Papa Leo XIV- Taasisi za serikali na kimataifa zinaposhindwa,jumuiya za kidini na kiraia lazima zithubutu kutoa unabii
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV alituma ujumbe wake tarehe 21 Agosti 2025 kwa Askofu Nicolo Anselmi wa Jimbo Katoliki la Rimini katika fursa ya Toleo la 46 la Mkutano wa Urafiki kati ya Watu, ambalo uhamisishwa kila mwaka na Harakati ya Kikanisa na ‘Comunione e libarazione’ yaani “Ushirika na Ukombozi” unaofunguliwa tarehe 22 Agosti 2025. Katika ujumbe huo uliotiwa saini na Katibu Mkuu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin alianza kuwa Mada ya Mkutano huo utakaofanyika siku zijazo ni mwaliko wa matumaini: "Katika maeneo ya jangwa tutajenga kwa matofali mapya."
Baba Mtakatifu Leo XIV anatoa salamu zake kwa waandaaji, watu wa kujitolea, na washiriki wote, kwa matumaini kwamba watatambua kwa furaha kwamba jiwe lililokataliwa na wajenzi limewekwa kuwa "jiwe la pembeni, teule, la thamani; na kila aaminiye hatatahayarika" (rej. 1Pet 2:6). Tumaini, kwa kweli, halikatishi tamaa (taz. Rm 5:5). Majangwa kwa ujumla ni maeneo yaliyokataliwa na kuchukuliwa kuwa hayafai katika maisha. Hata hivyo, pale inapoonekana kwamba hakuna kitu kinachoweza kuzaliwa, Maandiko Matakatifu huendelea kurudi ili kusimulia vifungu vya Mungu. Katika jangwa, kwanza kabisa, watu wake wanazaliwa. Hakika, ni kwa kusafiri tu kupitia ukali wake ndipo uchaguzi wa uhuru hukomaa. Mungu wa Kibiblia—ambaye hutazama, kusikiliza, na kujua mateso ya watoto wake na kushuka chini ili kuwaweka huru ( Kutoka 3:7-8)—hubadilisha jangwa kuwa mahali pa upendo na maamuzi, na kuifanya isitawi kama bustani ya matumaini. Manabii wanalikumbuka kama mpangilio wa uchumba, ambapo wanarudi kila wakati mioyo yao inapopoa, ili kuanza upya kutoka kwa uaminifu wa Mungu (Hos 2:16).
Wamonaki na watawa katika jangwa kwa ajili ya kutuwakilisha sote mbele ya Bwana
Kwa milenia, mamonaki na watawa wamekaa jangwani kwa niaba yetu sote, wakiwakilisha wanadamu wote, mbele ya Bwana wa ukimya na uzima. Baba Mtakatifu ameshukuru kwamba moja ya maonesho ya Mkutano wa mwaka huu 2025 ni wa ushuhuda wa mashahidi wa Algeria. Ndani yao unaangaza wito wa Kanisa wa kukaa jangwani katika ushirika wa kina na wanadamu wote, wakishinda kuta za kutoaminiana zinazopinga dini na tamaduni, kwa kuiga kikamilifu vuguvugu la kufanyika mwili na kujitoa kwa Mwana wa Mungu. Njia hii ya uwepo na usahili, ya maarifa na "mazungumzo ya maisha," ndiyo njia ya kweli ya utume. Sio onyesho la kibinafsi, katika mchanganyiko wa utambulisho, lakini kujitolea hadi kufa kwa wale wanaomwabudu Yesu peke yake kama Bwana mchana na usiku, katika furaha na katikati ya dhiki.
Jumuiya za kidini na za kiraia zithubutu kutoa unabii
Katika barua hiyo kwa Mwashamu Askofu Nicolò Anselmi, Askofu wa Rimini, Baba Mtakatifu anabainisha kuwa Kama ilivyo desturi, kutakuwa na mazungumzo kati ya Wakatoliki wenye mitazamo tofauti na wamini wa madhehebu mengine na wasioamini. Haya ni mazoezi muhimu katika kusikiliza, ambayo hutayarisha "matofali mapya" ambayo kwayo tutajenga wakati ujao ambao Mungu tayari ameweka kwa ajili ya wote, lakini ambao unafunuliwa tu kwa kukaribishana. Hatuwezi tena kumudu kuupinga Ufalme wa Mungu, ambao ni Ufalme wa amani. Na pale ambapo wale wanaohusika na taasisi za serikali na kimataifa wanaonekana kushindwa kutekeleza sheria, upatanisho, na mazungumzo, jumuiya za kidini na jumuiya za kiraia lazima zithubutu kutoa unabii. Hii ina maana kuruhusu sisi wenyewe kuendeshwa katika jangwa na kuona nini sasa kinaweza kutokea kutoka katika kifusi na kutokana na mateso mengi sana, ya wasio na hatia.
Mungu alichagua wanyenyekevu kwa njia ya tumbo la Bikira Maria
Papa Leo XIV aliwahimiza maaskofu wa Italia "kukuza programu za elimu katika kutotumia nguvu, mipango ya upatanisho katika migogoro ya ndani, na mipango ya kukaribisha ambayo inabadilisha hofu ya wengine kuwa fursa za kukutana." Na anatuomba tena: "Kila jumuiya na iwe "nyumba ya amani", ambapo tunajifunza kuondosha uadui kupitia mazungumzo, ambapo haki inafanywa na msamaha unalindwa. Amani sio utopia wa kiroho: ni njia ya unyenyekevu, inayofanywa kwa ishara za kila siku, ambayo huingiliana na uvumilivu na ujasiri, kusikiliza na kutenda. Na leo hii, zaidi ya hapo awali, inadai uwepo wetu mtazamo na wa kuzaa” (Hotuba kwa Maaskofu wa Baraza la Maaskofu wa Italia, Juni 17, 2025). Kwa hiyo, Baba Mtakatifu anatuhimiza kutoa jina na umbo jipya, ili imani, matumaini na mapendo viweze kutafsiri katika uwongofu mkuu wa kiutamaduni. Papa wetu mpendwa Francisko alitufundisha kwamba "chaguo kwa maskini ni kategoria ya kitaalimungu kabla ya kuwa ya kitamaduni, kijamii, kisiasa, au kifalsafa" (Evangelii Gaudium, 198). Mungu, kiukweli, alichagua wanyenyekevu, wadogo, wasio na nguvu, na, kutoka kwa tumbo la Bikira Maria, akawa mmoja wao, kuandika historia yake katika historia yetu. Uhalisia halisi, basi, ni ule unaojumuisha wale "wanaoshikilia mtazamo mwingine, ambao wanaona vipengele vya ukweli ambavyo havitambuliwi na vituo vya mamlaka ambapo maamuzi ya uamuzi zaidi hufanywa" (Fratelli tutti, 215).
Maendeleo kwa njia za usawa na ushiriki wa wote
Baba Mtakatifu Leo anabainisha kuwa bila wahanga wa historia, bila wale wenye njaa na kiu ya haki, bila wapenda amani, bila wajane na yatima, bila vijana na wazee, bila wahamiaji na wakimbizi, bila kilio cha viumbe vyote, hatutakuwa na matofali mapya. Tutaendelea kufuata ndoto ya upotovu ya Babeli, tukijidanganya kwamba kugusa mbingu na kujitengenezea jina kuwa ndiyo njia pekee ya mwanadamu ya kuishi duniani ( Mwa 11:1-9). Tangu mwanzo, hata hivyo, kukataa sauti za wengine na kukataa kuelewana ni uzoefu wa kupotosha na kudhalilisha hadhi. Uzoefu huu lazima ukabiliwe na uvumilivu wa kukutana na Siri inayobadilika kila wakati, ambayo tofauti ya kila mtu ni ishara. Bila silaha na kupokonywa silaha, uwepo wa Wakristo katika jamii za kisasa lazima kwa umahiri na kimawazo kutafsiri Injili ya Ufalme katika aina za maendeleo badala ya njia za ukuaji zisizo na usawa na uendelevu. Ili kumtumikia Mungu aliye hai, ni lazima tuache ibada ya miungu ya faida, ambayo imeathiri sana haki, uhuru wa kukutana na kubadilishana, ushiriki wa wote katika manufaa ya wote, na hatimaye amani. Imani inayojitenga na hali ya jangwa ya ulimwengu, au ambayo inachangia kwa njia isiyo ya moja kwa moja kuivumilia, haitakuwa tena mfuasi wa Yesu Kristo. Mapinduzi ya kidijitali yanayoendelea yanahatarisha kuzidisha ubaguzi na migogoro: kwa hiyo ni lazima ukumbwe na ubunifu wa wale ambao, wakimtii Roho Mtakatifu, si watumwa tena, bali watoto. Kisha jangwa linakuwa bustani, na “mji wa Mungu,” uliotabiriwa na watakatifu, unageuza sura zetu za ukiwa.
Baba Mtakatifu Leo anaomba maombezi ya Bikira Maria, Nyota ya Asubuhi, ili kuunga mkono dhamira ya kila mtu katika ushirika na Wachungaji wao na jumuiya za kikanisa ambamo wamejumuishwa: “Katika harambee pamoja na washiriki wengine wote wa Mwili wa Kristo, basi tutatenda kwa maelewano. Changamoto zinazowakabili ubinadamu hazitakuwa za kuogofya sana, siku zijazo zitakuwa giza kidogo, utambuzi utakuwa mgumu sana. Ikiwa pamoja tunamtii Roho Mtakatifu!"Na kwa upande wa Kardinali Parolin alisema: “ Ninapoungana kwa moyo wote na wale ambao wa Baba Mtakatifu na kuwatakia mema binafsi, ninachukua fursa hii kutoa heshima zangu za dhati, Mwashamu Askofu kwa kujitolea