Papa Leo XIV:kuutambua uovu ni fursa ya kuzaliwa upya!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika Katekesi ya Baba Mtakatifu Leo XIV iliyofanyika Jumatano tarehe 13 Agosti 2025 iliyofanyika katika Ukumbi wa Paulo wa VI, badala ya Uwanja wa Mtakatifu Petro, kutokana na kuongeza kwa jua kama ilivyokuwa imetarajiwa, kabla ya kuingia aliwasalimia wale waliokuwa wamekusanyika nje katika Uwanja wa Patriano: Buongiorno a tutti, buenos dias, bom dia, tutaonana baada ya Katekesi, tutapita tena hapa. Mungu awabariki.” Mara baada ya kufika katika Ukumbi wa Paulo VI, saa 4.00 kamili masaa ya Ulaya na saa 5 katika saa za Afrika Mashariki aliwaelekea waamini na mahujaji wote kwa lugha ya kiingereza, kihispania na kiitaliano.
Kwa kiingereza alisema: “Asubuhi hii tutakuwa na watazamaji katika sehemu kadhaa, katika nyakati tofauti ili kukaa kidogo nje ya jua na joto kali. Tunakushukuru kwa subira yenu na tunamshukuru Mungu kwa zawadi nzuri ya uhai, hali ya hewa nzuri na baraka zake zote.”
Kwa kispanyola Papa alisema: “Kwa hiyo, tutashiriki na wasikilizaji asubuhi ya leo katika sehemu mbili, kwa sababu kuna watu hapa jirani, watu katika Kanisa, na pia katika Uwanja. Karibu, kila mtu. Na kidogo kidogo, tutasalimia vikundi vyote haraka iwezekanavyo.”
Kwa lugha ya kiitalianao, Baba Mtakatifu alisema: “Kwa hivyo, leo tunafanya katekesi hii kwa nyakati hizi tofauti, katika sehemu ili kujikinga na jua, kutokana na joto kali. Asante kwa kufika. Karibuni nyote.”
Papa akianza Katekesi yake alisema "tuendelee katika Shule ya Injili kwa kufuata nyayo za Yesu katika siku zake za mwisho wa maisha yake. Leo tunatafakari tukio la karibu, la kushangaza, lakini la kweli kabisa: Karamu kuu ya Pasaka wakati Yesu alifunua kwamba mmoja wa wale Kumi na Wawili alikuwa karibu kumsaliti: "Amin, nawaambia, mmoja wenu, ambaye anakula pamoja nami, atanisaliti"(Mk 14:18). Maneno yenye nguvu. Yesu hawasemi ili kuwashutumu, bali kuonesha jinsi ambavyo upendo, wakati ni wa kweli, hauwezi kupuuza ukweli. Chumba cha karamu kuu, ambapo muda mfupi kabla ya kila kitu kilitayarishwa kwa uangalifu, ghafla kilijazwa na uchungu wa kimya, unaojumuisha maswali, mashaka, na mazingira magumu."
Papa alisisitiza kuwa lakini ni uchungu ambao pia tunaujua vizuri, wakati kivuli cha usaliti kinapoingia kwenye uhusiano wa karibu zaidi. Na bado, tunaona jinsi ambavyo Yesu alivyozungumza kuhusu yale ambayo yanakaribia kutokea yanashangaza. Haamshi sauti, haonyoshei kidole, hataji jina la Yuda. Anazungumza kwa namna ambayo kila mtu anaweza kujiuliza. Na hiyo ndiyo hasa ilitokea. Mtakatifu Marko anatuambia: “Wakaanza kuhuzunika, na kumuuliza mmoja baada ya mwingine, Je ni mimi?
Papa Leo XIV alikazia kusema: swali hili, “Je, ni mimi?”, labda ni mojawapo ya lile nyoofu zaidi tunaweza kujiuliza. Sio swali la wasio na hatia, lakini la mwanafunzi ambaye anagundua udhaifu wake mwenyewe. Sio kilio cha wenye hatia, lakini kunong'ona kwa mtu ambaye, akitaka kupenda, anajua anaweza kuumiza. Ni katika ufahamu huu ambapo njia ya wokovu huanza. Yesu hasemi kufedhehesha. Anasema ukweli kwa sababu anataka kuokoa. Na ili kuokolewa, ni lazima tujisikie: kuhisi kwamba tunahusika, kuhisi kwamba tunapendwa licha ya kila kitu, kuhisi kwamba uovu ni halisi lakini hauna neno la mwisho. Ni wale tu ambao wamejua ukweli wa upendo wa kina wanaweza pia kukubali jeraha la usaliti. Mwitikio wa wanafunzi si hasira, bali huzuni. Hawana hasira, wana huzuni. Ni maumivu yanayotokana na uwezekano halisi wa kuhusika.
