbikiza silaha za nyuklia kama mpango mkakati wa masuala ya kisiasa. Lakini ikumbukwe kwamba, utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za nyuklia kwa ajili ya vita ni kinyume cha kanuni maadili na utu wema! Ni katika muktadha wa kumbukizi ya Maadhimisho ya Miaka 80 tangu miji ya Hiroshima na Nagasaki iliyoko nchini Japan iliposhambuliwa kwa mabomu ya nyuklia Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake, anayaelekeza macho yake kwa Wahanga wa mashambulizi ya silaha za nyuklia nchini Japan, “Hibakusha” ambao ni kielelezo na ushuhuda wa watu wanaotaka ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kuona kwamba, dunia inakuwa huru dhidi ya vitisho vya mashambulizi ya kinyuklia. Hawa ni watu walioguswa na hatimaye kutikiswa na mashambulizi haya, changamoto na mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kujenga na kudumisha mazingira ya haki, amani na usalama. Miji ya Hiroshima na Nagasaki ni kumbukumbu hai ya madhara ya Mashambulizi ya Vita Kuu Pili ya Dunia yaliyotokea Mwezi Agosti 1945 na kwamba, barabara, shule na nyumba nyingi bado zinazonesha makovu ya Vita kuu ya Pili ya Dunia na kama alivyowahi kusema Hayati Baba Mtakatifu Francisko kwamba, vita ni dalili za kushindwa kwa binadamu. Mtu mwenye upendo wa kweli hana sababu ya kubeba silaha na kwamba, amani ya kweli inasimikwa katika ujasiri wa kuweka pembeni silaha na hasa zile silaha za maangamizi zinazoweza kusababisha maafa makubwa kwa wat una mali zao.
Silaha za nyuklia ni kinyume kabisa cha ubinadamu na kina saliti utu, heshima na kazi ya uumbaji na kwamba, binadamu wote wanahimizwa kulinda na kutunza amani na utulivu. Miji ya Hiroshima na Nagasaki ni kumbukumbu endelevu inayoitaka Jumuiya ya Kimataifa kuachana na ndoto inayosimikwa katika maangamizi na badala yake, Jumuiya ya Kimataifa ijikite katika haki, udugu wa kibinadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, kumbukizi hii ya Miaka 80 tangu miji ya Hiroshima na Nagasaki ishambuliwe kwa bomu la nyuklia, inakuwa ni nafasi kwa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti katika mchakato wa kutafuta na kudumisha amani ya kudumu kwa familia yote ya binadamu na kuendelea kujikita katika amani. Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV amewapatia baraka zake za kitume watu wote waliohudhuria katika kumbukizi hii.
Naye Kardinali Blase Joseph Cupich, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Chicago nchini Marekani katika mahubiri yake, kama sehemu ya kumbukizi ya miaka 80 tangu miji ya Hiroshima na Nagasaki ishambuliwe anasema kwamba, shambulizi hili lilikiuka masharti ya Sheria na Mikataba ya Kimataifa na kwamba, kanuni maadili na utu wema haukuzingatiwa. Lengo la shambulizi hili lilikua ni kusitisha Vita Kuu ya Pili ya Dunia haraka iwezekanavyo. Marekani ilidhani kwamba, kwa kutumia bomu la nyuklia, ingeweza kupunguza madhara yake kisaikolojia ikilinganishwa na miji mingine iliyokuwa imeathirika vibaya kwa vita. Huu ni uamuzi uliotolewa na Rais Harry Truman wa Marekani. Watu wengi wanasikitishwa na madhara yaliyotokea kutokana na shambulio la miji ya Hiroshima na Nagasaki. Hii ndiyo hofu inayotanda pale Jumuiya ya Kimataifa inaposikia Iran anataka kutumia silaha za nyuklia.
Hii ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika kanuni maadili na utu wema pamoja na Sheria za Kimataifa, kwa kushinda: chuki, uhasama, ukabila na utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko. Upokonyaji silaha kwa ujumla na kamili chini ya udhibiti mkali na mzuri wa Jumuiya ya Kimataifa ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele cha pekee, ili kukuza na kudumisha usalama na amani ya kweli. Umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kusitisha mashindano ya utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za maangamizi, Marekani inapaswa kuonesha mfano bora wa kuigwa. Marekani, Urusi, Uingereza, China, Ufaransa, India, Pakistan, Israel, na Korea Kaskazini zinajulikana kumiliki silaha za nyuklia, ingawa Israel ndiyo pekee kati ya hizi ambayo haijawahi kuthibitisha rasmi hili. Marekani imekuwa nchi ya kwanza yenye nguvu za nyuklia baada ya kutengeneza silaha hizo kwa siri kama sehemu ya Mradi wa Manhattan wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Kwa kujibu, Umoja wa Mataifa ulianzisha Mkataba wa Kuzuia Uenezaji (NPT), uliopangwa kuzuia kuenea zaidi kwa silaha za nyuklia, kukuza upokonyaji silaha, na kuwezesha matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia. Mkataba huo ulianza kutumika mnamo 1970, lakini sio nchi zote zilitia saini, na silaha za nyuklia zilienea. Takwimu zinaonesha kwamba kuna silaha kati ya 10, 500 hadi 12, 300 sehemu mbalimbali za dunia zinazotishia usalama, amani na maisha ya binadamu.
Kumbe, kuna haja anasema Kardinali Blase Joseph Cupich, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Chicago nchini Marekani kwa nchi zenye silaha za kinyuklia kuwajibika kikamilifu ili kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya vitisho vya utamaduni wa kifo. Wahanga wa mashambulizi ya silaha za nyuklia nchini Japan, “Hibakusha” ni sauti ya kinabii, mashuhuda na vyombo vya amani. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika ujenzi wa mazingira yatakatosaidia kuzuia kuenea zaidi kwa silaha za nyuklia, kukuza upokonyaji silaha, na kuwezesha matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia sehemu mbalimbali za dunia pamoja na kuhakikisha kwamba, kamwe Jumuiya ya Kimataifa isitumbukizwe katika matumizi ya silaha za maangamizi na badala yake, majadiliano katika ukweli na uwazi na diplomasia ya Kimataifa itumike kutafuta suluhu ya amani.