Papa leo XIV: Sikukuu ya Kung'ara Bwana: Nuru ya Matumaini na Faraja
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mababa wa Kanisa wanasema, haikuwa rahisi kwa Mtakatifu Petro kukubali Fumbo la Pasaka, yaani, mateso, kifo na ufufuko kwa Kristo Yesu kutoka kwa wafu; hii ilikuwa ni kashfa ya Fumbo la Msalaba. Kristo Yesu anawaandaa Mitume wake kuweza kukabiliana na Kashfa ya Msalaba kwa kugeuka sura, kutokea kwa Musa na Eliya yaani: Utimilifu wa Unabii na Sheria na ushuhuda wa sauti kutoka mbinguni ikisema, “Huyu ni Mwanangu, mteule wangu msikieni Yeye. Rej. Lk 9:31. Huu ni mwaliko kwa waamini kutafakari utukufu wa Kristo Yesu, Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, ili wanapomwona ametundika Msalabani watambue kwamba, mateso yake yalikuwa ni ya hiari, wawe tayari kutangaza na kushuhudia kwamba, Kristo Yesu ni Mng’ao wa Baba wa milele. Kwa Ubatizo, mwamini anazaliwa mara ya pili na hivyo kushiriki katika Ufufuko wa kristo Yesu kwa njia ya Roho Mtakatifu anayefanya kazi katika Sakramenti za Mwili wa Kristo. Kung’ara sura ni limbuko la ujio mtukufu wa Kristo Yesu, atakaye ubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu. Waamini wataufikia pia utukufu wa Kristo Yesu kwa njia ya Fumbo la Msalaba. Rej. KKK 554-556.Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Katekesi yake kuhusu Fumbo la Pasaka, Jumatano tarehe 6 Agosti 2025 amewakumbusha waamini kwamba, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Kung’ara Bwana. Uso wa Bwana unaong’ara, uwe ni chemchemi ya matumaini na faraja kwa waja wake. Baba Mtakatifu amewaombea waamini wote zawadi na karama ya Roho Mtakatifu, ili ziwasaidie kuwa ni mashuhuda wakarimu wa tunu msingi za maisha ya Kikristo! Huu ni mwaliko kwa waamini kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu, ili liweze kuangaza hatua na maisha yao kama waamini, ili hatimaye, Kristo Yesu aweze kung’ara ulimwenguni. Waamini wajenge utamaduni wa kumsikiliza Kristo Yesu anapoongea nao kwa njia ya Maandiko Matakatifu na hivyo kuwa tayari kupokea ukweli kuhusu Mungu na utekelezaji wake unaopata chimbuko lake kutoka katika undani wa moyo wa mwanadamu.
Baba Mtakatifu Benedikto XVI, akifanya tafakari kuhusu Sikukuu ya Kung’ara Bwana anasema kwamba, huu ni muhtasari wa Mafumbo ya Imani ya Kanisa, yaani: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, ili aweze kuwaimarisha wafuasi wake katika hija ya mwanga wa imani. Ni kielelezo cha mshikamano wa dhati kati ya Kristo Yesu na kazi ya uumbaji ambayo ameikomboa kwa njia ya Fumbo la Msalaba. Mama Kanisa katika maadhimisho haya, anaungama kwa dhati kabisa kuhusu: Ubinadamu na Umungu wa Kristo; Kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu na Mkombozi wa dunia sanjari na kuzaliwa kwa Kanisa Sakramenti ya wokovu kwa binadamu! Sherehe hii inagusa kwa namna ya pekee, umuhimu wa Kanisa kusimama kidete kulinda na kutunza kazi ya uumbaji kama anavyokaza kusema Mtakatifu Damascene. Kristo Yesu anaufunua Umungu wake kwa njia ya mwili uliotukuka, ndiyo maana Kanisa linamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa, shukrani na utukufu kwani ukuu una Yeye milele hata na milele! Hii ni changamoto kwa kila mwamini kuhakikisha kwamba, anatoa nafasi kwa mwanga wa imani, ili uweze kumletea mabadiliko ya dhati katika maisha, kwa kuifia dhambi na nafasi zake, ili kutoa fursa ya kuishi katika utu mpya unaofikia hatima yake katika Fumbo la Msalaba wa Kristo. Baba Mtakatifu Benedikto XVI anakaza kusema, huu ni mchakato wa toba na wongofu wa ndani, unaopania kumsafisha na kumtakasa mwamini katika hija ya maisha yake ya kiroho, ili siku moja aweze kuufikia utukufu wa maisha na uzima wa milele. Ni ufunuo wa mwanga utakaozima giza la Kashfa ya Fumbo la Msalaba, tayari kutoa nafasi kwa binadamu kumwabudu, kumsifu, kumtukuza na kumwomba Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kabisa, kuisikiliza sauti ya Mungu na kutekeleza mapenzi yake katika uhalisia wa maisha yao, kwani Neno la Mungu ni dira na mwongozo wa maisha. Neno la Mungu ni Ufunuo wa utambulisho wa Mwana wa Mungu kama siku ile ya Ijumaa kuu atakavyosema yule Akida kwamba, “kwa hakika huyu alikuwa ni Mwana wa Mungu.”