Papa Leo XIV alifafanua kuwa “Na huzuni huu, ikiwa unakubaliwa kwa dhati, unakuwa mahali pa uongofu. Injili haitufundishi kuukana uovu, bali kuutambua kuwa ni fursa chungu ya kuzaliwa upya. Kisha Yesu aliongeza msemo unaotusumbua na kutufanya tufikiri: “Ole wake mtu yule ambaye Mwana wa Adamu anasalitiwa naye!(Mk 14:21 ). Haya ni maneno makali, kwa hakika, lakini lazima ieleweke kwa usahihi: sio laana, bali ni kilio cha maumivu. Katika Kigiriki, "ole" hiyo inasikika kama maombolezo, "ole," mshangao wa huruma ya dhati na ya kina. Tumezoea kuhukumu. Hata hivyo, Mungu anakubali kuteseka. Anapoona ubaya, halipizi kisasi, bali uhuzunika. Na aliongeza kusema kwamba "ingekuwa afadhali kama hangezaliwa kamwe" sio hukumu iliyotolewa kwa kipaumbele, lakini ni ukweli ambao kila mmoja wetu anaweza kuutambua: ikiwa tunakataa upendo uliotuumba, ikiwa kwa kuusaliti tunakuwa wasio waaminifu kwetu wenyewe, basi tunapoteza maana ya kuletwa kwetu duniani na kujitenga wenyewe kutoka katika wokovu.
Hata hivyo, Papa aliongeza kusema “pale pale, mahali penye giza zaidi, nuru haizimiki. Badala yake, huanza kuangaza. Kwa sababu ikiwa tunatambua mapungufu yetu, ikiwa tunajiruhusu kuguswa na maumivu ya Kristo, basi tunaweza kuzaliwa mara ya pili. Imani haituzuii sisi kutokuwa na dhambi, bali daima hutupatia njia ya kutokea: ile ya huruma. Yesu hakashifu mbele ya udhaifu wetu. Anajua vizuri kwamba hakuna urafiki ambao hauwezekani na hatari ya usaliti. Lakini Yesu anaendelea kutumaini. Anaendelea kukaa mezani na wenzake. Haachi kumega mkate, hata kwa wale ambao watamsaliti. Hii ndiyo nguvu ya kimya ya Mungu: yeye kamwe haachi meza ya upendo, hata wakati anajua kuwa ataachwa peke yake.
Papa Leo XIV, alisisitiza kuwa “ sisi pia tunaweza kujiuliza leo, kwa dhati: "Je, ni mimi?" Sio kuhisi kushtakiwa, lakini kufungua nafasi katika ukweli katika mioyo yetu. Wokovu unaanzia hapa: kutokana na ufahamu kwamba tunaweza kuwa watu wa kuvunja imani kwa Mungu, lakini kwamba tunaweza pia kuwa wale wa kuikusanya, kuilinda, na kuifanya upya. Hatimaye, hili ni tumaini: tukijua kwamba, hata kama tunaweza kushindwa, Mungu kamwe hashindwi. Hata kama tunaweza kusaliti, Yeye haachi kutupenda. Na ikiwa tutajiruhusu kufikiwa na upendo huu, wanyenyekevu, wenye kujeruhiwa, lakini waaminifu daima, basi tunaweza kweli kuzaliwa upya. Na tuanze kuishi tena kama wasaliti, bali kama watoto ambao wanapendwa kila wakati," alihitimisha, Baba Mtakatifu.
Salamu za Papa baada ya Katekesi,
Baba Mtakatifu Leo XIV, mara baada ya Katekesi yake alitoa salamu kwa lugha mbali mbali ambapo kwa lugha ya kiitaliano alisema: “Ninawakaribisha kwa moyo mkunjufu mahujaji wanaozungumza Kiitaliano. Kwa namna ya pekee, ninawasalimia washiriki wa Mkutano Mkuu wa Mabinti wa Msalaba. Pia ninawasalimu waamini wa Verona, Modena, na Manerbio, nikiwatia moyo kila mmoja kufanya maendeleo katika uadilifu na usafi wa imani na maisha.” Hatimaye, Papa Leo XIV, mawazo yake yaliwaendea wagonjwa, wenye ndoa ambao aliomba wawapigie makofi, “kwa wenzi wote wapya na vijana, hasa wale wanaoshiriki katika Kambi ya Kimataifa ya Shirika la Vijana la “Giorgio La Pira”.
Papa akielekeza mawazo ya Sherehe ijayo ya Bikira Maria alisema “ Maadhimisho ya Kupalizwa mbinguni yanapokaribia, ninayo furaha kuwasihi muelekeze daima sala zenu kwa Bikira Maria, kwa kufuata kielelezo chake katika kukumbatia kikamilifu wito wa “kuzoeana” na Mungu na kujali kila mwanamume na mwanamke.Baraka kwa wote.”
Papa hatimaye, kama ilivyokuwa imepangwa, alikwenda katika Basilika ya Mtakatifu Petro, kuwasalimia hata waamini na mahujaji waliokuwa wanamsubiri na ambao walifuatilia katekesi yake. Aliwashukuru na kuwabariki.