Sikukuu ya Kung’ara sura Bwana wetu Yesu Kristo ni tukio ambalo linaelezwa na Injili tatu: Marko, Mathayo na Luka na linaadhimishwa tarehe 6 Agosti ya kila mwaka. Kristo Yesu akiwa ameambatana na Mitume wake: Petro, Yakobo na Yohane akapanda nao mlimami kusali. Akiwa anasali sura yake ikageuka, ikang’ara na mavazi yake yakawa meupe wanatokea Musa na Eliya. Hawa ni watu muhimu sana katika historia ya Wayahudi. Musa ndiye anayewakilisha Torati, yaani sheria na taratibu zinazoongoza maisha yote ya Wayahudi. Eliya yeye anawakilisha Manabii. Zaidi ya hapo uwepo wa pamoja Musa na Eliya, yaani Torati na Manabii, katika lugha ya kibiblia maana yake ni ufunuo wa Maandiko Matakatifu. Torati na Manabii ni neno lililotumika kumaanisha Maandiko Matakatifu katika Agano la Kale. Mwisho wa tukio hilo ni kwamba linashuka wingu na ndani ya wingu hilo inasikika sauti ikisema: “Huyu ni mwanangu mpendwa msikieni Yeye.” Wingu na sauti hii ni ile ile iliyosikika siku ya ubatizo wa Yesu. Wingu ni alama ya uwepo wa Mungu kumbe sauti hiyo inayosikika inaonekana moja kwa moja kuwa ni ushuhuda wa sauti ya Mungu: “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye.” Mk 9:7: Haya pia ni maandalizi ya ufunuo wa Siku ya Mwisho, atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Tukio hili linaonesha mabadiliko ambayo Kristo Yesu aliyapata daima alipokuwa akisali na kuzungumza na Baba yake wa mbinguni. Linaonesha utukufu wa Mungu ambao daima ulifichika katika ubinadamu wake na linaonesha utukufu ambao Yesu na wote wanaomwamini wataupata baada ya adha ya Msalaba na mahangaiko ya maisha ya duniani; linaonesha Yesu kama utimilifu wa Torati na Manabii na linaagiza kumsikiliza yeye, yaani kulipokea Neno lake na kuliishi kama wafuasi wake. Ni katika muktadha huu, Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Sikukuu ya Kung’ara Bwana tarehe 6 Agosti 2024 aliwaalika waamini akisema, “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Msikieni yeye.” Mt 17:5. Siri ya maisha inasimikwa katika utamaduni wa kumsikiliza Kristo Yesu kwa umakini mkubwa. Chukua Injili, soma na sikiliza kile ambacho Kristo Yesu anataka kukuambia katika roho yako, kwa sababu Kristo Yesu anayo maneno ya uzima wa milele.
Katika maadhimisho ya Sikukuu ya Kung’ara Bwana, Kanisa kwa mwaka huu, 2025, linafanya kumbukizi ya miaka 47 tangu Mtakatifu Paulo VI alipofariki dunia, akiwa kwenye Ikulu ndogo ya Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma na kuzikwa tarehe 12 Agosti 1978 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Mtakatifu Paulo VI anasema, Sikukuu ya Kung’ara kwa Kristo Yesu inaangaza nuru ya ajabu katika maisha ya kila siku ili kufukuzia mbali giza la kifo linalosumbua akili ya mwanadamu. Mlimani Tabor, Yesu anaufunua utukufu na Umungu wake, mbele ya mashuhuda aliowateuwa mwenyewe yaani Petro, Yakobo na Yohane ili kudhihirisha kwamba, kweli alikuwa ni Mwana mpendwa wa Mungu, Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya Nafsi yake. Rej Mt 17:2. Tukio hili linautukuza ubinadamu wa Kristo Yesu unaofumbatwa katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu! Rej. Mk 8:31-34. Hapa Yesu anadhihirisha utukufu wa Fumbo la Pasaka, kielelezo makini cha sadaka na majitoleo yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, ili hatimaye, aweze kustahilishwa kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru. Mwili uliotukuka mbele ya Mitume wa Kristo Yesu ni mwili wa Kristo na kwamba, hata mwili wa binadamu utapata urithi wa mwanga wa uzima wa milele, kwa kushiriki katika utukufu na kwa njia hii wapate kushiriki tabia ya Uungu kwa kuokolewa na uharibifu ulioko duniani kwa sababu ya tamaa.
Hii ni sehemu ya tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana, iliyokuwa imeandaliwa na Mtakatifu Paulo VI kwa ajili ya Sikukuu ya Kung’ara kwa Yesu, tarehe 6 Agosti 1978, lakini kutokana na homa kali iliyomshika siku hiyo, hakuweza kutokeza mbele ya waamini na matokeo yake, jioni akafariki dunia katika amani ya Baba wa milele! Mtakatifu Paulo VI anakaza kusema, waamini wanasubiri kushirikishwa utukufu wa Mungu ambao walianza kuutafuta kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Mtakatifu Paulo VI katika tafakari yake, aliwakumbuka hata wale ambao kutokana na sababu mbalimbali walikuwa wanateseka, ili nao, hata katika hali na mazingira kama haya, waweze kupata walau mwanya wa mapumziko. Hawa ndio wale watu wasiokuwa na fursa za ajira, kiasi hata cha kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu katika familia na jamii katika ujumla wake. Ni watu wanaoteseka kutokana na umaskini na baa la njaa sehemu mbalimbali za dunia pamoja na wale wote walioathirika kutokana na sera na mikakati tenge ya uchumi na maendeleo jamii. Kutokana na mahitaji msingi ya umati wote huu, Kanisa linapenda kumtolea Bikira Maria sala na maombi yake, ili aweze kusaidia kuombea umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu.